Friday, January 16, 2015

JINSI YA KUMTAMBUA KUKU ANAYE UMWA NA KUKU MWENYE AFYA


TOFAUTI ZA MUONEKANO YA KUKU MWENYW AFYA NA KUKU MGONJWA

KUKU MWENYE AFYA
    Macho na sura angavu
     Hupenda kula na kunywa maji
     Pua zilizo safi, upanga na undu mwekundu, manyoya
     laini na yaliyopangika vizuri
     Hupumua kwa utulivu
     Sehemu ya kutolea haja huwa kavu
     Kinyesi kikavu, cheupe na kisicho na rangi
     Hutaga mayai kawaida

 KUKU ASIYE KUWA NA AFYA NZURI(MGONJWA)
           Huonekana mchovu na dhaifu
           Hula na kunywa kidogo au zaidi ya kawaida
           Hutoa kamasi puani, ute na matongotongo; manyoya
           yaliyovurugika
           Hupumua kwa shida na kwa sauti
           Sehemu ya kutolea haja inakuwa na unyevunyevu na
           kinyesi kuganda
           Huharisha, kinyesi huwa na damu au minyoo
           Hutaga mayai machache au husimama kutaga kabisa
           Huwa na tabia ya kujitenga na wenzake katika kundi

NAMNA YA KUBORESHA UFUGAJI WA KUKU


Wafugaji wengi wa Tanzania wanafuga kuku wa kienyeji. Ndege hawa kwa kawaida wanafugwa sehemu za vijijini ambapo wanaachiwa huru kuzurura.

Kuna uwezekano mkubwa sana wa kizazi kujirudia kwa kuwa jogoo anaweza kumpanda mtetea ambaye alitokana naye, au kumpanda mtetea ambaye wamezaliwa pamoja. Kuzaliana kwa namna hiyo kunasababisha matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kudumaa, kupunguza uzalishaji wa mayai, kuwa na vifaranga dhaifu ambavyo ni rahisi kushambuliwa na magonjwa, na mengineyo mengi yasiyokuwa ya kawaida. Ufugaji huru ambao una udhibiti ni muhimu sana ili kuepuka kizazi kujirudia. Kuku wanaweza kuwekwa kwenye makundi na kuachiwa kwa makundi ili kuzuia uwezekano wa kuzaliana kwa kizazi kimoja.

Mfugaji anayetaka kufanikiwa katika ufugaji wa kuku wa kienyeji ni lazima achanganye mbinu za kienyeji na za kisasa. Hii inajumuisha njia zifuatazo:

Kuchagua aina/mbegu

Kuchagua mbegu inamaanisha: Mtetea au jogoo mwenye ubora wa hali ya juu , akiwa na sifa kama uzalishaji wa juu wa mayai au uzalishaji wa nyama, wanachanganywa na aina mfugaji alionayo, au kuboresha mbegu ambayo ni dhaifu. Kuna makundi matatu ya aina za kuku;

• Kuku wenye umbo dogo ni wazuri zaidi kwa uzalishaji wa mayai.
• Kuku wenye umbo kubwa ni wazuri zaidi kwa uzalishaji wa nyama.
• Mbegu iliyochanganywa ni nzuri kwa uzalishaji wa mayai na nyama.

Endapo mfugaji anataka kufuga kuku kwa ajili ya mayai, basi anaweza kuchanganya mbegu ya kienyeji aliyonayo na mbegu yenye umbo dogo ambao wana historia nzuri ya uzalishaji wa mayai, na kama anataka kuzalisha kwa ajili ya nyama, basi anaweza kuchagua wenye umbo kubwa. Na ambae anahitaji kwa ajili ya mayai na nyama, basi anaweza kuchanganya mbegu.

Chagua mbegu kwa umakini

Wafugaji wenye uzoefu huchanganya mbegu tofauti ambazo zina ubora na sifa maalumu, kama vile uwezo wa kukabiliana na magonjwa, ukubwa wa mayai, umbo, na kiasi cha chakula wanachohitaji.

Vigezo vifuatavyo vinaruhusu uchaguzi sahihi:

1. Mtetea au jogoo kati ya kilo 1 mpaka 2, anahesabiwa kuwa kwenye kundi la umbo dogo.
2. Kuku wote wenye uzito wa kilo 3 au zaidi wanahesabiwa kwenye umbo kubwa.

Kuku wenye kilo 2 mpaka 3 wanahesabiwa kuwa mbegu mchanganyiko (Chotara).

Uzalishaji mzuri wa kuku ni pamoja na kuhakikisha kuwa, kila baada ya mzunguko mmoja, jogoo anabadilishwa, au kuku wote pamoja na mayai yake wanauzwa na kuleta aina nyingine ili kuzuia kizazi kujirudia.  Ruhusu jogoo mmoja kuhudumia kuku 10 tu. Mfugaji pia anaweza kuzuia uwezekano wa kizazi kujirudia kwa kuweka kumbukumbu rahisi, kwa mfano, unaweza kuweka viota na kufahamu ni kuku yupi yupo kwenye kiota kipi na kwa muda upi.

Kumbukumbu ni muhimu

Uwekaji wa kumbukumbu ni lazima!  Kumbukumbu humsaidia mfugaji kufahamu kizazi na tabia za kila kuku ambaye amechaguliwa kwa ajili ya uzalishaji, kiasi kwamba anaweza kuelezea kuhusu kila kuku aliye naye bandani, kwa kuzingatia uzalishaji wa mayai na nyama

Thursday, January 15, 2015

UFUGAJI WA KUKU: BANDA LA KUKU WA KIENYEJI


UFUGAJI WA KUKU: BANDA LA KUKU WA KIENYEJI
Sifa za banda bora la Kuku
. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa kama ifuatavyo:

Liwe jengo imara
 Pasiwe na sehemu zilizo wazi kwenye msingi na kati ya ukuta na paa.
 Banda lijengwe na vifaa vinavyopatikana katika mazingira yako ili liwe na gharama utakayoweza kumudu.
 Unaweza kutumia matofali ya udongo, udongo, miti, fito,n.k. Ukitumia fito au mabanzi ondoa maganda ili kuthibiti mchwa.
 Jengo mara litazuia maadui kama panya, vicheche, paka, nyoka na wezi kuingia ndani ya banda na kuwadhuru au kuwaiba kuku.

Liwe rahisi kusafisha
 Kuta na sakafu visiribwe zisiwe na nyufa ili kurahisisha kusafisha.
 Pia itadhibiti kusiwe na wadudu wa kujificha katika nyufa kama papasi, viroboto n.k.
 Sakafu ya banda lazima iwekewe matandazo kama pumba ya mpunga au maranda ya mbao au mabaki ya mazao au nyasi kavu kutegemeana na kinachopatikana kwa urahisi katika mazingira yako.
 Matandazo haya husaidia kunyonya unyevu unaotokana na kinyesi cha kuku au maji yanayomwagika katika banda.
 Banda hubakia kavu bila kuwa na harufu mbaya na wadudu kama inzi hata vimelea vya magonjwa hudhibitiwa.

Eneo la nje kuzunguka banda kuwe na usafi wa kudumu
Hali ya usafi nje ya banda itafanya wadudu kama siafu au mchwa na wanyama kama panya na paka mwitu wakose maficho. Nje ya banda ndani ya uzio kuwe na miti midogo na mimea mingine midogo kwa ajili ya kivuli.
Ufugaji wa nusu huria
Banda liwe na nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo: Kwa kawaida eneo la mita mraba moja hutosha kuku wanne wanaotaga au kuku 8 wa nyama. Nafasi ya mita mraba 1 inatosha vifaranga 16 hadi kufikia umri wa majuma manne.
Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha: Banda linaloweza kuingiza hewa safi na kutoka ndani yake hubaki kavu. Harufu mbaya hutoka na kuku huweza kupumua hewa safi. Hii husaidia pia kudhibiti kuzaliana kwa vimelea vinavyosababisha magonjwa,hivyo hudhibiti magonjwa.
Lisiwe na joto sana au baridi sana: Panda miti ya kuzunguka banda lako ili eneo liwe na kivuli cha kutosha na pia lisiwe na upepo mkali.Kama hali halisi ya eneo la kufugia ina joto kubwa kwa vipindi virefu paa la banda wakati wa ujenzi liinuliwe juu zaidi kuruhusu mzunguko zaidi wa hewa na joto la paa ( kama ni la bati) liwe mbali juu ya kuku.
Joto kwenye banda linaweza kusababishwa na msongamano wa kuku, hivyo mfugaji aangalie aweke idadi ya kuku inayowiana na ukubwa wa banda lake.

Paa lifunike ukuta kwa sehemu kubwa
Liwe imara na lisilovuja. Waweza kutumia mabati, nyasi, madebe, makuti n.k. kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya kuezekea.Wakati wa kuezeka paa lisiishie karibu sana na ukuta bali liwe na sehemu kubwa iliyozidi ukuta kuzuia mvua kuingia ndani kama ni ya upepo ( angalia mchoro hapa chini).

Vifaa vinavyohitajika katika banda la kuku
Kuku wakifugwa kwa mtindo wa nusu ndani na nusu nje wanahitaji huduma mbalimbali ndani ya banda na ndani ya wigo. Ili kutoa huduma hizi vifaa vifuatavyo ni muhimu viwe katika banda:



Kinywesheo cha kujitengenezea

Kuna njia nyingi za kutengeneza vyombo vya kuwekea maji ya kuku ya kunywa.
 Aina ya mojawapo unayoweza kutumia ndoo au debe la lita kumi au ishirini ya plastiki. Kata ndoo hiyo pande nne kutoa nafasi ya kuku ya kunywea kama kielelezo kinavyoonyesha. Tengeneza idadi ya vyombo hivi inayowiana na wingi wa kuku ulionao.
 Au waweza kutumia sufuria au beseni pana kiasi. Hii huwekewa tofali au jiwe safi pana baada ya kuwekewa maji ya kunywa ili kuzuia kuku wadogo wasizame na maji yasichafiliwe kirahisi.
 Vifaa maalum vya kunyweshea kuku vinapatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo.




Kilishio
Vyombo hivi ni muhimu viwe vimetengenezwa vizuri ili visiwe chanzo cha upoteaji wa chakula. Unapotengeneza kilishio cha kuku kumbuka kuwa kuku wana tabia ya kuchakura. Husambaza au kupekua chakula kwa miguu hata kwa midomo ili kupata chakula cha chini.
Tabia hii husababisha kumwagwa kwa chakula kingi chini na kusababisha hasara. Unaweza kudhibiti tatizo hili kwa kutengeneza vyombo visivyoruhusu kuku kuchakura kama inavyoonyeshwa kwenye kielelezo hapa chini.
Unaweza kutengeneza kilishio hiki wewe mwenyewe au fundi seremala waliopo katika eneo unaloishi. Inafaa kilishio kiwe chembamba ili kuku wasiweze kuingia. Pia kinatakiwa kiwe kirefu ili kuku waweze kula bila kusongamana.


Muunganiko wa Viota
Zipo aina tofauti za viota ambazo hutumika kwa ajili ya kutagia. Ipo aina ya ambayo ni ya kutagia kuku mmoja mmoja. Vipimo vinavyopendekezwa kwa kila kiota ni upana wa sentimita 30, urefu sentimita 30 na kina sentimita 35. Upande wa mbele uachwe wazi ila sentimita 10 za kwanza kutoka chini zizibwe na ubao ( angalia kielelezo). Weka idadi ya viota inayotosheleza kuku ulio nao.
Pia ipo aina nyingine inayoweza kutumiwa na kuku zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja. Ni kama kiota kimoja kilichogawanywa katika vyumba kadhaa. Ila kila chumba kina vipimo kama vya kiota kimoja( angalia picha hapa chini).Aina hii ya kiota ina upana wa sentimita 30 na kina sentimeta 35 na urefu wake unategemea idadi ya viota.
Viota vinatakiwa kuwa na giza ili kuku wasiogope kuingia kutaga ndani yake. Pia giza husaidia kupunguza tabia ya kuku kula mayai na kudonoana. Kiota kinafaa kuwekwa mahali ambako ni rahisi kuku kuingia na kutoka. Vile vile iwe ni sehemu itakayorahisisha usafishaji wa kiota chenyewe.



Mbegu bora ya Alzet ambayo mkulima atafaidika na Alzeti hii
Nyanya iliyostawi nakukomaa vyema huwa na Mavuno bora ambayo hukuza kipato cha mwananchi/mkulima
kijana aliye jikita kwenye kilimo cha matikiti maji
   Dalili za mavuno Bora ya Mahindi kwa mwananchi wetu hujionesha mapema