Thursday, April 25, 2013

Waziri wa Kilimo atiwa msukosuko bungeni

 Hotuba ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza imezidi kupingwa kwa madai kuwa imejaa majibu ya uongo kwa Watanzania.
Licha ya suala hilo, kitendo cha Waziri Chiza kupeleka mradi wa bwawa la umwagiliaji Wilaya ya Kakonko ambako ndiko jimboni kwake, kilionekana kuwakera wabunge.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika juzi, Mbunge wa  Viti Maalumu, Azzah Hilali (CCM) alisema Hotuba ya Waziri Chiza ilitolewa bungeni bila ya kufanyiwa utafiti wa kutosha, kwani vitu vingi vinaonekana havina uhalisia.
“Mambo mengi hapa ya Waziri hayana ukweli, kwani unaposema chakula hutolewa kwa wananchi mara baada ya wakurugenzi kuleta maombi siyo kweli,” alisema Hilali.
Alisema tangu Oktoba mwaka jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, aliomba chakula cha msaada lakini kilipelekwa nusu Februari mwaka huu.
Pia, Mbunge huyo alikosoa hotuba hiyo kuwa imetumia jina la Waziri Mkuu vibaya, kwani kiongozi huyo aliagiza chakula cha msaada kupelekwa Shinyanga tangu muda mrefu, lakini hakuna kitu chochote kilichofanyika.
“Ndiyo maana tunasema mnadanganya, wewe fikiria hata hao wataalamu wenu mnaowatuma wanaishia maofisini, huku mnakuja kutoa taarifa kuwa wamefika huko na kufanya kazi, jamani Watanzania wamechoshwa kudanganywa,” alilalamika.
Kuhusu mradi wa bwawa la Kakonko, Mbunge huyo alimtuhumu moja kwa moja Waziri Chiza kuwa anapanga miradi ya maendeleo kwa upendeleo.
Alisema Serikali ilitangaza Kahama kuwa italisha Mkoa wa Shinyanga, lakini hakuna mradi hata mmoja ulioelekezwa wilayani humo, badala yake miradi imepelekwa maeneo yenye neema ya mvua na kuhoji dhambi waliyomfanyia Mungu.

No comments:

Post a Comment