Friday, November 9, 2012

Serikali yakamilisha utafiti misimu ya kilimo

SERIKALI imesema tayari imeshafanya utafiti wa misimu ya kilimo nchini na kutambulika kwa kanda za kilimo kulingana na kiasi cha mvua zinazonyesha.
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alibainisha hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR).
Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua kama serikali haioni kuwa kuna haja ya kufanya utafiti wa misimu ya kilimo nchini, ili kupeleka mbolea ya ruzuku kwenye eneo husika katika muda muafaka.
Pia alitaka kujua ni kwa nini serikali isiwakopeshe wakulima mbolea hiyo, ili wawe nayo kwa wakati unaofaa kisha walipe baada ya kuuza mazao yao.
Akiendelea kujibu swali hilo, Malima alisema serikali imekuwa ikiratibu mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kwa kila wilaya ya mikoa kwa aina na kiasi.
“Baada ya kupokea mahitaji hayo serikali inawasiliana na makampuni ya pembejeo za kilimo, ili kuhakikisha uwepo wa pembejeo hizo katika maeneo yote hapa nchini kwa wakati kabla ya msimu huo kuanza,” alisema.
Alifafanua kuwa katika mwaka 2012/2013 mahitaji ya mbolea nchini yanakadiriwa kuwa tani 485,000.
Naibu waziri huyo alisema pamoja na mahitaji ya pembejeo kujulikana na kampuni, bado imekuwepo changamoto kwa baadhi ya mikoa kutofanya tathmini ya mahitaji halisi ya pembejeo katika maeneo yao na hivyo kuwahimiza kununua pembejeo mapema.
Aidha alisema changamoto hizo zimesababisha mawakala kukaa muda mrefu bila kuuza kutokana na wakulima kusubiri hadi mvua zinyeshe ndipo wanunue pembejeo.

No comments:

Post a Comment