Thursday, May 2, 2013

Kikwete kufungua kongamano la kikanda la kilimo

RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kufungua kongamano kubwa la kikanda la kilimo la muungano wa umoja wa vyama vya kilimo Kusini mwa Afrika (SACAU), lililopangwa kufanyika kuanzia Mei 13 hadi 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo litakaloangalia kwa undani suala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha Afrika linatayarishwa na Baraza la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
Akitangaza kongamano hilo jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa SACAU, Ishmael Sunga, alisema litashirikisha washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 14 za Kusini mwa Afrika pamoja na wawakilishi wa vyama vya wakulima kutoka maeneo mengine ya Afrika. Sunga alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utaangalia ushirikiano kati ya SADC/COMESA/EAC katika masuala ya kilimo.
“Mkutano utaangalia ushirika huo kwa undani, muundo wake na umuhimu wake kwa wakulima na biashara katika sekta hii ya kilimo,” alisema.
Pia mkutano huo utaangalia makisio ya mahitaji ya bidhaa za kilimo duniani na kuona fursa na tishio lake kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Sunga, kongamano hilo litaangalia kama mfumo wa kifedha uliopo sasa unaweza au hauwezi kuendeleza sekta ya kilimo katika siku zijazo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ACT, Janet Bitegeko, alisema kongamano hilo litakalokusanya wakulima toka sehemu mbalimbali Afrika litashuhudia kuzinduliwa kwa mradi wa majaribio wa kilimo wa SACAU nchini.
Alisema kuwa inatarajiwa kongamano hilo litakuja na majibu thabiti ya jinsi ya kuinua kilimo nchini, katika kanda na Afrika kwa ujumla.
ACT ni chama kinachounganisha wadau mbalimbali wa kilimo hapa nchini.

No comments:

Post a Comment