Msitu wa Ruvu Kusini uliopo wilayani Kibaha,
Mkoa wa Pwani upo hatarini kutoweka baada ya kuvamiwa na wananchi wanaofanya
shughuli zao ndani ya eneo la msitu huo zikiwemo zile za ukataji miti, uchomaji
mikaa na ujenzi wa mabwawa ya samaki.
Kutokana na hatari hiyo, wananchi wa maeneo
hayo wameiomba Serikali kusimamisha shughuli zinazofanywa katikati ya msitu huo
kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kutoweka kwa msitu huo.
Mbali na hilo, wananchi wa vijiji vya Boko
Mnemera na Mpiji vilivyopo jirani na mashamba hayo wamekitupia lawama Kitengo
cha Mitambo na Mizani kilichopo chini ya Wakala wa Barabara nchini (Tanrods)
kuruhusu mitambo yao kuingia na kufanya uchimbaji wa mabwawa katika mashamba
hayo.
Wakizungumza na waandishi wa habari
waliotembelea maeneo hayo, wananchi wa maeneo hayo waliiomba Serikali kuingilia
kati uvamizi wa maeneo hayo na kutafuta suluhu haraka ili kuepusha hatari ya
ukame inayowanyemelea.Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpiji na Boko
Mnemera, Said Mwenyegoha, ameiomba Serikali kuingilia kati vitendo hivyo.
Alisema miongoni mwa waliovamia katika msiku
huo wameanzisha uchimbaji wa mabwawa ya samaki hatua anayosema haikufuata
taratibu za kupata kibali kutoka Serikali ya kijiji na kuufunga mkondo wa maji
unaotegemewa na wanakijiji hao.Mwenyegoha anasema tayari wametoa taarifa
ofisi za wilaya kuhusiana na uharibifu unaofanywa na wavamizi hao.
Hadi sasa
hakuna hatua za haraka zilizochukuliwa.Wamiliki wa shamba la mifugo la Soga na Alavi
Estate, lililoko maeneo ya jirani na msitu huo wa Serikali wanasema hatua
iliyofanywa na wavamizi ya kuingia katika maeneo ya mashamba na misitu hiyo
italeta athari kubwa kwa wanavijiji wa maeneo hayo.
Mmiliki wa Soga Faisal Edha, anasema mashamba
hayo pamoja na msitu yamekuwa na faida kubwa kwa Taifa kutokana na kuzalisha
maziwa lita 2,000 kila siku pamoja na kuzalisha mitamba na kusambaza kwa
wananchi maeneo mbalimbali nchini.
Alionya, endapo Serikali itashindwa kufunga
mabwawa hayo kuna uwezekano wa kutoweka kwa mashamba hayo pamoja na misitu huku
wananchi wa vijiji hivyo wakiwa hatarini kukosa maji.
“Tunaomba Serikali ichukue hatua haraka maana
iwapo wavamizi hawa wataachwa na hasa huyu aliyechimba mabwawa kuna uwezekano
wa mifugo yetu kufa kutokana na ukame,” alisema.
Naye Meneja wa Mashamba ya Alavi Estate, Amir
Mndeme anasema suala hilo lina athari kubwa kwa wanavijiji hivyo Serikali
haipaswi kulinyamazia jambo hilo bali lichukue hatua za haraka ili kunusuru
mashamba hayo kuendelea kutoa uzalishaji.
Akizungumzia suala la mtambo wa Tanroad
kuhusika katika uchimbaji wa mabwawa hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mitambo na
Mizani wa wakala huyo, Sylvester Semfukwe anasema kuwa mtambo huo ulikodishwa
Februari 14, mwaka huu na mtu mmoja (jina linahifadhiwa) na kwamba mamlaka hiyo
haikujua mtambo unaenda wapi na kufanya shughuli gani.
Anasema Kitengo cha Biashara cha mamlaka hiyo
kimekuwa kikikodisha mitambo yake kwa wananchi na mashirika bila kuhoji
shughuli zinazoenda kufanywa na kuitaja gharama ya ukodishaji wa mtambo huo kwa
saa nane kuwa ni Sh650,000 ambazo zililipwa na mteja aliyekodi mitambo hiyo.
WAJASIRIAMALI 16 kutoka Mikoa ya Mwanza, Pwani na Kagera
wamepata elimu ya usindikaji wa zao la muhogo na viwango vinavyozingatia ubora
unaokubalika katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA C).
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni,
wilayani Misungwi baada ya mafunzo hayo, mshauri wa usindikaji na masoko wa
IITA Dkt. Gabriel Nduguru, alisema wakulima wasindikaji wa zao la muhogo,
hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu viwango na ubora wa bidhaa zao.
Alisema kuwa mafunzo hayo kwa wasindikaji hao,
yalitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo Alisema wanafanya utafiti wa mazao
na kusaidia kuainisha viwango vinavyotumika kwa nchi za EAC, baada ya kuridhiwa
na mawaziri wa nchi za Jumuiya hiyo.
Alisema wananchi watafahamu viwango vya ubora baada ya
kuwapa mafunzo ya usindikaji na watazalisha chakula chenye ubora na kuuza
katika masoko ya uhakika na watajiongezea kipato .
cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na Shirika la
Viwango nchini (TBS ).
Alisema IITA ilifanya utafiti na kubaini changamoto hiyo kwa wasindikaji wengi
wa zao la muhogo, hivyo ikaamua kutoa elimu inayohusu ubora na viwango kwa
wasindikaji hao ili kuwawezesha kupata masoko ya uhakika.
"Wakulima na wasindikaji hao hawakuwa na elimu,
hivyo bidhaa zao hazikuwa bora na salama na zilitishia afya za walaji.Baada ya
kubaini hilo tukaona tuwafundishe jinsi ya kusindika muhogo salama kwa
kuzingatia viwango vya ubora kulingana na mahitaji ya walaji," alisema Dkt.
Ndunguru.
Dkt. Ndunguru alisema changamoto kubwa kwa wasindikaji
zao la muhogo, ni vifungashio na mitambo ya kisasa kwani ni kiwanda kimoja tu
ambacho hakitoshelezi mahitaji.
IMEELEZWA kuwa usimamizi hafifu wa kanuni na
sheria za uvuvi ndani ya Ziwa Victoria ndio chanzo kinachochangia kupotea kwa
samaki mkoani Mara. Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mfawidhi ulinzi na rasilimali
za uvuvi Mkoa wa Mara, Braison Meela wakati akitoa taarifa katika kikao cha
wadau wa uvuvi katika ziwa hilo kilichofanyika kwenye ukumbi wa uwekezaji
uliopo katika Ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Meela alisema kuwa kumekuwepo na wasimamizi
wabovu katika kusimamia kanuni na sheria ya uvuvi kuanzia ngazi ya kata hadi
Taifa hali inayochangia kupungua kwa rasilimali hiyo ambayo ndiyo inayoingiza
pato kubwa katika nchi hii .
Alisema kuwa lengo ni kuchukua hatua stahiki
ili kuwa na rasilimali endelevu ya samaki katika ziwa hilo litakalofikiwa iwapo
hatua sahihi na za makusudi zitachukuliwa dhidi ya wanaosababisha kupungua
wingi wa samaki hao ndani ya ziwa.
Akizungumzia kuhusu changamoto zilizopo
katika sekta hiyo alisema kuwa ongezeko la matumizi ya mbinu haramu ya uvuvi
kama vile matumizi ya dawa za kilimo ya kuvulia samaki, usimamizi hafifu wa
sheria na kanuni zake kama vile wataalam, BMU, wanasiasa na serikali ya vijiji
ambapo matokeo yanaachwa yanaenda kama yalivyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
maadili na ukiukwaji wa miiko ya utumishi kwa baadhi ya watendaji.
"Nyavu za timba ni nyavu ambazo zimekuwa
zikitumiwa mara kwa mara kuvulia samaki kwa njia ya uvuvi haramu na nyavu hizi
zinatokea nchi za nje kwani wanaozingiiza ni wenzetu kwa kuwa wanajua bidhaa
hiyo ina soko hapa kwetu hivyo tunapaswa kila mmoja kuwa mlinzi wa rasilimali
hii," alisema Meela.
Akizungumzia viashiria vya kupungua kwa
samaki alisema kuwa viwanda vya samaki vinazalisha kwa kiwango cha chini ya asilimia
hamsini ya uwezo wake, hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya wateja wao.
Mmoja wa wadau hao ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Butiama Magina Magesa
alisema kuwa inashangaza sana kuona hapa nchini hakuna viwanda vinavyozalisha
nyavu hizo, lakini nyavu hizo zimezagaa katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi
huku vyombo vya dola vimeshindwa kudhibiti uingizwaji wa nyavu hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa akifungua
kikao hicho alisema kuwa BMU ambao ndio kama ya kufuatilia matumizi mabaya ya
zana hizo lakini hao ndio wanaowakingia kifua wavuvi haramu kwa kuwaambia
wafiche zana hizo wakati wa oparesheni ili wakimaliza waendelee na shughuli zao
kama kawaida.
Alisema nchi jirani zinazozungukwa na ziwa
hilo wananufaika na mazao ya ziwa hilo lakini Mkoa wa Mara umeshindwa kunufaika
na mazao yanayotokana na ziwa hilo kwa sababu ya watu wa BMU kutokuwa na
maadili ya utendaji kazi kama dhamana yao.