Ugonjwa hatari unaoshambulia mahindi na kusababisha
saratani kwa binadamu umeingia nchini na wakulima sasa wametahadharishwa
kutokula mahindi hayo wala unga ambao haujakobolewa.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huo huota
‘fungus’ ambao ina sumu inayoitwa ‘Aflatoxin’ ambayo inaweza kusababisha
madhara kwa wanyama na binadamu hususan ugonjwa wa saratani.
Mbali na kutikisa mikoa kadhaa na kusababisha
hasara kubwa kwa wakulima, ugonjwa huo ambao umeanzia nchini Kenya
unaendelea kusambaa kwa kasi na sasa umeingia pia nchini Uganda.
Awali ugonjwa huo uliripotiwa kuzikumba wilaya za
Babati mkoani Manyara na Meatu mkoani Shinyanga tu, lakini sasa
umesambaa hadi katika mikoa jirani ikiwamo Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama jana
aliithibitishia blog hii kuwa mkoa wake umekumbwa na ugonjwa huo na
tayari umesambaa katika wilaya tatu; Moshi Vijijini, Siha na Hai. “Ni
kweli baadhi ya wilaya zimekumbwa na ugonjwa huo, bahati mbaya sana
hauna tiba na unasambaa kwa kasi... Wataalamu wanaendelea kuwaelimisha
wakulima kutambua dalili zake,” alisema Gama.
Gama alisema endapo mkulima atabaini shamba lake
kushambuliwa na ugonjwa huo katika hatua za awali, anachotakiwa kufanya
ni kung’oa mimea yote ya mahindi na kuichoma moto.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga alisema
takriban hekari 14 zimeshambuliwa na ugonjwa huo katika shamba la Watawa
wa Kanisa Katoliki Mailisita na shamba la mkulima wa Lambo.
Alisema tayari wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo ya Selian (SARI) ya Jijini Arusha wamefika wilayani humo na
kutoa tahadhari kwa wakulima juu ya athari za ugonjwa huo.
Mfanyabiashara mashuhuri wa mjini Moshi, John Bennett anayemiliki
mgahawa wa Golden Shower aliitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi na
wafanyabiashara na kuchukua tahadhari.
“Utajuaje unga wa dona haukutokana na hayo mahindi
au pumba ya chakula cha mifugo hayakutokana na hayo? Hili jambo ni zito
sana si la kufanyia utani hata kidogo”alisema Bennett.
Mkulima wa Kijiji cha Kikavu Chini wilayani Hai,
Justine Mvungi alisema wataalamu kutoka SARI wamewataka kuchoma moto
miche ya mahindi ambayo watagundua imeshambuliwa.
“Wametuambia takriban shamba likishambuliwa,
tung’oe mahindi hayo na kuyachoma moto, wametuambia kama tulishavuna
basi tukoboe mahindi hayo maana kiini chake kina madhara,”alisema.
“Aliongeza kusema” hata tukikoboa mahindi
tumeambiwa zile pumba zake tusiipe mifugo kwa sababu itaathirika…
Ugonjwa huu wa mmea wa mahindi umeleta taharuki kubwa kwa wakulima na
wananchi.”