Tuesday, February 3, 2015

Magimbi, mkombozi wakati wa njaa

Hello Mkulima Mbunifu, naomba maelezo jinsi ya kuzalisha zao la magimbi hali ya hewa, ardhi, mvua au umwagiliaji na mda gani tangu kupanda hadi kuvuna. Asante – David Kilangi. yamMagimbi ni chakula muhimu chenye kiwango kikubwa cha wanga kinachohitajika katika mwili wa binadamu na moja kati ya mazao makuu ya chakula kama vile viazi mviringo, mihogo na viazi vitamu. Zao hili hulimwa katika sehemu mbalimbali duniani kama barani Afrika, Caribbean, Asia, America na Pacific. Kwa nchi za Afrika, zao hili hutumika zaidi kunapokuwa na uhaba wa chakula, kwani lenyewe hupatikana msimu wote wa mwaka na katika majira yote.
 Matumizi Magimbi hutumika kama chakula kikuu na huweza kupikwa kwa kuchanganya na ndizi, nyama, viazi, kupika kwa kukaanga, kuchemsha, kuchoma au kwa namna yoyote ila ambayo mlaji ataamua kutengeneza mlo wake.
  Pia hutumika kutengenezea unga wa ugali kwa kukatakata na kukausha kisha kuchanyanga na mahindi pamoja na mtama. Kulingana na kukua na kuongezeka kwa njia nyingi za ujasiriamali, zao hili kwa sasa hutumika kwa kutengenezea kaukau (crisps) kama ilivyo kwa viazi mviringo, viazi vitamu, ndizi na mihogo.




 Aina yam 2Kuna aina nyingi za magimbi zinazolimwa katika nchi mbalimbali ulimwenguni kama Dioscorea rotundata, Dioscorea alata, Dioscorea esculenta, Dioscorea Cayensis, Dioscorea dumetorum, Dioscorea bulbifera lakini kwa hapa Tanzania, kuna aina tatu za magimbi ambazo ndizo hulimwa kwa wingi.
Aina hizo za magimbi huweza kuwekwa katika makundi mawili ambazo ni magimbi yenye viazi na yasiyokuwa na viazi ila huwa shina kuu ambalo ndilo hutumika kama chakula (huwa na rangi ya zambarau).
Hata hivyo, magimbi yenye viazi vimegawanyika pia mara mbili, kuna magimbi yenye viazi vyeupe na yenye viazi vyeusi (vikimwenywa kwa ndani yana rangi nyeupe na vidoti vya zambarau au nyeusi kwa mbali).
 Hali ya hewa Zao hili hustawi katik maeneo yenye kiasi cha nyuzi joto 25°C hadi 30°C na mwinuko wa mita 900 kutoka usawa wa bahari. Magimbi hustawi katika eneo lenye ubaridi, unyevu na maeneo ya msitu. Aidha, hustawi katika eneo la tambarare au hata milimani, lakini zaidi katika maeneo ya bondeni au kwa kuotesha penye migomba, miti au kahawa ili kupata kivuli kwani hayahitaji kupigwa na jua sana.
 Udongo Magimbi hustawi katika udongo tifutifu (loam soil). Udongo ni lazima uwe na rutuba ya asili ili kuleta mavuno mengi na yenye ubora.
 Mbolea Zao la magimbi halihitaji mbolea nyingi. Kinachotakiwa ni kuotesha katika ardhi yenye rutuba ya asili kwani ikiwekwa mbolea mara nyingi husababisha majani kumea na kushindwa kuweka viazi. Ikiwa ardhi haina rutuba yake ya asili basi waweza kuweka mbolea ya mboji kidogo hasa wakati wa kuandaa shamba. Sambaza mboji katika shamba zima ndipo ulilime, hii itasaidia udongo kuchanganyika vizuri na mbolea.

  Mbegu Mbegu za magimbi hutokana na mzizi mkuu (tunguu) ambalo huwa nene na ndilo linalobeba viazi au chipukizi ambalo hujitokea pembezoni mwa shina.
 Namna ya kuandaa mbegu Baada ya kung’oa na kuondoa viazi wakati wa kuvuna, chukua mzizi mkuu na kata kwa kupunguza na kubakiza kiasi cha sentimita mbili hadi 4 kuungana na majani yake. Punguza majani kwa kuyakata na kubakiza jani kuu la katikati peke yake au yakiwa mawili hadi matatu. Acha kwa siku chache ili kuponyesha kidonda chake ndipo uoeteshe (siku 5 hadi 7).
 Uoteshaji Ni vyema kuotesha mwanzoni mwa msimu wa mvua japo pia unaweza kuotesha wakati wowote.
• Hakikisha shamba limelimwa vizuri kwa kuondolewa magugu yote kasha kufukiwa.
• Piga mashimo kwa umbali wa mita 1 kati ya shimo na shimo na mita 1 kati ya mstari na mstari.
• Shimo liwe na urefu wa futi moja.
• Baada ya hapo chukua mbegu uliyoiandaa na fukia vizuri (walau kiasi cha sentimeta 10 kiwe kimefunikwa kwa udongo).

  Usafi wa shamba Shamba la magimbi huweza kufanyiwa usafi kama shamba la migomba. Mara nyingi magimbi huua magugu yaliyomo shambani pindi tu linapoanza kushika ardhini na kuanza kuweka viazi. Aidha, katika sehemu yenye joto ambayo matandazo huwekwa shambani, si rahisi kwa magugu kuota.
 Umwagiliaji Kutokana na kuwa magimbi huoteshwa katika eneo lenye maji ya kutosha kama kwenye chemichemi ama eneo lenye ubaridi na unyevu, halihitaji kumwagiliwa. Kiasi cha maji, unyevu na ubaridi huo unatosha kusaidia katika kukuza, kuweka viazi na kukomaa vizuri. Aidha, katika maeneo ambayo yana hali ya joto ni vyema kuweka matandazo shambani baada ya kuotesha ili kulinda unyevu.

  Magonjwa  Zao la magimbi husumbuliwa na magonjwa ya mizizi kama Botryodiplodia theobromae, Rhizopus nodosus, Fusarium oxysporum, pamoja na wadudu kama nematode au beetle na ili kuepuka hayo ni vyema kufanya kilimo cha mzunguko ama kupumzisha shamba kwa muda baada ya kuvuna. Pia huweza kushambuliwa sana na fuko. 

 Kukomaa hadi kuvuna Magimbi hukomaa vizuri na kuanza kuvunwa baada ya miezi nane hadi kumi toka kuoteshwa na ni vyema zaidi kuvuna katika kipindi cha masika kwani mara nyingi kuvuna wakati wa mvua viazi havitaiva kama vikipikwa na pia huwasha mdomo kama pilipili.

posted by elias wa eastern garade farm
 
 

No comments:

Post a Comment