Wednesday, March 5, 2014

KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU



WADAU wanaoshughulika moja kwa moja na mchakato wa usajili wa kampuni hapa nchini wametakiwa kufanya kazi kwa karibu zaidi ili kuimarisha kiwango cha Tanzania kimataifa katika kujenga mazingira ya biashara.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa CEO Roundtable.

Alisema mamlaka hizo zinatakiwa kutekeleza mradi unaojulikana kama Tanzania Investment Window Project kabla ya Mei, mwaka huu ili faida za ubunifu wake ziweze kuunganishwa katika viwango vya mwaka kesho, vinavyohusiana na jinsi nchi zinavyoimarisha mazingira ya biashara.

Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na Mpango wa ONE UN, unalenga kuwezesha makampuni ya ndani na ya nje kujisajili kwa urahisi zaidi na kwa muda mfupi.

Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa msaada wa kiufundi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Biashara na Maendeleo (UNCTAD) kiko katika juhudi kuhakikisha kuwa taratibu za usajili wa kampuni unarahisishwa kupitia mtandao.

Mpango huo uliasisiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Oktoba, mwaka jana nchini China. Mpango huo utaruhusu wawekezaji kusajili kampuni, kupata vibali vya uwekezaji, vibali vya kazi na huduma nyingine kupitia njia ya mtandao.

Dkt. Turuka alitaja baadhi ya taasisi zinazotakiwa kufanya kazi kwa karibu kama Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Biashara, Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Jiji la Dar es Salaam na TIC.

"Mamlaka hizi ziteue wawakilishi wa ngazi za juu kabisa watakaofuatilia kwa haraka utekelezaji wa mradi huu," alisema, huku akipendekeza kikosi kazi hicho kukutana kila mwezi kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Alisema kuwa mradi huo unachukuliwa kwa umakini mkubwa na Waziri Mkuu Pinda ambaye ametaka kuelezwa kila wakati maendeleo yake hadi pale utakapotekelezwa.
Pia alitoa shukrani zake kwa wadau wote waliowezesha mradi kufikia hatua iliyofikiwa hadi sasa kwa kipindi cha mwaka uliopita hasa kuhusiana na taarifa zinazohusu taratibu za uwekezaji.

Alisema hadi sasa taratibu 30 ziko wazi na zinaweza kufikiwa kirahisi kupitia mtandao wa TIC katika lugha zaidi ya 70.

No comments:

Post a Comment