Friday, November 9, 2012

Used Tractors For Sale

Call: +255 777 086 076

Serikali yakamilisha utafiti misimu ya kilimo

SERIKALI imesema tayari imeshafanya utafiti wa misimu ya kilimo nchini na kutambulika kwa kanda za kilimo kulingana na kiasi cha mvua zinazonyesha.
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR).
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua kama serikali haioni kuwa kuna haja ya kufanya utafiti wa misimu ya kilimo nchini, ili kupeleka mbolea ya ruzuku kwenye eneo husika katika muda muafaka.
Pia alitaka kujua ni kwa nini serikali isiwakopeshe wakulima mbolea hiyo, ili wawe nayo kwa wakati unaofaa kisha walipe baada ya kuuza mazao yao.
Akiendelea kujibu swali hilo, Malima alisema serikali imekuwa ikiratibu mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kwa kila wilaya ya mikoa kwa aina na kiasi.
“Baada ya kupokea mahitaji hayo serikali inawasiliana na makampuni ya pembejeo za kilimo, ili kuhakikisha uwepo wa pembejeo hizo katika maeneo yote hapa nchini kwa wakati kabla ya msimu huo kuanza,” alisema.
Alifafanua kuwa katika mwaka 2012/2013 mahitaji ya mbolea nchini yanakadiriwa kuwa tani 485,000.
Naibu waziri huyo alisema pamoja na mahitaji ya pembejeo kujulikana na kampuni, bado imekuwepo changamoto kwa baadhi ya mikoa kutofanya tathmini ya mahitaji halisi ya pembejeo katika maeneo yao na hivyo kuwahimiza kununua pembejeo mapema.
Aidha alisema changamoto hizo zimesababisha mawakala kukaa muda mrefu bila kuuza kutokana na wakulima kusubiri hadi mvua zinyeshe ndipo wanunue pembejeo.

Wednesday, November 7, 2012

Karoti inahitaji palizi ya mara kwa mara

Nimepanda karoti lakini sitaki kutumia dawa za viwandani kuua magugu mbali na kupalilia kwa mikono ni dawa gani za asili ninazoweza kutumia kuua magugu?

 
Magugu ni tatizo kubwa kwa karoti.  Hii ni kwa sababu ni zao linalokuwa taratibu na pia majani yake si mapana kuweza kuweka kivuli halikadhalika kupambana na wadudu. Magugu yasipodhibitiwa, yataathiri mavuno kwa kiasi kikubwa. Kwa bahati mbaya hakuna dawa za asili za kuulia magugu. Viini vyovyote vinavyoweza kutumika kuulia magugu ni wazi kuwa pia vinaweza kuathiri mazao pia. Hivyo, wakulima wanaofanya kilimo hai hufanya palizi kwa kutumia mikono au mashine.

Utunzaji wa karoti kwa njia ya kilimo hai, ni lazima uanze hata kabla ya wakati wa palizi. Panda karoti sehemu ambayo haina magugu mengi, na ambayo haija athiriwa sana na magugu kama vile mbaruku, mtunguja na nyasi.  Panda karoti kwenye sehemu uliyovuna mazao kama vile maboga, matango, tikiti, vitunguu au spinachi.  Baada ya kuvuna mazao yaliyotangulia, lima shamba lako na upande mbegu za karoti kwenye kitalu kisichokuwa na magugu.


Udongo ni lazima uvunjwe vizuri ili kuepusha hali itakayozuia mizizi kwenda chini ipasavyo. Karoti inahitaji udongo unaoweza kuruhusu kwenda chini vizuri, na unaopitisha maji vizuri, na wenye kiasi kikubwa cha malighafi zinazo oza (udongo mweusi). Utunzaji wa udongo kwa ajili ya kilimo hai, ni pamoja na kuweka mbolea vunde, pamoja na matandazo ambayo huongeza rutuba kwenye udongo kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo wakati wa kupanda karoti, inabidi shamba lisiwe na mabaki ya mazao ambayo hayaozi kwa kuwa yanaweza kuathiri uotaji wa mbegu za karoti. Endapo dawa za kuulia magugu zitatumika, inabidi zitumike kabla ya kupanda kwa kuwa zinaweza kuuwa miche ya karoti pia.


Karoti zinahitaji kukua kwa haraka bila vipingamizi ili kuwa na majani pamoja na mizizi iliyo imara. Kupalilia mapema ni muhimu ili kuepuka upotevu wa mavuno, hasa katika wiki 10 za mwanzo toka kuota. Wakulima wa karoti hutumia jembe la mkono kupalilia kati ya mstari na mstari wa miche ya karoti. Lakini magugu yanayo ota katikati ya karoti ni lazima yang’olewe kwa mikono. Kuwa makini ili usijeruhi mimea! Kwa kawaida kupalilia kwa kutumia jembe la mkono hufanyika mara 3 katika kipindi chote cha ukuaji.

Bei mpya ya korosho yatangazwa



Bodi ya Korosho Tanzania imetangaza bei ya kununulia korosho kwa msimu wa 2012/ 2013 kwa wakulima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo. Mudhihir Mudhihiri, alisema katika msimu huo kilo moja ya korosho kwa daraja la kwanza itakuwa inanunuliwa kwa Sh. 1200 wakati daraja la pili itanunuliwa kwa Sh. 960 kwa kilo.
Mudhihili alisema kwamba wadau wa korosho wamekubaliana kuwa wakulima watalipwa malipo yao kwa awamu mbili na malipo ya kwanza yatakuwa asilimia 70 ya bei dira na ya pili yatakuwa asilimia 30.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu zoezi la kukusanya korosho kwa wakulima ambalo hufanywa na vyama vya msingi kwa katika msimu wa manunuzi limechelewa kufanyika kutokana na vyama hivyo kuchelewa kupata mikopo ya kuviwezesha kulipia zao hilo kwa wakulima.
Mudhihili alisema licha ya msimu wa ununuzi wa zao hilo kufunguliwa tangu Septemba mwaka huu, lakini ununuzi huo umechelewa kuanza na hivyo kuwaathiri sana wakulima.
Aliongeza kuwa akutokana na tatizo hilo, Waziri wa Chakula, Ushirika na Masoko, Christopher Chiza, aliamua kuitisha kikao cha dharura kilichojumuisha Bodi ya Korosho, Bodi ya Leseni ya Maghala, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya CRDB, NMB na Benki ya Rasilimali (TIB) kwa ajili ya kuzungumzia mkanganyiko wa bei dira.

Tuesday, November 6, 2012

Vitunguu, kiungo cha chakula chenye faida kwa mkulima


Hapo awali kitungu kilikuwa ni zao lililokuwa linapatikana porini katika ukanda wa bahari ya Mediterania. Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi 20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).

Matumizi


Kitunguu hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, na pia hutumika kama dawa ya kansa ya tumbo, vidonda na majipu.



Ustawi

Zao la vitunguu hustawi katika udongo wa tifu tifu wenye mbolea ya kutosha, ukiwa na uchachu wa udongo (PH) kiasi cha 6 – 6.8.  Udongo wa mfinyanzi haufai kwa zao la vitunguu kwa kuwa hauruhusu viazi vya vitunguu (bulbs) kutanuka.  Hivyo uwezekano wa kupata mazao ni mdogo. Pia udongo wa kichanga haufai kwa zao la kitunguu kwa kuwa hauna mbolea na hivyo vitunguu huwa vidogo sana, jambo ambalo ni vigumu kupata mazao yanayofaa kwa soko.
Zao la kitunguu huhitaji unyevu muda wote wa ukuaji wake. Zao hili lina mizizi mifupi hivyo linahitaji kumwagiliwa maji mara kwa mara.

Aina za vitunguu


Kuna aina mbili za vitunguu ambazo zimezoeleka:
• Vitunguu vya asili kama vile Singida, na Rujewa (aina hii ina rangi ya kahawia iliyopauka).
• Chotara: Hii ni aina ya vitunguu inayojulikana kama vitunguu vya kisasa. Katika kundi hili kuna vitunguu kama Texas grano, Red creole, Bombay red, White granex, na Super rex.

Mgawanyiko


Zao la vitunguu limegawanyika katika makundi mawili. Hii inatokana na uhitaji wa mwanga na ukuaji wake.  Aina ya kwanza inahitaji mwanga kwa saa 8-13 ili kuweza kuchanua na kutoa mbegu.


Aina ya pili inahitaji mwanga kwa saa 13-15 kuweza kuchanua na kutoa mbegu.


Kupanda


Vitunguu hupandwa kwa kutumia mbegu ambazo husiwa kwenye vitalu.  Kitalu kinaweza kuwa na upana wa mita 1, urefu unategemeana na ukubwa wa eneo ulilo nalo.


Unaweza kupanda vitunguu kwenye matuta mbonyeo (
Sunken bed). Aina hii ya upandaji hutumika kwenye eneo lenye shida ya maji. Upana wa tuta uwe mita moja.

Kupanda kwenye matuta mwinuko (
Raised bed) upandaji wa iana hii hutu mika sehemu yenye maji mengi au yanayotuama.

Tahadhari
: Maji yakituama kwenye vitunguu hufanya vitunguu kuoza, hivyo kuathiri mavuno.

Nafasi


Vitunguu vipandwe kwa nafasi ya sentimita 7.5 kutoka mche hadi mche, sentimita 12.5 kutoka mstari mmoja hadi mwingine kwenye matuta.


Mbole ya kupandia


Unaweza kutumia mboji, au samadi iliyo oza vizuri kupandia. Baada ya hapo unaweza kuongeza mboji baada ya miezi miwili. Endapo unafanya kilimo kisichozingatia misingi ya kilimo hai, unaweza kupanda kwa kutumia mbolea aina ya NPK (20:10:10) baada ya mwezi na nusu, unaweka mbolea ya Urea.


Palizi


Vitunguu ni zao lenye uwezo mdogo sana wa kushinda na magugu. Hivyo, inabidi shamba liwe safi muda wote wa ukuaji hadi kuvuna.


Uvunaji


Kwa kawaida, vitunguu huchukua muda wa miezi 5-6 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Unaweza kuanza kuvuna vitunguu baada ya asilimia 75 ya shingo za vitunguu kuvunjika.  Baada ya kuvuna, unaweza kuweka kwenye madaraja (grades) kwa kufuata ukubwa, rangi na unene wa shingo ya kitunguu. Vitunguu vyenye shingo nyembamba hudumu zaidi, vyenye shingo nene huoza haraka.


Ukataji


Hakikisha kuwa shingo ya kitunguu inabaki kiasi cha sentimita 2. Hii husaidia kuzuia kuoza haraka.


Namna ya kuhifadhi vitunguu


Baada ya kuvuna, hifadhi vitunguu kwenye kichanja chini ya kivuli na uvitandaze vizuri.  Unaweza kuhifadhi vitunguu kwa kufunga kwenye mafungu na kuvitundika.  Vitunguu vikihifadhiwa vizuri vinaweza kukaa hadi miezi minne bila kuharibika, hii hutegemeana na aina ya uhifadhi.


Wadudu wanaoshambulia vitunguu

Kuna aina nyingi za wadudu wanaoweza kushambulia vitunguu.  Hawa wafuatao ni baadhi ya wadudu waliozoeleka kwenye zao la vitunguu.


Thiripi
Thiripi (Thrips): Wadudu hawa hukaa kwenye jani sehemu inayokutana na shina. Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani ya vitunguu na kusababisha majani kuwa na doti nyeupe.

Madhara:
Husababisha vitunguu kudumaa hivyo kuathiri ukuaji wake jambo ambalo huathiri mavuno pia.

Kimamba
Kimamba: Wadudu hawa hufyonza maji kwenye vitunguu, na kusambaza ugonjwa wa virusi. Husababisha kudumaa kwa vitunguu. Wadudu hawa ni hatari zaidi kwa kuwa husambaza virusi vinavyoingia hadi kwenye mbegu.

Minyoo fundo (Nematodes):
Aina hii ya minyoo hushambulia mizizi ya vitunguu. Hali hii husababisha kudumaa kwa vitunguu kwa kuwa hushindwa kufyonza maji na chakula kutoka ardhini.

Vidomozi (Leaf minor):
Hushambulia majani kwa kujipenyeza kwenye ngozi ya jani na kusababisha michoro ambayo huathiri utendaji wa majani.

Utitiri mwekundu (Red spider mites):
Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani na kusababisha vitunguu kunyauka.

Funza wakatao miche:
Funza hawa hutokana na wadudu wajulikanao kama Nondo, na hushambulia shina na kulikata kabisa.

Namna ya kukabiliana na wadudu hawa


Unaweza kukabiliana na wadudu hawa kwa kufanya kilimo cha mzunguko.  Usioteshe vitunguu sehemu moja kwa muda mrefu, au kufuatanisha mazao jamii ya vitunguu kama vile
leaks.

Tumia mbegu bora zilizothibitishwa kutoka kwenye kampuni zinatambuliwa kisheria na kibiashara.  Kupanda kwa wakati unaotakiwa; vitunguu visipandwe wakati wa kiangazi. Vipandwe wakati wa majira ya baridi na kuvunwa wakati wa joto. Tumia dawa za asili za kuulia wadudu, au dawa nyinginezo zinazopendekezwa na wataalamu wa kilimo.


Magonjwa yanayoshambulia vitunguu


Purple blotch
1. Purple blotch: Ugonjwa huu husababishwa na ukungu (fungus). Ugonjwa huu husababisha mabaka ya zambarau na meusi katika majani ya vitunguu.  Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu unyevu mwingi.
Madhara:
Ugonjwa huu hupunguza mavuno mpaka asilimia hamsini (50%).

2. Stemphylium leaf blight:
Hukausha majani kuanzia kwenye ncha hadio kwenye shina.; Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu na ukungu mwingi.
Madhara
: Hupunguza mavuno hadi kwa asilimia sabini na tano (75%).

Onion yellow draft virus
3. Magonjwa ya virusi (Onion yellow draft virus): Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa na rangi iliyochanganyika, kijani na michirizi myeupe au njano.  Vitunguu hudumaa kwa kiasi kikubwa;Ugonjwa huu husababishwa na kimamba.
Madhara:
Huathiri mavuno kwa asilimia 80 mpaka asilimia 100%.

4. Kuoza kwa kiazi (Bulb rot): Husababishwa na fangasi. Ugonjwa huu hutokea vitunguu vikishakomaa, huku udongo ukiwa na maji maji.  Vitunguu vikishakomaa visimwagiliwe tena.

Uharibifu wa vitunguu usiotokana na magonjwa


1. Kuchipua baada ya kuvunwa:
Hali hii hutokea endapo vitunguu vitavunwa kabla ya muda wake.  Endapo vitunguu havitakaushwa vizuri baada ya kuvunwa. Hali hii husababisha uharibifu mpaka asilimia themanini (80%).  Sehemu ya kukaushia vitunguu iwe na hewa inayozunguka na mwanga wa kutosha. Vitunguu vikiwekwa gizani huchipua kwa urahisi.

2. Muozo laini (Soft rot):
Ugonjwa huu hushambulia vitunguu baada ya kukomaa; husababishwa na vimelea (bacteria). Vitunguu hutoa harufu mbaya ya uozo.  Kuepuka hilo vuna kwa wakati unaofaa, hifadhi sehemu yenye mwanga na hewa inayozunguka.

Virusi

Unaweza kuzuia vimamba ambao ndio wanaoeneza virusi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu.

Ufugaji wa nguruwe

Nguruwe ni mnyama mwenye faida, na ni rafiki kwa mazingira na hahitaji gharama kubwa.....


Ufugaji wa Nguruwe ni lazima uwe wa kisasa ili kupata mazao bora. Unaweza kupata kila unachohitaji wewe, familia na hata ndugu zako kutokana na ufugaji wa nguruwe”, anasema Bwana Lomaiyani Molel kutoka Arusha. Jamii nyingi hapa Tanzania huchukulia nguruwe kama mnyama mchafu na asiyefaa kuwa karibu naye na hata kwa matumizi kama lishe. Zaidi, nyama yake inapendwa na haina madhara kwa afya na inapendekezwa kuliwa zaidi kuliko nyama nyekundu. Unaweza kuanzisha mradi wa nguruwe kwa gharama ndogo lakini baada ya kipindi cha miezi tisa tu ukaanza kujipatia kipato kutokana na ufugaji huo.


Ufugaji
Kwa kawaida nguruwe wanafugwa na watu wa kada zote, wafugaji wadogo wadogo na hata wakubwa. Aina hii ya ufugaji huweza kumpatia mkulima kipato pamoja na lishe kwa familia, na hauhitaji gharama kubwa.

Banda

Nguruwe wanahitaji kuwa na banda lililojengwa kwa vifaa nafuu. Unaweza kutumia mchanga na simenti kuweka sakafu, ama ukatumia udongo wa mfinyanzi kwa ajili ya kuweka sakafu. Ukubwa wa banda unategemeana na idadi ya nguruwe unaotaka kufuga. Mita 3 kwa mita 2.5 zitawaweka guruwe 8-10 wanaonenepeshwa kwa soko au nguruwe jike mmoja na nguruwe ndume mmoja.

Malisho

Ulishaji wa nguruwe ni rahisi kwa kuwa wanakula aina mbalimbali za vyakula kulingana na mazingira wanayofugwa. Unaweza kuwalisha kwa kutumia majani laini ya aina mbalimbali, na pia hulishwa kwa kutumia masalia ya nafaka (pumba). Unaweza kuwalisha kwa kutumia mashudu au pumba aina ya Wheat Poland. Pia unaweza kuwalisha kwa kutumia mabaki ya jikoni.

Kuzaliana

Nguruwe hubeba mimba kwa kipindi cha siku 114, ambazo hugawanyika kwa miezi 3, wiki 3 na siku 3. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kuzaa watoto 6 hadi 14 kwa mara moja. Watoto wa nguruwe (piglets) huanza kula chakula cha kawaida wanapofika umri wa mwezi mmoja na nusu mpaka miezi miwili. Endapo nguruwe watapata matunzo mazuri, baada ya miezi 8 wanakuwa na uzito kati ya kilo 50-70 na wanaweza kuuzwa.

Matunzo

Baada ya nguruwe kuzaa anatakiwa kupatiwa chakula cha kutosha na cha kutia nguvu ili kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya watoto wake. Watoto wa nguruwe wachomwe sindano ya madini ya chuma (Iron injection) baada ya siku moja au mbili toka kuzaliwa. Hii ni muhimu sana vinginevyo wanaweza kufa wote. Kata meno (tooth clipping) baada ya miezi mitatu. Unaweza kuhasi madume (castration) baada ya miezi miwili.

Magonjwa yanayoathiri nguruwe

Kuna aina nyingi za magonjwa yanayoshambulia nguruwe, lakini yapo yale yaliyozoeleka ambapo ni lazima kukabiliana nayo ili kuwa na ufugaji wenye tija.

Ugonjwa wa miguu na midomo

Ugonjwa huu huathiri nguruwe sehemu za miguu na midomo. Ni ugonjwa ambao hushambulia nguruwe mara kwa mara hasa wasipokuwa na matunzo mazuri. Ugonjwa wa miguu na midomo, hudhoofisha nguruwe kwa haraka sana, ikiwa ni pamoja na kupungua uzito.


Chanjo:
Chanjo kwa ajili ya ugonjwa wa midomo na miguu (FMD vaccine) hutolewa kila baada ya mwaka mmoja. Hii inasaidia kuwaweka nguruwe wako katika hali nzuri zaidi bila kushambuliwa na magonjwa hayo.

Tiba:
Ugonjwa huu hauna tiba halisi. Inapotokea nguruwe wakawa wameshambuliwa kinachofanyika ni kutibu magonjwa nyemelezi kwa kutumia antibiotics.
 
Homa ya Nguruwe (Swine fever)
Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa homa ya nguruwe huenea kwa haraka sana miongoni mwa makundi ya nguruwe, na huua kwa haraka sana, lakini hauna madhara kwa binadamu na hauambukizwi kwa binadamu. Nguruwe walioambukizwa waanshikwa na vindonda ama mapunye kwenye ngozi. Pia masikio na ngozi huwa mekundu.

Chanjo: Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba. Kinachofanyika mlipuko unapotokea ili kuwa salama ni kuwateketeza nguruwe wote walioathirika na kuanza upya. Unaweza kuteketeza kwa kuwachoma moto.
Muhimu: Baada ya kuwateketeza nguruwe wagonjwa, safisha banda kisha nyunyiza dawa aiana ya Acon au Ectomin, na uache banda wazi kwa kipindi cha wiki moja kabla ya kuweka nguruwe wengine.

Ugonjwa wa mapafu (Pneumonia)

Huu ni ugonjwa unaoshambulia sehemu za koo na mapafu ya nguruwe, ambapo husababisha kukohoa na kupumua kwa shida. Ugonjwa huu husababishwa na bacteria (Secondary bacterial), joto kupita kiasi, vumbi na gesi inayotokana na madawa makali.


Tiba:
Homa ya mapafu kwa nguruwe inatibika kwa kutumia antibiotics. Pamoja na kuwaweka wanyama sehemu safi, isiyo na baridi kali au joto la kupitiliza kiwango.

Kimeta (Anthrax)

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Bacillus anthracis, wadudu hawa wanabaki kuwa hai kwa muda mrefu na wanaweza kuwa kwenye udongo wakiwa hai kwa kipindi cha miaka mingi.

Chanjo:
Chanja nguruwe wako dhidi ya kimeta kama utakavyoelekezwa na wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.
Tiba:
Unaweza kutibu nguruwe wako kwa kutumia dawa aina ya Penisilin au Oxytetracycline.

Muhimu:
Homa ya nguruwe ni lazima iwekewe karatini kwa sababu husambaa kwa haraka sana. Nchini Tanzania mlipuko wa homa ya nguruwe umekuwa ukitokea mara kwa mara maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Malawi na katika mkoa wa Mbeya.