Friday, March 7, 2014

ALLIANCE GINNERIES LTD WASHAURI SERIKALI ITOE ELIMU UBORA WA MBEGU MPYA




UONGOZI wa kinu cha kuchambua zao la Pamba cha Alliance Ginneries Ltd, Wilayani Bariadi, Simiyu umeishauri Serikali itoe elimu kuhusu ubora wa mbegu mpya ya UKM08 ili kuondoa mkanganyiko kwa wakulima na kuiondoa sokoni mbegu ya UK91 ili kuimarisha na kuboresha kilimo cha mkataba.

Pia kampuni hiyo imewekeza kwa kusambaza tani 20,000 za mbegu hiyo aina ya UKM08 kwa wakulima wa mashamba darasa, katika vijiji vya Ikungulyabeshi, Nguliati, Kilalo, Ikungulyabashashi na Nyamagana, Kata ya Kasoli.

Ushauri huo ulitolewa juzi na meneja wa kinu hicho cha Alliance, Boaz Ogola, alipozungumza na waandishi wa habari, waliotembelea mashamba darasa yanayosimamiwa na kinu hicho mkoani Simiyu, baada ya kumalizika kwa mkutano wa wadau wa zao la pamba (Ginners) wa Wilaya za Bariadi na Itilima, kuhusiana na kilimo cha mkataba na changamoto zake.

 Alisema mbegu ya UK91 ambayo imedumu sokoni kwa kipindi cha miaka zaidi ya 10 imechoka, hivyo kusababisha wadudu waizoee na kuishambulia kwa urahisi, ambapo aliwataka wakulima kuacha kuitumia na kuendelea nayo ni kuzidi kujididiza kiuchumi.

Ogola alisema madai ya baadhi ya wakulima na wanasiasa kuwa mbegu hizo za UKM08 zisizo na manyoya hazioti ni uongo uliopitiliza, bali zimeonesha kuwa na tija kwa wakulima tofauti na mbegu ya UK91 ambayo uzalishaji wake kwa ekari ni kilo 200 hadi 300.

"Kitaalamu ili pamba iwe na tija kwa mkulima, mbegu isikae sokoni kwa miaka 10, inachoka na wadudu wanaizoea, hivyo nguvu ya uzalishaji inapungua. UK 91 imechoka sasa inapaswa iondoke badala yake wakulima watumie UKM08 ambayo imeonyesha tija na ina uwezo wa kuzalisha kilo 800 hadi 1,200 kwa ekari,"alisema Ogola na kuongeza;

"Uwekezaji huo wa tani 20,000 za mbegu za UKM08 kwa wakulima tulioingia nao mkataba, tunaamini baada ya miaka miwili tani milioni 1,440,000 zitakuwa zimezalishwa mbegu za kutosheleza mahitaji ya wakulima," alisema.

Alisema mbegu hizo zina tija kwa pande zote kwa mkulima na mchambuaji endapo zitapandwa na kutunzwa kitaalamu na baada ya kuvuna na kuchambuliwa pamba hiyo mbegu bora zitapatikana kwa asilimia 75. 

 

 Alidai kwamba baada ya kuchambuliwa kwa pamba uzalishaji wa nyuzi ni asilimia 33, mbegu asilimia 63 na asilimia 2 ni taka (west) kulinganisha na mbegu ya UK91. Hivyo serikali haina budi kuiondoa mbegu ya UK91 sokoni ili wakulima watumie UKMO8 ambayo ina tija kwao na yenye uwezo wa kuzalisha kilo 800 hadi 1,200 kwa ekari.

Aidha mratibu wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo cha zao la Pamba na Viwanda vya nyuzi (CDTP), Donald Sayi, aliwataka wawekezaji wa zao hilo kutokana na uzalishaji wake kushuka waangalie na kuwekeza kwenye maeneo wanayoweza kupata faida.

Alisema wakulima wanawategemea wawekezaji hao ambao ni wanunuzi na wachambuzi, hivyo mapato yao yakiimarika, halmashauri pia zitapata mapato mazuri na kuzishauri zitenge asilimia 10 ya mapato hayo kwa ajili ya elimu ya huduma za ugani kwa wakulima.
"CDTP hatuna nia ya kumweka mtu pembeni, tunataka twende sote kwani mafanikio ni yetu wote. Wakulima wapate faida kwa jasho lao kadhalika na wachambuzi pia. Kipato kikiimarika kati ya wakulima na wachambuzi ni faraja kwetu,"alisema Sayi.

Alisema kilimo cha mkataba cha zao la pamba kinafadhiliwa na Tanzania Gatsby Trust (TGT), ambapo CDTP ni washauri, lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikipinga kwa madai kuwa wanunuzi na wachambuaji wa zao hilo wanawanyonya wakulima kwa kuwakopesha pembejeo, mbegu na viuadudu, jambo ambalo si kweli.


1 comment: