UTANGULIZI
Ndizi ni zao linalolimwa katika ukanda wa tropiki na hutumika kwa ajili ya kupikia na kama matunda. Vilevile ndizi huweza kutengenezea starch, chips, pombe (mbege), ama kukaushwa na kuuzwa kama matunda yaliyokaushwa. Wakati mwingine ndizi hutumika kutengenezea unga ambao huweza kutumika kwenye supu, mikate, ugali na uji. Maua ya ndizi huweza kutumika kama mboga, ila ni lazima yachemshwe kwenye mji ya chumvi ili Kuondoa ladha ya uchungu. Majani ya mmea huu ni chakula kizuri cha kuku na wanyama na huwa na virutubisho aina ya protein kwa wanyama hawa. Pia majani haya hutumika kwa ajili ya kupakia vitu mbalimbali na kwa ajili ya kuezekea nyumba. Pia ni mazuri sana kwa kutandazia shamba ama bustani. Halikadhalika migomba hutumika kuzuiya ama kupunguza kasi ya upepo.
MAHITAJI YA MAJI, HALI YA HEWA NA UDONGO
Wakulima wa mwanzo kabisa wa ndizi walitokea huko Maleshia na kusini mashariki mwa bara la Asia. Huko ndizi ilikuwa ikilimwa kwenye udongo wenye rutuba nyingi sana na udongo wa volkano. Pia kwenye delta za mito na kandokando ama ndani ya misitu ambako udongo huwa na rutuba sana.
Ndizi hukua vizuri sehemu zenye joto kidogo na unyevu nyevu na mwinuko wa 0-1800 m kutoka usawa wa bahari . Aina nyingine kama ‘DWARF CAVENDISH’ huweza kusitawi hadi kwenye mwinuko wa mita 2100 kutoka usawa wa bahari (sehemu za milimani sana).
Mahitaji ya mvua ni ya wastani wa 1000mm kwa mwaka japokuwa migomba husitawi vizuri kama ikipata maji ya kutosha. Hii ni pamoja na kumwagilia kipindi cha kiangazi bila kutuamisha maji.
Halijoto ya 27°C hadi 38°C ndio ifaayo kwa kilimo cha ndizi na migomba hudumaa kama kuna baridi sana (chini ya 13°C.)
Upepo mwingi ni tatizo kwa migomba kwa kuchana majani na kuyaharibu pia kuangusha migomba. Kupanda migomba kwa vikundi husaidia kuzuiya upepo na ikibidi migomba iliyobeba ndizi iwekewe nguzo kama zinapatikana.
Udongo mzuri kwa kilmo cha ndizi ni tifutifu yenye uwezo wa kupitisha maji na hewa kwa urahisi. Udongo wenye mbolea nyingi ni mzuri sana kwa migomba.
UPANDAJI
Ndizi hupandwa kwa kutumia vichipukizi ama migomba midogo ama sehemu za viazi zenye uwezo wa kutoa vichipukizi. Uzao wa ndizi hutegemea sana aina na umri wa vichipukizi vilivyotumika wakati wa upandaji. Vichipukizi vizuri ni vile vilivyochongoka vyenye urefu wa sentimeta 75 na upana wa chini ya shina wa sentimeta 15 na majani yake yamechongoka. Hivi huzaa baada ya miezi 18 tangu hayajapandikizwa. Vipandikizi hutoa ndizi hata baada ya miaka 2-3. Migomba mikubwa wastani huzaa bada ya miezi 5-8. Vichipukizi maji vyenye majani mapana havifai kwa kupandikiza kwani huzaa ndizi ndogo na uwezekano wa kupona baada ya kupandikizwa ni mdogo.
VIPIMO
Miche ama vichipukizi vya migomba vipandwe kwenye shimo lenye urefu wa sm 60 na upana wa sm 60. Udongo uchanganywe vizuri na mbolea ya kutosha. Kama mvua hazitoshi, shimo liwe na urefu wa sm 150 na upana wa sm 100.
NAFASI
Kwa aina za migomba midogo nafasi kutoka mmea hadi mmea iwe mita 3, na kutoka mstari hadi mstari iwe mita 3. Migomba 1000 kwa ekari.
Kwa aina ndefu. Mmea hadi mmea mita 3 na mstari hadi mstari mita 4. Migomba 480 kwa ekari.
MUDA WA KUPANDA MIGOMBA
Muda muafaka ni mwisho wa msimu wa kiangazi ama mwanzo wa msimu wa mvua.
MCHANGANYO WA MAZAO
Mazao kama kahawa, mahindi,mbogamboga, papai, miti ya matunda, kivuli na mbao, na mikunde kunde.
MATUNZO
Wiki 4-6 tangu migomba ipadwe, inapaswa kupaliliwa. Pia migomba inafaa kupangiliwa kwa mafungu. Migomba isizidi minne kwa kila kifungu. ‘KISUMU’, vichipukizi vyote viondolewe kubaki na mgomba mmoja mkubwa, na midogo mitatu yenye umri tofauti tofauti ili kupata mazao mwaka mzima.
Migomba mingi sana husababisha kuzaa ndizi ndogo. Vichipukizi vyenye afya ndio vibakishwe, Uchaguzi ufanyike kufuata nafasi iliyopo. Vichipukizi visivyotakiwa vikatwe na kuharibiwa sehemu inyokua.
KUTANDAZIA
Matandazo ni muhimu sana na ikibidi yawekwe shamba zima. Matandazo yawekwe umbali wa sm 60 kutoka kwenye kila fungu la migomba. Hii inasaidia Kuepuka wadudu waharibifu kwenye mizizi ya migomba.
MBOLEA
Migomba huhitaji sana mbolea ili izae vizuri. Mimea aina ya mikunde kunde inaongeza rutuba kwenye udongo kama ikipandwa shambani. Pia mbolea ya samadi na mboji ni muhimu sana. Kama kipato kinaruhusu tunashauriwa kutumia mbolea ya miamba ya Minjingu; ‘MINJINGU ROCK PHOSPHATE’ kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mizizi ya migomba.
MAGONJWA NA WADUDU WANAOSHAMBULIA MIGOMBA
Bacterial wilt(Mnyauko wa bacteria).
Mwanzoni jani mojawapokati ya majani machanga matatu huanza kuwa njano na kuvunjika. Baadae majani mengine hunyauka na kudondoka kuzunguka shina la mgomba. Ndizi iliyoshambuliwa na ugonjwa huu huwa na madoadoa kwa ndani kama inavyoonekana.
NINI CHA KUFANYA
Tumia aina zinazostahimili ugonjwa huu kama zipo.
Tumia vichipukizi visivyo na ugonjwa huu.
Ondoa migomba yote iliyoathirika na uiteketeze.
UGONJWA YA VIRUSI
BUNCHY TOP
Ugonjwa huu huweza kutokea wakati wowote wa ukuaji wa migomba.
Huenezwa na aphids na hushambulia hata vichipukizi. Mimea iliyoathiriwa huweza kushindwa kuzaa na ama ikizaa huzaa ndizi ndogo na ngumu.
NINI CHA KUFANYA
Tumia vichipukizi visivyo na ugonjwa huu.
Ondoa kabisa migomba yenye dalili za ugonjwa huu, pamoja na viazi vyake na teketeza.
Thibiti aphids ambao ndio waenezaji.
MAGOJWA YA FANGASI
MICHIRIZI MEUSI (Black leaf streak )
Ni ugonjwa hatari sana wa migomba na unashambulia majani ya ndizi. Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa na upepo na hukua vizuri kwenye hali ya unyevunyevu. Sehemu za pembezoni mwa jani huanza kukauka na hatimaye jani zima hufa.
Ugonjwa huu husababisha mazao duni na ndizi kuiva kabla ya kukomaa.
NINI CHA KUFANYA
Ondoa na haribu kwa moto majani yaliyoathirika. Vinginevyo ondoa majani yaliyoathirika na weka mbali na shamba la migomba ama fukia chini sana.
Epuka kumwagilia majani kwa juu, tunashauriwa kumwaga maji kwenye shina.
Epuka kupanda kwenye msongamano.
UGONJWA WA PANAMA (Fusarium wilt).
Huu ni ugojwa utokanao na fangasi waishio ardhini na hushambulia mizizi na kuziba njia za kusafirisha maji na madini kwenye mmea, kwahiyo mmea hunyauka na kufa. Majani huwa ya njano na hatimaye kukauka
NINI CHA KUFANYA
Tumia migomba inayostahimili huu ugonjwa kama Dwarf Cavendish.
Kusafisha shamba na Kuondoa visiki vilivyo shambani huweza kusaidia kupunguza ugonjwa huu.
Majivu yanaweza kuwekwa kuzunguka
(UGONJWA WA MUOZO SIGARA) THE CIGAR END ROT DISEASE
Ugojwa huu unaweza kuathiri matunda ya ndizi yaliyoiva, na kusababisha kuoza na kukauka kwa ndizi kuanzia mwisho. Palipoathirika huwa na ungaunga kama majivu.Huonekana kama sigara iliyozimwa. Ugojwa huweza kuendelea hadi wakati wa kuhifadhi ama kusafirisha. Huweza kuharibu mkungu mzima na kusababisha hasara kubwa.
NINI CHA KUFANYA
Zingatia usafi shambani.
Epuka kujeruhi ndizi na usikate ua la ndizi wiki 8-11 tangu izae.
ANTHRAC NOSE
Huu ni ugonjwa unaoshambulia ndizi baada ya kuvuna, hasahasa wakati wa kuhifadhi na kusafirisha. Madoa madogo ya kahawia ama jeusi huanza kutokea kwenye ndizi. Mara nyingi hushanbulia ndizi zilizokomaa vizuri. Hushamiri vizuri kukiwa na hali ya unyevunyevu
Anthracnose Anthracnose fruit rot on banana
NINI CHA KUFANYA
Hakikisha usafi shambani
Punguza kujeruhi ndizi.
Ziweke ndizi kwenye maji ya moto 50° kwa dakika 5.
Kunyuzia mafuta ya jatrofa yaliyochanganywa na maji huzuiya anthracnose hadi siku 12