Nyanya ni zao la chakula na biashara. Kilimo cha zao hili hufanyika majira yote
(masika na kiangazi), na faida hupatikana haraka na ni ya kuridhisha ikilinganishwa
na mazao mengine. Pamoja na umuhimu wa zao hili, wadudu waharibifu na
magonjwa huathiri uzalishaji na ubora wa matunda. Ili mkulima aweze kupata faida
na kuongeza pato la kaya yake ni vema kuzingatia udhibiti wa magonjwa na wadudu
wa zao hili. Kipeperushi hiki kinatoa maelezo ya udhibiti wa magonjwa na wadudu
muhimu ya zao la Nyanya.
MAGONJWA YA NYANYA
Bakajani chelewa (Late blight)
Ugonjwa huu huenenzwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na hali ya hewa hasa
ya unyevunyevu, na huenezwa na upepo. Majani, shina, matunda hushambuliwa.
Majani huwa na ukungu mweupe na kijivu, na baadaye hukauka. Matunda huwa na
mabaka ya kikahawia na baadaye kuoza. Mashina pia huwa na mabaka ya kikahawia.