Thursday, May 2, 2013

Wazalishaji kilimo hai kupata soko la kimataifa

WAZALISHAJI wa mazao ya chakula yanayozalishwa kwa mfumo wa kilimo hai nchini wana fursa ya kuuza mazao yao kwenye soko la kimataifa ikiwa watazingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula na kuzingatia taratibu bora za kilimo.
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam juzi na Mratibu wa Mtandao wa Trade Africa Network Tanzania, Deusdedit Kizito, alipozungumza na waaandishi wa habari kuelezea ziara ya mafunzo ya wiki mbili nchini Ujerumani katika maonesho ya biashara ya Fruit Logistica ya Berlin na maonesho ya bidhaa za kilimo hai ya BioFach, Nuremberg, Ujerumani.
Kizito ambaye pia alikuwa kiongozi wa msafara huo alisema ziara hiyo imefungua milango kwa wazalishaji wa bidhaa zinazotokana na kuzalishwa kwa mfumo wa kilimo hai nchini, kwani wanaweza kuomba na kupatiwa mikopo ya kuendeleza biashara zao kutoka kwenye mashirika ya kimataifa ambayo yameonesha nia ya kukuza biashara hiyo nchini iwapo watakuwa wamepata wanunuzi wa bidhaa zao Ulaya.
“Mikopo hiyo itatumika kukuza mitaji yao kwa kujenga mahala pa kuhifadhia bidhaa zinazozalishwa ikiwamo vyumba vya baridi, magari yenye majokofu kwa ajili ya usafirishaji wa matunda na mbogamboga na pia gharama za kuuza bidhaa nje ya nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa mashirika hayo yanaweza kutoa mikopo hadi asilimia 80 ya thamani ya biashara husika na kuongeza kuwa yanatoa mikopo kwa miradi ya maendeleo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (SME’s), vyama vya ushirika kwa kugharamia mtaji wa uendeshaji na shughuli nyinginezo.
Pia alisema ziara hiyo imefanikisha upatikanaji wa masoko ya bidhaa za asali, kahawa, viungo vya aina mbalimbali, matunda halisi na yaliyokaushwa hasa maembe, nanasi, maparachichi na pensheni.
Kutokana na ziara hiyo, mtandao huo unaishauri serikali kuwa na sera za wazi kuhusu matumizi ya ardhi kuhusiana na wakulima wanaolima kwa kuzingatia mfumo wa kilimo hai na uhifadhi wa ardhi na wakulima wengine wasiozingatia mfumo huo.
“Pia serikali inapaswa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Trade Africa Network Tanzania kama inavyofanya kwa Sido na Tan Trade. Hii inatokana na ukweli kuwa Trade Africa Network Tanzania inalenga kuendeleza ubora na kuongeza thamani ya bidhaa za wazalishaji wadogo ili waweze kukuza kwenye soko la kimataifa,” alisema.
Wakati huohuo, Kizito alisema maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Afrika mwaka huu yatafanyika kuanzia Mei 23 na kilele kuwa Mei 25. Maadhimisho hayo yatafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment