Wednesday, February 19, 2014

KUTOKA OFISI YA MKUU WA MKOA MANYARA



FURUSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MKOA WA MANYARA
Mkoa una fursa nyingi za uwekezaji hususani katika huduma za Kiuchumi (Kilimo na Mifugo, Viwanda, Biashara, Utalii na Madini); Kijamii (Elimu, Afya na Maji); na Kiutamaduni (Michezo na Utamaduni).
FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA HUDUMA ZA KIUCHUMI KILIMO
Kuna maeneo makubwa yanayofaa kwa shughuli za kilimo cha kwaida na kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa. Mazao yanayozalishwa kwa wingi ni pamoja na Mahindi, Alizeti, Mbaazi, Mtama, Ngano, Maharage, Miwa, Vitunguu Maji, Vitunguu Saumu na Mpunga ambayo hutumika kama mazao ya Biashara na Chakula kwa wakazi wa Mkoa, Mikoa jirani na Nchi jirani za Kenya, Somalia, Ethiopia, Eritiria na Sudani. Hivyo wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika sekta hii. MIFUGO
Mkoa una zaidi ya mifugo milioni 2. Wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika sekta hii hususani katika uanzishaji wa ranchi na viwanda vikubwa na vidogo vya kusindika mazao ya mifugo ambayo ni nyama, maziwa na ngozi. Fursa nyingine ya kuwekeza katika sekta hii ni ujenzi wa majosho na mabwawa kwa ajili ya kuogesha na kunyweshea mifugo.

VIWANDA
Mkoa unawakaribisha wawekezaji ili waanzishe na kuwekeza katika viwanda Vikubwa, vya kati na Vidogo kwa ajili ya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na sekta nyingine. Kwa sasa Mkoa una Kiwanda kikubwa cha Mbolea cha Minjingu ambacho husambaza mbolea yake ndani na nje ya Mkoa na Kiwanda cha kusindika nyama kilichopo Wilayani Simanjiro. Kadhalika, Mkoa unakadiriwa kuwa na viwanda vidogovidogo 4560 vinavyofanya kazi za: Kusindika Nyama na Maziwa, mafuta ya Alizeti, Kusaga na kukoboa nafaka na Kutengeneza Mkaa usiotoa moshi wenye athari.

BIASHARA
Tayari makampuni kadhaa kama vile Kampuni ya Usafirishaji ya Mtei ‘express’, kampuni za Simu za Vodacom, Airtel, Zantel na Tigo na taasisi za fedha kama Benki ya Posta Tanzania, NMB, NBC, CRDB, EXIM nk. wanaendelea na shughuli mbalimbali za biashara ndani ya Mkoa. Hata hivyo bado kuna fursa nyingi za kuwekeza hususani katika uanzishaji wa maduka makubwa yenye bidhaa mbalimbali, hoteli za kitalii, vituo vya utamaduni, huduma za usafirishaji, mawasiliano na shughuli za kibenki. UTALII Mkoa una maeneo mazuri ya vivutio vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Ziwa Manyara ambako hupatikana aina mbalimbali za wanyamapori kama Simba, Chui, Chita, Twiga, Pundamilia, Swala, Nyati, Pofu, Ngiri, Mbuni, Korongo nk. Eneo jingine la utalii ni Yaeda Chini ambako upatikana jamii ya Wahadzabe ambao huishi kwa kutegemea uwindaji, matunda, mizizi na asali. Hivyo, Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuanzisha na kuwekeza katika hoteli na vituo vya utamaduni kwa ajili ya kutoa huduma muhimu kwa Watalii mbalimbali wanaotembelea Mkoa huu.

MISITU
Wawekezaji wanakaribishwa katika Mkoa kuwekeza katika shughuli za Ufugaji nyuki na uzalishaji Asali. Mkoa una eneo lenye ukubwa wa hekta 927,526 za hifadhi za Misitu zilizohifadhiwa kisheria ambamo shughuli za ufugaji nyuki na uzalishaji Asali zinaweza kufanyika. Tayari baadhi ya wananchi wanaendelea na shughuli hii katika misitu asili na binafsi iliyopo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa.

MADINI
Mkoa una utajiri mkubwa wa madini ya Tanzanite ambayo yanathamani kubwa na hayapatikani mahali popote duniani isipokuwa Mkoani Manyara Wilaya ya Simanjiro eneo la Mirerani. Madini mengine yanayopatikana Mkoani hapa ni pamoja na: Ruby, Green Garnet, Green Tourmaline na Rhodilite. Ukiacha madini ya Tanzanite, hakuna uwekezaji katika aina nyingine ya madini tajwa hapo juu hivyo Wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza katika Sekta ya Madini.

FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA HUDUMA ZA KIJAMII
Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Sekta za Elimu, Afya na Maji kwani huduma zinazoendelea kutolewa kupitia Sekta hizi bado hazitoshelezi na ni duni katika baadhi ya maeneo. Lengo kuu la Mkoa ni kuimarisha Sekta hizi ili kusaidia kuleta maendeleo ya haraka na kuondoa umaskini kwa Wananchi.

FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA HUDUMA ZA KITAMADUNI
Ili kudumisha tamaduni zilizopo, Mkoa kupitia Hospitali ya Rufaa ya Haydom iliyopo Wilayani Mbulu inajenga kituo cha Utamaduni (4corners) kitakachofanya utafiti wa mila na desturi za makabila 4 ya Mkoa wa Manyara ambayo ni Wahadzabe, Wanyaturu, Wairaqw na Wabarbaig. Vilevile, Mkoa unakituo cha Redio cha kijamii cha ORKENERI RADIO SERVICE 94.40RS FM kilichopo Wilayani Simanjiro kinachofanya kazi kubwa ya kutangaza utamaduni wa jamii ya Kimaasai. Hata hivyo Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuanzisha vituo vingine vya Utamaduni katika maeneo mbalimbali kama vile Yaeda Chini ili kuwavutia zaidi Watalii. Aidha, Mkoa unawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Michezo ya aina mbalimbali kwani kwa Miaka mingi sasa Mkoa umekuwa chimbuko la Wanariadha maarufu nchini Tanzania ambao walipeperusha Bendera ya Tanzania katika mashindano mbalimbali ndani na nje na kuuletea sifa Mkoa na Nchi. Miongoni mwawanariadha hao ni; Gidamis Shahanga, Joh Bura, John Stephen Akhwari, Zakayo Malekwa na Simon Robert Naali.

No comments:

Post a Comment