Bibi Li Haibo ni ofisa wa kamati ya kijiji kimoja kilichoko kaskazini
mashariki mwa China. Mwezi huu amepata kazi mpya, ambayo ni kuwafundisha na
kuwaelekeza wanakijiji kufanya biashara kupitia Internet, ili kuwasaidia
kuongeza kipato chao.
Mwishoni mwa mwezi Februari, mkoa wa Jilin ulifanya mkutano wa mafunzo ya
wafanyabiashara kupitia Internet. Viongozi wa idara za biashara za kaunti
mbalimbali na wahitimu wa vyuo vikuu wanaofanya kazi katika kamati za vijiji
mkoani humo, walikusanyika pamoja kusikiliza mafunzo ya wataalamu wa kampuni ya
Alibaba ambayo ni kampuni maarufu inayotoa huduma ya biashara kupitia Internet
nchini China.
Mkoa wa Jinlin ambao unazalisha mazao ya kilimo kwa wingi lakini uchumi hake
haujaendelezwa vizuri, ulipanga kuwasaidia wakulima katika vijiji 100 kufanya
biashara ya bidhaa zenye sifa ya kipekee za huko kupitia Internet.
Takwimu zilizotolewa na kituo cha utafiti cha Ali kinachomilikiwa na kampuni
ya Alibaba zinaonesha kuwa, hadi tarehe 30 Novemba mwaka 2013, maduka ya ngazi
ya vijiji na miji midogo yaliyosajiliwa kwenye tovuti ya Taobao.com yalikuwa
milioni 1.05. Idadi hiyo iliongezeka kwa laki 4 na 60 elfu kuliko mwaka 2012,
ambalo ni ongezeko la asilimia 76.3.
Bibi Li Haibo sasa ni naibu katibu wa kamati ya chama ya kijiji cha
Erdaohezi mjini Dunhua mkoani Jilin. Ni mhitimu wa chuo kimoja cha uchumi, na
alianza kufikiria njia ya kuwasaidia wanakijiji kuuza mazao ya ginseng na uyoga
mweusi.
Bibi Li anasema, hata katika vijiji viliyoko nyuma kiuchumi, watu wananunua
bidhaa kwa wingi kupitia Internet, na makampuni mbalimbali ya usambazaji wa vitu
yameanzisha matawi yao vijijini, hivyo biashara kupitia Internet ina
mustakabali mzuri.
Gongzhuling ni moja ya kaunti zilizoko mkoani Jilin. Mamia ya makampuni ya
huko yameanza kuuza bidhaa zao kupitia Internet, lakini bidhaa nyingi zinauzwa
katika kaunti hii tu.
Mkurugenzi wa idara ya biashara Bw. Sun Dianpu ana mpango wa kuwaelekeza
wazalishaji na wauzaji kujifunza ujuzi kuhusu biashara kupitia Internet,
kuanzisha maduka kwenye tovuti, na kuuza mahindi na maharagwe yanayozalishwa
huko nchini kote.
Katika mikoa ya pwani ya Jiangsu, Zhejiang na Shandong, baadhi ya vijiji
vimepewa jina la "vijiji vya Taobao", kwa sababu maelfu ya wanavijiji
wameanzisha maduka yao kwenye tovuti ya Taobao.com.
Ripoti ya maendeleo ya biashara kupitia Internet katika kaunti za China
mwaka 2013 iliyotolewa na kituo cha utafiti cha Ali mwezi Januari inaonyesha
kuwa, kati ya kaunti 100 zinazopata maendeleo zaidi katika biashara kupitia
Internet, kauti 49 ni za mkoa wa Zhejiang.
Katika kijiji cha Liucun mjini Yiwu mkoani Zhejiang, karibu kila familia
inashughulikia mauzo ya bidhaa kupitia Internet. Thamani ya mauzo ya maduka
zaidi ya 2000 ya wanakijiji hao ilikuwa yuan bilioni 2 mwaka jana.
Mkoa wa Jilin pia umechukua hatua ya kujenga "vijiji vya Taobao"
na kaunti za biashara kupitia Internet. Jumba la Jilin ni moja kati ya jukwaa
kubwa la biashara linalojengwa.
Mkurugenzi wa idara ya biashara ya Jilin Bibi Cong Hongxia anasema, jumba
hilo litakusanya bidhaa kutoka sehemu mbalimbali, zikiwemo mchele, maharagwe,
ginseng, vyura, maji yenye madini, uyoga mweusi na matunda ya blueberry
yanayozalishwa kwenye mlima Changbai.
Naibu meneja mkuu wa kampuni ya Alibaba Bw. Gao Hongbing anasema, mikoa ya
pwani iliyoko kusini mashariki mwa China imetangulia kuendeleza biashara
kupitia Internet na imepata maendeleo ya kasi. Ingawa mikoa iliyoko kaskazini
mashariki na kaskazini magharibi mwa China ilichelewa kuendeleza shughuli hizi,
lakini bado inaweza kupata fursa nyingi.
Takwimu za kituo cha utafiti cha Ali zinaonesha kuwa, hadi mwezi Desemba
mwaka jana, China imekuwa na "vijiji 20 vya Taobao", ambavyo viko
katika mikoa saba ikiwemo Hebei, Shandong, Jiangsu, Zhejiang na Guangdong.
Wanavijiji wa vijiji hivyo wameanzisha maduka elfu 15 kwenye tovuti ya Taobao.com
ambayo yanashughulikia mauzo ya bidhaa za majumbani, nguo, mifuko, mazao ya
kilimo, bidhaa ndogondogo, na vitu vinavyotumiwa wakati wa michezo au utalii.
Shughuli hizi zimewasaidia wanakijiji elfu 60 kupata kazi.
Kituo cha utafiti cha Ali kinasema, kama zaidi ya asilimia 10 ya watu katika
kijiji kimoja wanafanya biashara kupitia Internet, na thamani ya mauzo inazidi
yuan bilioni 10, basi kijiji hicho kinaweza kuitwa "kijiji cha
Taobao".
Wataalamu wanaona kuwa, wanavijiji wengi kufanya biashara kupitia internet
ni jambo la kipekee nchini China, na mwaka huu biashara hiyo itaendelea kupata
maendeleo ya kasi.