Wednesday, February 19, 2014

KILIMO CHA KUTUMIA MAHEMA CHAINUA UZALISHAJI WA KILIMO NCHINI KENYA



 




Wakikabiliwa na eneo dogo la kulima kutokana na kukua kwa idadi ya watu na hali za hewa zisizotabirika, wakulima wengi wa Kenya wamegeukia teknolojia ya kilimo cha mahema kama njia ya kuongeza uzalishaji na kunyanyua kipato chao.
Kukua kwa umaarufu wa kilimo wa mahema kulioneshwa katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya kila mwaka mjini Nairobi mwezi wa Oktoba ambapo waoneshaji wa kilimo cha kutumia mahema walisema kuwa waliona kuinuka kwa hamu ya umma katika kilimo hicho.
"Wakenya wengi wameanza kufuata kilimo cha kutumia mahema kwa sababu kinahitaji mtaji mdogo ili kuanzisha na wakulima wanaweza kuzalisha zaidi katika shamba dogo," alisema Moses Khaemba wa Kampuni ya Hortipro Limited, iliyoko Nairobi ambayo inatengeneza mahema ya kilimo kwa gharama ndogo.
Pamoja na kuwa inakuwa ya gharama ndogo na rahisi kuyaweka, mahema ya kilimo pia gharama ndogo ya ushughulikiaji, yantumia maji kwa ufanisi na yanaweza kuhamishwa baina ya vitalu, alisema, na kuongeza kuwa wakulima wanaweza kuona faida yake kuanzia mavuno ya kwanza
"Kilimo cha kutumia mahema ya plastiki kina faida nyingi," Khaemba aliiambia Sabahi. "Faida hizi ni pamoja na uzalishaji wa juu zaidi na wa kuendelea kwa kila ekari moja, jambo lenye maana ya kupata faida kubwa zaidi, kujikinga na masuala ya hali ya hewa kama vile ukungu na upepo, kutokuwepo na hatari ya wadudu waharibifu, kupata mwanga asilia na upitishaji wa hewa, miongo mirefu ya upandaji na matumizi madogo ya maji, hasa katika maeneo yenye ukame."
Ukubwa wa mahema ya kilimo unategemea na uwezo wa mkulima wa kuyashughulikia na ukubwa wa shamba, alisema. Wastani wa kila hema moja ni upana wa mita 8 na urefu wa mita 30 na hugharimu shilingi 150,000 (dola 1,800). Kampuni imepokea zaidi ya maombi 1,000 ya mahitaji kutoka kwa wakulima mwaka huu -- ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na 2011 -- vivyo hivyo na ongezeko la mahema mengi katika shamba hilo hilo, Khaemba alisema.
Mahema ya kulimia yanaweza kuwa ama katika muundo wa jadi kama nyumba au muundo wa upenyo - marefu yakiwa yamefunikwa kwa plastiki juu ya mazao. Wakulima wasema kwa kutumia mahema yenye umbo la upenyo, wanaweza kuzalisha zaidi kuliko katika ardhi ya wazi.
"Mimi ninayo mahema mawili katika shamba langu la ekari tatu huko Karen Estate mjini Nairobi ambako nimepanda nyanya," Margaret Wanjiku, mweny umri wa miaka 54, aliiambia Sabahi.
Wanjiku, ambaye alistaafu miaka mitano iliyopita kutoka shirika moja la kimataifa la msaada, alisema kuwa mmea wa nyanya unaweza kuzalisha kilo 16 hadi 20 za nyanya.
Ingawa bei hubadilikabadilika kutokana na upatikanaji wa bidhaa na mahitaji, alisema kuwa kila mita mraba moja ya nyanya humuingizia kiasi cha shilingi 3,000 (dola 35). "Ninauza nyanya zangu kwenye duka kubwa iliopo karibu na nyingine kwa majirani zangu," alisema.
Amos Karanja ametenga sehemu ya shamba lake la robo ekari huko Kitengela, Jimbo la Kajiado, kwa ajili ya kulima nyanya ndani ya mahema. "Ingawa ninayo kazi ya mchana, ninajaribu aina hii ya kilimo kama njia ya kupata mapato ya ziada ili kuisadia familia yangu," aliiambia Sabahi.
Dan Wanjohi kutoka kampuni Daner Greenhouse Limited huko Ongata Rongai, eneo la makazi ya watu katika Mkoa wa Bonde la Ufa, alisema kuwa kimwonekano aina yoyote ya mboga inaweza kulimwa katika mahema ya kilimo, ikiwa ni pamoja na matango, vitunguu na kabichi.
"Wakulima wengi nchini Kenya wanapendelea kulima nyanya kwa sababu ni mmea unaotoa mazao mengi na mtu hupata faida ndani ya miezi mitatu baada ya kuotesha," aliiambia Sabahi.
Alisema kuwa kampuni yake inatumia chuma cha pua katika ujenzi wa hema la ukubwa wa mita 8 kwa 30 na huuzwa kwa shilingi 200,000 (dola 2,300) kwa moja. Gharama ni pamoja na kulaza bomba kwa ajili ya umwagiliaji maji kwa matone.
Hata hivyo, wakulima ambao hawawezi kumudu gharama za majengo ya chuma cha pua, bado wanaweza kutumia mahema ya vipenyo kwa kutumia mbao kwa gharama ya chini zaidi. "Nililipa shilingi 70,000 (dola 818) kwa kujenga hema langu," Karanja aliiambia Sabahi.

No comments:

Post a Comment