Tuesday, March 18, 2014
WASINDIKAJI MPUNGA WAANZISHA UMOJA
WASINDIKAJI wa zao la mpunga Jijini Mbeya wameanzisha umoja wao ili uweze kuwasaidia kupata soko la uhakika la ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na nguvu ya pamoja ya kutatua matatizo ya wasindikaji wa zao hilo.
Imeelezwa kuwa wasindikaji wa mpunga wamekuwa katika mazingira magumu ambapo mchele unakuwa hauna ubora kutokana na kila mkulima kuzalisha anavyojua hivyo kuwa na chombo cha pamoja kutaweza kusaidia kuwa usindikaji bora wa zao hilo.
Hayo yamesemwa juzi na Mwenyekiti wa muda wa Umoja wa wasindikaji wa Mpunga Jijini humo, Peter Mlegula wakati wa mkutano wa wasindikaji hao uliofanyika jijini Mbeya.
Mlegula alisema kuwa bado kuna changamoto nyingi kwa upande wa wasindikaji lakini kwa nguvu ya pamoja itaweza kusaidia kufika pale wanapohitaji ili kuweza kutatua kero za wasindikaji wa mpunga ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiwakabili .
"Huu umoja tulioanzisha utakuwa na manufaa makubwa sana kwetu sisi wasindikaji kwani hivi sasa tumepata chombo cha pamoja cha kusemea kero zetu ambapo hapo awali hatukuwa na sehemu yeyote ya kusemea," alisema Mwenyekiti huyo.
Msindikaji mwingine Diana Mwaisabila kutoka Wilaya ya Mbarali alisema kuwa lengo la kuanzisha umoja huo ni baada ya kuona wasindikaji wa zao la mpunga hawana mwelekeo wowote kwani kila mmoja anasindika zao hilo anavyojua.
Alisema kuwa umoja huo utaweza kuwasaidia kukaa pamoja na shirika la umeme Tanesco kujadili ongozeko la umeme ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwanyonya wasindikaji wa zao la mpunga.
Kwa upande wa msindikaji mwingine, Abel Mwakipesile alisema kuwa kama msindikaji amefarijika sana kuwa na chombo chao ambacho kitaweza kusaidia hata serikali kuwatambua ili waweze kusaidiwa.
Mkutano huo wa siku moja wa wasindikaji wa zao la mpunga mkoani Mbeya uliandaliwa na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wasindikaji kwa kuwa na chombo chao wenyewe.
BODI YA PAMBA YAJITOSA SAKATA LA QUTON
BODI ya Pamba nchini (TCB) Kanda ya Ziwa imetoa ufafanuzi kuhusiana na malalamiko ya wakulima wa zao la pamba wanaolalamikia kugoma kuota kwa mbegu za pamba zilizosambazwa na Kampuni ya Quton huku wengi wakidai kulipwa fidia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wiki iliyopita, Kaimu meneja wa bodi ya Pamba, Buluma Kalidushi baada ya kuwepo kwa malalamiko hayo, bodi yake iliunda timu ya kufuatilia ili kuweza kubaini ukweli wake lakini hata hivyo wizara kwa upande wake pia iliunda tume ya wataalamu ili kuchunguza malalamiko hayo.
Kalidushi alisema kwa taarifa alizonazo tayari tume ya wizara imekamilisha kazi yake na kinachosubiriwa hivi sasa ni kutolewa kwa taarifa hiyo ili kuweza kubaini sababu zilizosababisha mbegu hizo zisiote katika baadhi ya maeneo huku maeneo mengine zikionesha matokeo mazuri.
Alisema baada ya kutolewa kwa taarifa ya wataalamu hao kutoka wizarani ndipo itakapofahamika iwapo kuna umuhimu wa kulipwa fidia kwa wakulima waliopanda mbegu hizo na zikagoma kuota au kutolewa maelekezo mengine tofauti na suala la madai ya kutaka kulipwa kwa fidia.
"Ni kweli mbegu za Quton katika baadhi ya maeneo zimegoma kuota na zimesababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima, bodi tuliunda timu ya kufuatilia ili kuweza kubaini tatizo, lakini pia wizara iliunda tume na tayari imekamilisha kazi yake, tunasubiri kutolewa kwa taarifa.
"Hata hivyo, ukweli ni kwamba tatizo la mbegu kutokuota limetokea kwa mbegu hizi za Quton, ni tatizo la kila mwaka hata kabla ya kuwepo kwa mbegu hizo, malalamiko yamekuwa mengi kwa vile mbegu hizo zina mwenyewe (Quton ), zamani mbegu zilikuwa za wakulima wenyewe hawakupiga kelele sana zilipogoma kuota," alieleza Kalidushi.
Alisema tatizo la mbegu kugoma kuota mara nyingi linachangiwa na wakulima wenyewe kuchafua kwa makusudi pamba yao pale wanapokwenda kuiuza kwa lengo la kutaka kuongeza uzito ambapo wengi wana tabia ya kuweka maji na magadi na hivyo kusababisha mbegu kuoza.
Alisema tabia ya kuweka maji kwa lengo la kutaka kuongeza uzito wa pamba pale inapopimwa inafaida kidogo sana ikilinganishwa na hasara anayoipata mkulima pale anaporejeshewa mbegu zinazotokana na pamba yake aliyoiuza huku akiwa ameiwekea maji na hivyo kujikuta mwenyewe akipata hasara kwa mbegu hizo kutokuota.
Kwa upande mwingine kaimu meneja huyo alikanusha madai ya kukiukwa kwa taratibu za manunuzi kwa mujibu wa sheria katika kutoa zabuni ya usambazaji wa mbegu za pamba kwa kampuni ya Quton ambapo alisema taratibu zote zilizingatiwa na kampuni hiyo ndiyo iliyoshinda zabuni baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa.
WANANCHI FUATILIENI MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI'
MKURUGENZI Mtendaji wa Asasi isiyo ya
kiserikali ya Pugu Poverty Alleviation and Development Agency (PPADA)
Bw.Abraham Silumbu,amesema wananchi wamekuwa chanzo cha kuwepo kwa matumizi
mabaya ya fedha kutoka kwa watendaji kutokana na kushindwa kufuatilia matumizi
ya Fedha na Rasilimali za Umma (PETS) .
Hayo yamebainika hivi karibuni wakati mkurugenzi huyo akizungumzia juu ya dhana ya misingi ya ufuatiliaji wa PETS katika kata mbalimbali nchini.
Alisema kuwa ili wananchi waweze kuwa na maendeleo ni wakati sasa wa kuhakikisha kuwa wanafuatilia fedha zinazotolewa na Serikali na si kukaa kimya kwani kwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma maendeleo.
Alisema kuwa kuwepo kwa ufuatiliaji wa PETS kutaweza kusaidia kubaini ukweli na kuwasaidia kufanya maamuzi kwa kuwawajibisha watendaji wasio waadilifu na kuimarisha hali ya uwazi katika matumizi ya fedha na rasilimali zingine za umma.
Alisema kuna kila sababu ya kuilaumu jamii kwa kutoshiriki katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na rasilimali zao na kuchangia kuwepo na viashiria vya matumizi mabaya ya rasilimali zao.
Bw.Silumbu alisema Serikali imekuwa wazi kwa wananchi wake hasa kwa kutoa mwongozo elekezi wa jinsi ya kufanya ufuatiliaji huo, lakini wananchi wamekuwa kikwazo.
Alisema kuwa mwongozo huo umetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu -T
AMISEMI Desemba,
2009, ambao unawataka jamii wafanye ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na
rasilimali zao.
Bw.Silumbu alisema jamii imekuwa ikilalamika juu ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya rasilimali zao lakini hakuna jitihada zozote wanazofanya ili kuweza kupata haki hizo.
Alisema kuwa, asasi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi chini wa Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS) ambapo mpaka sasa tayari kata za Kitunda, Kivule, Msongola na Pugu zimefikiwa na mradi huu kwa awamu ya kwanza.
Subscribe to:
Posts (Atom)