Monday, April 29, 2013

Chamwino walia njaa

KUTOKANA na ukosefu wa mvua ya kutosha katika Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wakazi wake kwa sasa wanakabiliwa na baa la njaa, hali inayosababisha baadhi yao kukimbia familia zao.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Laurent Hoya, wakati alipokuwa akifungua kikao cha baraza la madiwani.
Hoya alisema kuwa hali ya chakula katika maeneo mengi wilayani humo ni mbaya kiasi ambacho wakazi wengi wanahitaji kupata chakula cha msaada haraka iwezekanavyo.
Alisema kutokana na mvua kutonyesha kwa kiwango cha kutosha ndiyo sababu ya wananchi kukosa chakula kutokana na mazao mengi kukauka kwa jua.
“Hata wale tuliowahamasisha walime mtama ambao ndio kama zao mbadala linalostahimili ukame lakini hakuna walichoambulia,” alisema.
Alisema kuwa viongozi wa halmashauri hiyo kuanzia ngazi za vitongoji wanatakiwa kufanya jitihada za haraka katika kuangalia ni namna gani wanaweza kutoa msaada.
“Nawaombeni tutoke na kauli moja hapa, hali ya chakula katika halmashauri yetu ni mbaya sana, mimi nimefanya ziara katika maeneo mengi nimejionea hali ilivyo, inatisha, chakula hakuna kabisa,” alisema.
Naye Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Godfrey Mnyamale, alithibitisha kuwepo kwa uhaba mkubwa wa chakula, hali ambayo inatishia maisha ya wakazi katika maeneo mengi.
Mnyamale alisema kuwa kutokana na hali hiyo wabunge pamoja na viongozi mbalimbali wilayani hapo wamefanya ziara katika vijiji vyote 77 na kuwataka wananchi kutumia vizuri akiba ya chakula waliyo nayo.
Hata hivyo alitoa wito kwa wanachi wenye mifigo kuiuza ili waweze kununua chakula na kujiwekea akiba ya kutosha.

No comments:

Post a Comment