Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika chini ya Idara ya Zana za Kilimo imeandaa mkakati wa kuboresha sekta ya kilimo ili wakulima waondokane na jembe la mkono na kutumia zana za kisasa ikiwa ni moja ya sababu zinazoweza kuleta tija kwenye sekta ya kilimo nchini.
Zana ambazo zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kutumia mafuta ya dizeli zinaweza kutumika katika mazingira mbalimbali ya kilimo nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya zana za kilimo ya Savoy Farm Ltd Bw. Omari Issa akizungumza katika maonesho ya Nane Nane , viwanja vya Nzuguni alisema mashine aina ya ‘palleting’ zimetengenezwa kwa ajili ya kuwakomboa wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na kilimo ili wazitumie katika shughuli zao.
Alisema mashine hizo zinatumia muda mfupi katika kukoboa mpunga na hivyo kurahisisha shughuli za mkulima.
‘’Tumetengeneza mashine za gharama nafuu ambazo zinawasaidia wakulima wa mpunga kukoboa nafaka kwa muda mfupi, hivyo aliwasihi wakulima kuzitumia ili warahisishe shughuli zao za kilimo’’, alifafanua Bw. Omary.
Alifahamisha kuwa mashine hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini,na lengo la kutengeneza mashine hizo ni kuwawezesha wakulima kuondoka kwenye matumizi ya teknolojia ya zamani ya ukoboaji kwa kutumia mikono na kujiunga kwenye teknolojia ya kisasa.
Kwa mujibu wa Bw. Omary mashine hizo zinatakiwa kwa wingi na amewaomba wakulima kununua zana bora za kilimo zinazotengenezwa nchini ili kupunguza gharama za kuagiza nje ya nchi.
Mmoja wa wakulima kutoka wilaya ya Manyoni aliyehudhuria maonesho hayo ,Bi. Salome Kazimoto alisema mashine za kukobolea mpunga zinasaidia kupunguza muda wa kukoboa kwa kutumia teknolojia ya zamani ambayo inachangia kurudisha nyuma ufanisi wa kazi.
Bi. Kazimoto alikiri kuwa mashine hizo zinamrahisishia kazi mkulima na kusema kuwa mpaka sasa idadi ya wakulima wanaotumia zana za kisasa ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wanaotumia zana za zamani za kilimo.
Baadhi ya wakulima wanaoshiriki kwenye maonesho haya ya kilimo wameitaka serikali kuelimisha wananchi ili watumie zana za kisasa katika shughuli zao.
‘’Endapo wakulima wataelimishwa ili watumie zana za kisasa za kilimo ili kujikwamua katika kilimo cha zamani kwa lengo la kuongeza uzalishaji’’aliongeza Bi. Kazimoto ambae ni mkulima.
Noel John, mkulima kutoka Morogoro alisema tangu aanze kutumia mashine za kisasa katika shughuli mbalimbali za kilimo katika zao la mpunga,amekuwa akifanya kazi hizo kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.
WIZARA KUNUNUA MAZAO YA NAFAKA NCHINI
Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imetangaza nia yake ya kutaka kununua mazao ya nafaka ili kumwekea mkulima wa hali ya chini soko la uhakika.Miongoni mwa mazao yatakayonunuliwa kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ni mpunga,maharagwe,karanga,choroko,ulezi,ufuta na mahindi,na yatanunuliwa kwa bei ya ushindani ya soko mwaka huu.Hayo ni kwa mujibu wa Mchumi wa bodi hiyo Bw. Edwin Mkwenda katika maonesho ya wakulima yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni Manispaa ya Dodoma.Bw. Mkwenda alisema tayari Serikali imeikabidhi bodi hiyo maghala yote yaliyokuwa ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC),ambayo hayakubinafsishwa zilizoko kwenye kanda saba ili kutunza mazao yatakayonunuliwa.Kuundwa kwa bodi hiyo ni ukombozi kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao husika
.Imetolewa na:Wizara ya kilimo tanazania
posted by vailet wa eastern grade farm
No comments:
Post a Comment