Tuesday, March 18, 2014

BODI YA PAMBA YAJITOSA SAKATA LA QUTON










BODI ya Pamba nchini (TCB) Kanda ya Ziwa imetoa ufafanuzi kuhusiana na malalamiko ya wakulima wa zao la pamba wanaolalamikia kugoma kuota kwa mbegu za pamba zilizosambazwa na Kampuni ya Quton huku wengi wakidai kulipwa fidia. 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wiki iliyopita, Kaimu meneja wa bodi ya Pamba, Buluma Kalidushi baada ya kuwepo kwa malalamiko hayo, bodi yake iliunda timu ya kufuatilia ili kuweza kubaini ukweli wake lakini hata hivyo wizara kwa upande wake pia iliunda tume ya wataalamu ili kuchunguza malalamiko hayo. 

Kalidushi alisema kwa taarifa alizonazo tayari tume ya wizara imekamilisha kazi yake na kinachosubiriwa hivi sasa ni kutolewa kwa taarifa hiyo ili kuweza kubaini sababu zilizosababisha mbegu hizo zisiote katika baadhi ya maeneo huku maeneo mengine zikionesha matokeo mazuri. 

Alisema baada ya kutolewa kwa taarifa ya wataalamu hao kutoka wizarani ndipo itakapofahamika iwapo kuna umuhimu wa kulipwa fidia kwa wakulima waliopanda mbegu hizo na zikagoma kuota au kutolewa maelekezo mengine tofauti na suala la madai ya kutaka kulipwa kwa fidia.

"Ni kweli mbegu za Quton katika baadhi ya maeneo zimegoma kuota na zimesababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima, bodi tuliunda timu ya kufuatilia ili kuweza kubaini tatizo, lakini pia wizara iliunda tume na tayari imekamilisha kazi yake, tunasubiri kutolewa kwa taarifa. 

"Hata hivyo, ukweli ni kwamba tatizo la mbegu kutokuota limetokea kwa mbegu hizi za Quton, ni tatizo la kila mwaka hata kabla ya kuwepo kwa mbegu hizo, malalamiko yamekuwa mengi kwa vile mbegu hizo zina mwenyewe (Quton ), zamani mbegu zilikuwa za wakulima wenyewe hawakupiga kelele sana zilipogoma kuota," alieleza Kalidushi.

Alisema tatizo la mbegu kugoma kuota mara nyingi linachangiwa na wakulima wenyewe kuchafua kwa makusudi pamba yao pale wanapokwenda kuiuza kwa lengo la kutaka kuongeza uzito ambapo wengi wana tabia ya kuweka maji na magadi na hivyo kusababisha mbegu kuoza.

Alisema tabia ya kuweka maji kwa lengo la kutaka kuongeza uzito wa pamba pale inapopimwa inafaida kidogo sana ikilinganishwa na hasara anayoipata mkulima pale anaporejeshewa mbegu zinazotokana na pamba yake aliyoiuza huku akiwa ameiwekea maji na hivyo kujikuta mwenyewe akipata hasara kwa mbegu hizo kutokuota. 

Kwa upande mwingine kaimu meneja huyo alikanusha madai ya kukiukwa kwa taratibu za manunuzi kwa mujibu wa sheria katika kutoa zabuni ya usambazaji wa mbegu za pamba kwa kampuni ya Quton ambapo alisema taratibu zote zilizingatiwa na kampuni hiyo ndiyo iliyoshinda zabuni baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa.

No comments:

Post a Comment