FURUSA ZA UWEKEZAJI
KATIKA MKOA WA MANYARA
Mkoa una fursa nyingi za uwekezaji hususani katika huduma za Kiuchumi
(Kilimo na Mifugo, Viwanda, Biashara, Utalii na Madini); Kijamii (Elimu, Afya
na Maji); na Kiutamaduni (Michezo na Utamaduni).
FURSA ZA UWEKEZAJI
KATIKA HUDUMA ZA KIUCHUMI KILIMO
Kuna maeneo makubwa yanayofaa kwa shughuli za kilimo cha kwaida na kilimo
cha umwagiliaji katika Mkoa. Mazao yanayozalishwa kwa wingi ni pamoja na
Mahindi, Alizeti, Mbaazi, Mtama, Ngano, Maharage, Miwa, Vitunguu Maji, Vitunguu
Saumu na Mpunga ambayo hutumika kama mazao ya Biashara na Chakula kwa wakazi wa
Mkoa, Mikoa jirani na Nchi jirani za Kenya, Somalia, Ethiopia, Eritiria na
Sudani. Hivyo wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika sekta hii. MIFUGOMkoa una zaidi ya mifugo milioni 2. Wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika sekta hii hususani katika uanzishaji wa ranchi na viwanda vikubwa na vidogo vya kusindika mazao ya mifugo ambayo ni nyama, maziwa na ngozi. Fursa nyingine ya kuwekeza katika sekta hii ni ujenzi wa majosho na mabwawa kwa ajili ya kuogesha na kunyweshea mifugo.
VIWANDA
Mkoa unawakaribisha wawekezaji ili waanzishe na kuwekeza katika viwanda
Vikubwa, vya kati na Vidogo kwa ajili ya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na
sekta nyingine. Kwa sasa Mkoa una Kiwanda kikubwa cha Mbolea cha Minjingu
ambacho husambaza mbolea yake ndani na nje ya Mkoa na Kiwanda cha kusindika
nyama kilichopo Wilayani Simanjiro. Kadhalika, Mkoa unakadiriwa kuwa na viwanda
vidogovidogo 4560 vinavyofanya kazi za: Kusindika Nyama na Maziwa, mafuta ya
Alizeti, Kusaga na kukoboa nafaka na Kutengeneza Mkaa usiotoa moshi wenye
athari.
BIASHARA
Tayari makampuni kadhaa kama vile Kampuni ya Usafirishaji ya Mtei ‘express’,
kampuni za Simu za Vodacom, Airtel, Zantel na Tigo na taasisi za fedha kama
Benki ya Posta Tanzania, NMB, NBC, CRDB, EXIM nk. wanaendelea na shughuli
mbalimbali za biashara ndani ya Mkoa. Hata hivyo bado kuna fursa nyingi za
kuwekeza hususani katika uanzishaji wa maduka makubwa yenye bidhaa mbalimbali,
hoteli za kitalii, vituo vya utamaduni, huduma za usafirishaji, mawasiliano na
shughuli za kibenki. UTALII Mkoa una maeneo mazuri ya vivutio vya utalii
ambavyo ni Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Ziwa Manyara ambako hupatikana aina
mbalimbali za wanyamapori kama Simba, Chui, Chita, Twiga, Pundamilia, Swala,
Nyati, Pofu, Ngiri, Mbuni, Korongo nk. Eneo jingine la utalii ni Yaeda Chini
ambako upatikana jamii ya Wahadzabe ambao huishi kwa kutegemea uwindaji,
matunda, mizizi na asali. Hivyo, Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuanzisha na
kuwekeza katika hoteli na vituo vya utamaduni kwa ajili ya kutoa huduma muhimu
kwa Watalii mbalimbali wanaotembelea Mkoa huu.
MISITU
Wawekezaji wanakaribishwa katika Mkoa kuwekeza katika shughuli za Ufugaji
nyuki na uzalishaji Asali. Mkoa una eneo lenye ukubwa wa hekta 927,526 za
hifadhi za Misitu zilizohifadhiwa kisheria ambamo shughuli za ufugaji nyuki na
uzalishaji Asali zinaweza kufanyika. Tayari baadhi ya wananchi wanaendelea na
shughuli hii katika misitu asili na binafsi iliyopo katika maeneo mbalimbali ya
Mkoa.
MADINI
Mkoa una utajiri mkubwa wa madini ya Tanzanite ambayo yanathamani kubwa na
hayapatikani mahali popote duniani isipokuwa Mkoani Manyara Wilaya ya Simanjiro
eneo la Mirerani. Madini mengine yanayopatikana Mkoani hapa ni pamoja na: Ruby,
Green Garnet, Green Tourmaline na Rhodilite. Ukiacha madini ya Tanzanite,
hakuna uwekezaji katika aina nyingine ya madini tajwa hapo juu hivyo Wawekezaji
wanakaribishwa kuwekeza katika Sekta ya Madini.
FURSA ZA UWEKEZAJI
KATIKA HUDUMA ZA KIJAMII
Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta za Elimu, Afya na Maji
kwani huduma zinazoendelea kutolewa kupitia Sekta hizi bado hazitoshelezi na ni
duni katika baadhi ya maeneo. Lengo kuu la Mkoa ni kuimarisha Sekta hizi ili
kusaidia kuleta maendeleo ya haraka na kuondoa umaskini kwa Wananchi.
FURSA ZA
UWEKEZAJI KATIKA HUDUMA ZA KITAMADUNI
Ili kudumisha tamaduni zilizopo, Mkoa kupitia Hospitali ya Rufaa ya Haydom
iliyopo Wilayani Mbulu inajenga kituo cha Utamaduni (4corners) kitakachofanya
utafiti wa mila na desturi za makabila 4 ya Mkoa wa Manyara ambayo ni
Wahadzabe, Wanyaturu, Wairaqw na Wabarbaig. Vilevile, Mkoa unakituo cha Redio
cha kijamii cha ORKENERI RADIO SERVICE 94.40RS FM kilichopo Wilayani Simanjiro
kinachofanya kazi kubwa ya kutangaza utamaduni wa jamii ya Kimaasai. Hata hivyo
Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuanzisha vituo vingine vya Utamaduni katika
maeneo mbalimbali kama vile Yaeda Chini ili kuwavutia zaidi Watalii. Aidha,
Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Michezo ya aina mbalimbali kwani
kwa Miaka mingi sasa Mkoa umekuwa chimbuko la Wanariadha maarufu nchini
Tanzania ambao walipeperusha Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali
ndani na nje na kuuletea sifa Mkoa na Nchi. Miongoni mwawanariadha hao ni;
Gidamis Shahanga, Joh Bura, John Stephen Akhwari, Zakayo Malekwa na Simon
Robert Naali.