Katika mwaka wa fedha 2012/13, Serikali ilitoa ruzuku ya tani
126,117 za mbolea ambapo jumla ya wakulima 940,783 walinufaika na tani
8,278 za mbegu bora za mahindi huku wakipata mbegu bora za mpunga tani
1,694.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa
Kilimo,Chakula na Ushirika Christopher Chiza ambaye alisema kuwa mipango
hiyo imetokana na kukubalika kwa baadhi ya mazao ya chakula kuruhusiwa
na kuwa mazao ya biashara.
Alikuwa akijibu swali la Martha Mosesi Mlata (Viti
Maalumu-CCM), ambaye alitaka kujua kama Serikali inatambua kwamba kuna
baadhi ya mazao ambayo ni chakula lakini yanatumika kama mazao ya
biashara hivyo kuna sababu ya kuyapa ruzuku.
Mlata alihoji pia sababu za wakulima wa Mkoa wa
Singida kuzuiwa wasilime zao la mahindi licha ya kuwa zao hilo linastawi
vizuri mkoani humo.
Waziri alisema Serikali ilijikita katika kutoa
mbolea ya ruzuku na pembejeo ili kuboresha uzalishaji wa mazao hayo na
kuhakikisha wakulima wanapata chakula cha kutosha na kuwaongezea kipato.
Alisema kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16, Wizara
kupitia mfumo wa matokeo makubwa imejiwekea malengo ya kuongeza
uzalishaji kwa kiasi cha mahindi tani 100,000 na mchele tani 290,000
katika mashamba mapya ya wakulima wakubwa na wadogo.
Kwa mujibu Chiza, katika miradi hiyo Serikali
inatarajia kutumia Sh 91.5 bilioni kugharimia ruzuku ya pembejeo za
mazao zikiwamo mbolea.