Saturday, May 11, 2013

Wakulima 3,000 kunufaika na kilimo shadidi

WAKULIMA 3,000 wa zao la mpunga katika vijiji vinane vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, watanufaika na mfumo wa kilimo shadidi (System of Rice Intensification (SRI) kuanzia msimu ujao wa kilimo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Elvin Mwakajinga, alibainisha hayo kwenye maadhimisho ya Siku ya Mkulima yaliyofanyika katika Kijiji cha Makifu na kuwakutanisha baadhi ya wakulima wa mpunga wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Mbarali, mkoani Mbeya na Iringa.
“Kunufaika kwa wakulima hao ni matokeo ya mafunzo ya kuanzishwa kwa mfumo huo katika Wilaya ya Iringa yaliyoendeshwa kwa wakulima 512 na Taasisi ya Maendeleo Mijini na Vijijini (RUDI) Novemba, mwaka jana na kufuatiwa na mashamba darasa 50 msimu huu wa kilimo,” alisema Mwakajinga.
Mwakajinga alisema ni jambo jema kwa mfumo huo kuwafikia wakulima wengi na ikiwezekana wote na kuwataka watendaji wa vijiji na kata kuanzisha na kufufua vikundi vya wakulima, ili wawe na nguvu ya pamoja.
Mtendaji Mkuu wa RUDI, Abel Lyimo, alisema katika maeneo ambayo mfumo tayari unatumika kama Kilombero na Mbarali, uzalishaji umefikia magunia 40 kwa ekari moja.
Kwa upande wao, wakulima hao walisema mfumo utawasaidia kuongeza kipato cha kaya na taifa kwa jumla na kuiomba serikali kusaidiana na taasisi ya RUDI kueneza mfumo huo kwa wakulima wote nchini.

Waziri Chiza kuzindua bodi mpya ya kahawa

 
Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), itazinduliwa wiki ijayo mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Astery Bitegeko, alithibitisha jana kuwa uzinduzi wa bodi hiyo ambao umepokewa kwa furaha na wakulima wa kahawa nchini utafanyika Jumatano ijayo.
Kuvunjwa kwa bodi ya awali kulitokana na malalamiko kutoka kwa wakulima akiwamo Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyedai uteuzi wake ulikiuka sheria ya kahawa ya mwaka 2001.
Wajumbe wapya wa bodi hiyo ni Dk Juma Ngasongwa anayekuwa mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Adolf Kumburu anayekuwa katibu wa bodi hiyo.
Wengine na taasisi wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Novatus Tiigelerwa (Kdcu), Profesa Suleiman Chambo (Muccobs), Thahir Nzalawahe na Philip Mbogela kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Profesa Chambo na Mbogela wameingia katika bodi hiyo kama wataalamu wa zao la kahawa linalokabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kuongeza uzalishaji, ubora na kusaka masoko mapya.
Wajumbe wengine ni Fatima Faraji (TCGA), Hyasinth Ndunguru (Kimuli Amcobs), Amir Hamza (TCA) na Maynard Swai kutoka Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU).

Thursday, May 9, 2013

KILIMO BORA CHA MAHINDI

Mahindi ni chakula muhimu na ni aina ya nafaka katika mataifa ya Afrika yaliyomo kusini mwa jangwa la Sahara. Ni chakula cha matumizi ya nyumbani kwa idadi ya watu inayokadiriwa kuwa asilimia 50. Ni chanzo muhimu cha madini na kuongeza nguvu mwilini, protini, madini ya chuma (iron) vitamini na madini mengine asilia.Waafrika hutumia mahindi kwa njia mbalimbali – (uji, ugali na pombe). Na mahindi ya kuchoma. Kila sehemu ya mmea wa mahindi ina thamani kiuchumi : punje, majani, shina na magunzi huweza kutoa kiasi kikubwa cha bidhaa nyinginezo zilizo chakula na zisizokuwa chakula.

Vile vile mahindi ni chakula muhimu cha mifugo (ng’ombe) na huhifadiwa kama silage. Pia mabaki ya mimea na nafaka na pia hutumika viwandani kutengeneza wanga na mafuta.
Mahitaji ya mahindi katika hali ya hewa, udongo na Mahindi ni mimea ambayo hustahimili mabadiliko mengi ya hali ya hewa na humea katika maeneo mengi tofauti. Kuna aina nyingi za mahindi yanayotofautiana katika muda wa kukomaa, mahindi huwa na ustahimili mkubwa kwa mabadiliko katika kiwango cha joto. Mahindi haswa huwa mimea ya maeneo ya joto ambako unyevu ni wa kutosha. Mmea huu unahitaji kiwango cha joto cha kila siku cha nyuzi joto 20º ili umee vyema. Joto la juu sana kwa mazao mazuri ni kama nyuzi joto 30º. Hupandwa sana katika sehemu zilizo katika kimo cha mita 3000 kutoka bahari hadi kwenye ukanda wa pwani. mahindi yaweza kupandwa kama chakula cha mifugo. 

Mahindi huwa yanaathirika na ukosefu wa unyevu wakati wa kutoa maua na matunda. Pia yanahitaji maji ya kutosha wakati wa kupanda. Katika nchi za joto jingi (tropiki), mahindi hufanya vyema katika mvua ya kiwango cha milimita 600 hadi 900 wakati wa kukua. Mahindi yanaweza kukuzwa kwenye aina nyingi za udongo lakini hukua vyema zaidi katika mchanga, usiotuamisha maji mengi, ulio na hewa ya kutosha na ulio na rutuba na madini ya kutosha. Kuwepo kwa mazao mengi ya mahindi kunapelekea kunyonywa sana kwa madini kwenye udongo. Mahindi yaweza kukuzwa katika udongo ulio na hali ya mchanga na (PH) kutoka 5 hadi 8 ingawa 5.5 hadi 7 ndio mwafaka. Mahindi yako katika kikundi cha mimea kinachoaminika kuathirika na hali ya chumvi katika maji na udongo. Kwa vile mimea ambayo ni michanga huwacha sehemu kubwa bila kuzingirwa na ardhi, mmomonyoko wa udongo na kupoteza maji hutokea sana sana hivyo basi ni bora umakini uzingatiwe katika uhifadhi wa udongo na maji kwa kuweka matandazo (mulching).

MATUMIZI YA MBOLEA
Mahindi hustawi zaidi yakiwekwa mbolea, iwapo mambo mengine yanayosaidia katika kukua pia yapo kwa kiwango kinachostahili. Mbolea inayotumiwa na wakulima wadogo mara nyingi huwa haitoshi. Mahindi ya kiwango cha juu yaweza tu kufikia kiwango cha juu cha Uzalishaji iwapo yatapewa lishe na madini ya kutosha. Mahindi ya tani 2 kwa hekta na tani 5 kwa hekta hutumia karibu kilo 60 N, kilo 10 za P205 na kilo 70 K20 kutoka katika udongo. MAhindi hunyonya Nitrogen pole pole katika miezi ya kwanza baada ya kupanda, lakini huongezeka hadi kiwango cha juu kabisa wakati wa kutoa maua na kukuza tunda (gunzi). Mahindi huhitaji nitrogen kwa kiwango cha juu na ukosefu huwa ndio kizingiti. Kiwango cha juu cha nitrogen kinahitajika mara tatu; kwanza wakati wa kupanda, pili, wakati ambapo mmea umefikia sentimita 50 za urefu na tatu, wakati matunda ya mahindi yanaanza kutoa zile nyuzi nyuzi nyororo (silking).

Udongo mwingi huwa na madini ya phosphorous (P205) na potassium (K20) lakini sio kiwango kinachotosheleza mahitaji haswa ya mbegu za mahindi zinapochipua. Nyunyuzia P205 karibu na mbegu ili ziote kwa haraka. K20 hutumika kwa kiwango kikubwa lakini hitaji la mimea hubainika baada ya upimaji wa hali ya udongo kujua kiasi cha mahitaji (soil test).

DALILI ZA UPUNGUFU WA MBOLEA
Ukosefu wa K20 husababisha ncha za majani kuwa na rangi ya njano na kuunda gunzi (cob) lisilo na punje hadi juu. Ukosefu wa P205 hufanya matawi kuwa na rangi ya samawati na mbegu zisizo laini. Dalili za ukosefu wa nitrogen ni majani ya rangi ya manjano na mimea dhaifu mifupi. Phosphate haifyonzwi haraka na mahindi na pia udongo mwingi wa nchi za joto hukosa madini hayo ya phosphate. Inashauriwa unyunyuzie mbolea ya kiasili kama samadi kabla ya kulima ili uboreshe hali ya udongo na kuongezea madini.

Katika ukulima wa kiasili,
(organic farming, Nitrogen (N) hutiwa kwenye udongo kupitia kwa upandaji wa mimea ya jamii ya mikunde (legumes) ambayo hutoa nitrogen katika hewa, Hata hivyo mapendekezo ya kimbolea yaliyo katika misingi ya uchunguzi wa udongo hutoa nafasi nzuri ya kupata kiasi kizuri cha mbolea bila kuweka kiwango cha chini au juu. Omba msaada kutoka kwa mafisa ugani wa kilimo waliyo katika eneo lako.
Katika maeneo yanayo tegemea mvua kukuza mahindi, panda mbegu wakati wa mvua ya kwanza. Hii itaruhusu mizizi kunyonya madini yaliyotengenzwa na bakteria katika udongo. Maji yaliyosimama huyeyusha na kuondoa madini ya nitrogen kutoka katika udongo na kusababisha ukosefu wa Nitrogen.


KUDHIBITI MAGUGU
Udhibiti wa magugu ni muhimu sana. Katika wiki 4 hadi 6 za mbele baada ya kumea, mahindi huathiriwa sana na magugu. Ni lazima mahindi yapandwe mara moja baada ya kutayarisha shamba. Unaweza kulima katikati ya laini za mahindi ili udhibiti magugu. Nchini Tanzania, kupalilia mara mbili kunahitajika kwa aina nyingi za mahindi, ingawa kupalilia kwa mara ya tatu kutahitajika kwa aina ambazo zinahitaji miezi 6 hadi 8 kukomaa. Kupalilia kwa mikono kunahitaji siku 15 kwa hekta la mikono (power tiller) ni masaa mawili mpaka matatu kwa ekari.

UHUSIANO WA NIPE NIKUPE
Desmodium (desmodium uncinatum) nyasi ya Molasses (melinis minutifolia) zikipandwa kati kati ya laini za mahindi huzuia wadudu kama stalk borers moths. Mimea hii hutoa kemikali ambazo huwafukuza wadudu aina stem borers’ moths. Zaidi ya hayo Desmodium huzui gugu haribifu,witchweed striga hermonthica. Napier grass (pennisetum purpureum) na Sudan grass (sorghum vulgare sodanese) ni mimea mizuri sana inayonasa wadudu aina ya stem borers. Napier grass ina njia yake madhubuti ya kujikinga dhidi ya wadudu wanaotoboa mmea kwa kutoa utomvu kutoka kwenye shina, ambayo huzuia wadudu kufyoza mmea na kusababisha uharibifu. Nyasi hizi pia huvutia adui wa stem borers kama mchwa, earwigs na buibui. Nyasi aina ya Sudan pia husaidia maadui asilia, kama nyigu (parasitic wasp)

MAHINDI TAYARI KWA KUVUNWA

Mahindi huweka kivuli kwenye mimea ya mboga mboga ikipandwa safu moja katikati ya mboga kwenye maeneo yaliyo na jua kali. Hii huongeza mazao ya mboga zilizopandwa hivi. na mimea jamii ya mikunde huongeza nitrogen kwenye udongo ambayo huitajika zaidi katika ukuaji wa mahindi pia hupunguza wadudu aina ya (leafhoppers, leafbeatles, stalk borers na fall army worm), upandaji wa mimea jamii ya mikunde ufanyike mara baada ya palizi ya kwanza

UVUNAJI
Uvunaji hufanyika kwa kutumia mikono kwa mashamba madogo na mashine (combine harvester) hutumika kwa ajili ya mashamba makubwa, Zao la wastani la mahindi ulimwenguni mnamo mwaka 2000 lilikuwa kilogramu 4255 kwa kila hekta. Zao la wastani nchini Marekani ilikuwa kilo 8600 kila hekta, huku mataifa yaliyo chini ya jangwa la Sahara la Afrika yakivuna kilo 1316 kwa kila hekta ya shamba. Zao la wastani katika taifa la Tanzania kati ya mwaka 2001-2005 lilikuwa kati ya gunia 15-19 kwa hekta (sawa na kilo 1350-1750) Ukilima kwa kuzingatia ukulima wa kisasa na kanuni zake kwa Tanzania utavuna kilo 5000 kwa hecta (ukanda wa pwani) na kilo 7500 kwa nyanda za juu kama Iringa, Mbeya, Ruvuma, Arusha n.k

Serikali yashauriwa kuboresha kilimo cha mpunga

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEja5ruF1cI73v7-vjmKbFZvJGHMjUWNDco2jXgHKFoCWX-u_w0HjwlRH8abF4vHrJilVQj0cS_G_a1Gw8A35kGMAY0pmVgyFk4fXCyI-AXxklvQ-y0goN3Kc4HGPQ9jjVaIqZP2WpFDfRs/s1600/AA_3356.JPG
SERIKALI imeshauriwa kutumia fedha zinazonunulia mchele toka nje ya nchi kuboresha kilimo cha mpunga hapa nchini. Ushauri huo ulitolewa na Meneja wa Mradi wa Shirika linalojihusisha na Shughuli za Maendeleo Vijijini (RLDC), Francis Massawe.

Alisema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kununua mchele toka nje ya nchi hivyo ni vyema fedha hizo ingezitumia kutoa elimu kwa wakulima namna ya kuboresha kilimo hicho waongeze vipato vyao.


“Ni vyema Serikali ikaliangalia suala hili kwa kina ili kuweza kuwasaidia wakulima wetu hapa nchini kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua na umasikini,” alisema Massawe.

Alisema wakati umefika sasa kwa wakulima kupatiwa mikopo na taasisi za fedha waweze kutumia mbegu bora na pembejeo za kilimo za kisasa kuendana na mazingira ya kilimo bora na cha kisasa.

Aalisema wamejipanga kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya vyakula unaongezeka waweze kuuza nje ya nchi na kuongeza Pato la Taifa.

Alisema wamekuwa wakiwawezesha wakulima na wafugaji kwa kuwapa elimu bora kuhusiana na kilimo na ufugaji ikiwemo kuwapa mikopo.

Alisema mkakati wao ni kuhakikisha wanaongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya vyakula kuuza nje ya nchi na wala si kuagiza mazao toka nje ya nchi
.

Tuesday, May 7, 2013

Wakulima waaswa kuzingatia ushauri wa watafiti, watalaamu

WAKULIMA nchini wametakiwa kuzingatia ushauri wa watafiti na wataalam mbalimbali wa kilimo waweze kuzalisha mazao bora yenye tija katika soko la Afrika Mashariki (EAC).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo (IITA), Dk.Victor Manyong alisema endapo wakulima watazingatia ushauri watazalisha bidhaa bora zenye kukidhi matakwa ya walaji na hatimaye kuzalisha faida itakayowakwamua wao na familia zao.


Alisema IITA imekuwa ikifanya utafiti katika nchi mbalimbali za EAC kwa wakulima wadogo na kwa Tanzania tangu utafiti wa kilimo uanze mwaka 1994 kwa zao la mihogo na imeweza kuwaelekeza wakulima ni mbegu zipi zinafaa kulingana na ardhi yao.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tumejikita katika utafiti mbalimbali na lengo kuu ni kuwasaidia wakulima waweze kulima kilimo cha kisasa kwa kutumia mbegu bora ambazo zitawasaidia kujiongezea kipato na kuachana na tabia ya kulima kwa mazoea,”alisema Manyong.

Alisema si kila mbegu au ardhi inafaa kwa kila zao hivyo kila fursa iliyopo inatumiwa kufanya utafiti na kugawa aina ya mazao yanayoonekana ni bora kwa majaribio kwa kuwapa wakulima ili na wao wajaribu na kutoa maoni yao.

Manyong alisema katika mkakati huo hadi sasa taasisi imeweza kubaini mbegu 18 za mihogo ambazo ni bora na zifaa kwa mkulima kupanda na kuzalisha faida kwa wingi endapo atazingatia maelekezo ya wataalam.

Alisema ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wakulima nchini taasisi imejenga jengo lenye maabara ya kisasa la utafiti ambalo linatarajiwa kulizinduliwa Mei 13 mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.

Manyong alisema kuzinduliwa kwa jengo hilo kutasaidia kuwapa uelewa zaidi wanafunzi na watalaam wa utafiti mbalimbali wa kilimo nchini.

Grace Kihwelu alilia zao la kahawa

Dodoma
Mbunge wa Viti Maalum, Grace Kihwelu (Chadema) ameitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa kufufua kilimo cha kahawa katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Akiuliza swali bungeni jana,mbunge huyo alisema kwa miaka mingi zao hilo limekuwa tegemeo kwa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro,lakini kwa sasa kilimo hicho ni kama kimekufa.
“Je Serikali ina mpango gani madhubuti na mahsusi wa kufufua kilimo cha kahawa Kilimanjaro ambacho kwa miaka mingi kimekuwa tegemeo kwa wananchi wa Kilimanjaro na mhimili mkubwa kwa uchumi wa taifa?” Alihoji Kiwelu.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira alisema Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza tasnia ya kahawa kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kahawa nchini kwa kuongeza tija na ubora wa kahawa kitaifa.
Aliyataja maeneo mahsusi ya mkakati huo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kutoka wastani wa sasa wa tani 50,000 kwa mwaka hadi tani 100,000 ifikapo mwaka 2022.
Nyingine ni kuongeza ubora wa kahawa ili kupata bei ya ziada katika masoko ya nje kutoka wastani wa asilimia 35 hadi kufikia wastani wa asilimia 70 ifikapo mwaka 2022,” alisema
Alisema maeneo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuimarisha huduma za ugani ili wakulima wazingatie kanuni bora za kilimo cha kahawa na kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) ili kuhakikisha upatikanaji wa miche bora ya kahawa.
Wassira alisema pia serikali inaendelea kuongeza matumizi ya viwanda vya kati vya kutayarisha kahawa ili kuongeza ubora wa zao hilo hivyo wakulima kunufaika na bei nzuri.