Tuesday, February 25, 2014

WAKULIMA WA TUMBAKU KUNUFAIKA







WAKULIMA wa zao la tumbaku mkoani Tabora watanufaika na ongezeko la bei ya zao hilo huku pembejeo zake zikishuka bei kwa kiwango kikubwa.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Bodi ya muda ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Hassan Wakasuvi alipozungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kurejea kutoka nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu ya mguu.
Wakasuvi alisema kwa muda mfupi ambao Bodi hiyo imekuwepo madarakani imefanikiwa kufanya mambo mengi likiwemo kusimamia na kuhakikisha wakulima wananufaika na zao hilo kwa kuuza kwa bei yenye tija.

Alisema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013 mbolea aina ya NPK iliuzwa kwa dola 53.90 ambapo msimu wa mwaka 2013/2014 iliuzwa kwa dola 51.35 ikiwa na tofauti ya dola 2.55.
Aidha alisema kuwa mbolea aina ya CAN katika msimu wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 38.60 ambapo msimu wa2013/2014 iliuzwa kwa 33.30 ikiwa na tofauti ya dola 5.30.

Aliendelea kufafanua kuwa mbolea aina ya UREA katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 46.60 na msimu wa mwaka 2013/2014 kuuzwa kwa dola 34.85 sawa na tofauti ya dola 11.75.
Pia alisema Confidor ya pakiti katika msimu wa mwaka 2013/2014 iliuzwa kwa dola 4.46 ambapo katika msimu wa 2013/2014 iliuzwa kwa dola 2.88 ikiwa na tofauti ya dola 1.58.

Alisema dawa aina ya Yavikonyo katika msimu wa 2012/2013 iliuzwa kwa dola 28.94 na 2013/2014 ikiuzwa kwa dola 20.60 sawa na tofauti ya dola 8.34.

Wakasuvi alisema katika kipindi hicho cha bodi ya muda pia walifanikiwa kuokoa fedha kiasi cha dola za Marekani 236,088.72 sawa na Sh 4,632,844,632 kutokana na tofauti ya bei ya msimu wa kilimo katika mwaka 2012/2013 na 2013/2014.

WAKULIMA WA PAMBA WAMLALAMIKIA RC




CHAMA cha Wakulima wa Pamba nchini (TACOGA) kimemlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula Said Magalula, kwa kitendo chake cha kuagiza kukamatwa na kuwekwa ndani kwa wawekezaji watatu wa zao la pamba akiwatuhumu kushindwa kufunga mikataba na wakulima .
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa kwa waandishi wa habari juzi mjini Kahama mkoani Shinyanga na mwenyekiti wa TACOGA, Elias Zizi, kitendo cha hicho kinadaiwa kupingana na agizo lililotolewa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, alipoagiza wakulima wasilazimishwe kujiunga na mpango wa kilimo cha mkataba mpaka pale watakapokuwa wamepewa elimu ya kutosha.

Zizi aliwataja wawekezaji waliokamatwa na kuwekwa ndani kwa agizo la mkuu huyo wa mkoa kuwa ni pamoja na mwakilishi wa kampuni ya Fresho Investment, Kampuni ya ICK Cotton Co. Ltd na Kahama Oil Mill Ltd ambao wote wanafanya shughuli zao katika mkoa huo wa Geita.

Mwenyekiti huyo ameelezea kushangazwa kwake na hatua ya mkuu wa mkoa huo ambayo amedai ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa na Rais Kikwete na kwamba mpango wa kilimo cha mkataba pamoja na kuwa ni hiari hata hivyo baada ya majaribio yake kulijitokeza changamoto kadhaa katika utekelezaji wake.

Akifafanua, alisema baada ya kujitokeza kwa changamoto hizo wadau wote walikubaliana kusitishwa kwa muda utekelezwaji wa mpango huo mpaka pale changamoto zilizojitokeza zitakapopatiwa utatuzi ikiwemo suala la elimu duni juu ya mpango huo kutobainishwa vizuri kuhusu faida au hasara zake.
Kutooneshwa wazi kwa bei ya pamba atakayolipwa mkulima pale atakapokuwa anauza pamba yake licha ya kukopeshwa huduma zote muhimu ambazo bei zake zinafahamika pamoja na kilimo hicho kutokuwa na bima itakayomlinda mkulima iwapo patatokea janga lolote kama vile suala la ukame.
"Lakini changamoto nyingine ni suala la vikundi vya wakulima kutosajiliwa kisheria hali inayowanyima haki ya kudai na kudaiwa kisheria, uwekezaji mdogo wa mkopeshaji ukilinganisha na jasho la mkulima wa pamba analowekeza kwa eneo moja.
"Sisi TACOGA tunalaani kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Geita kwa hatua ya kutoa agizo la kukamatwa kwa wawekezaji hao katika zao la pamba ambapo wanatoa huduma katika mkoa wake, kitendo hicho kimelenga kuzishinikiza pande mbili pasipo hiari yao kuingia kwenye kilimo hicho cha mkataba."
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita, Magalula, pamoja na kukiri kutoa agizo la kukamatwa na kuwekwa ndani kwa wawekezaji hao alikanusha sababu zilizotolewa na viongozi wa TACOGA na kufafanua kuwa kosa lao ni lakuwauzia wakulima viuatilifu kwa fedha taslimu badala ya kuwapa kwa mkopo kama yalivyo maelekezo ya Bodi ya pamba (TCB).
"Nikweli nilitoa agizo wakamatwe, lakini hao TACOGA wanapotosha ukweli, sijawakamata kwa kutokuwa na vikundi vya kilimo cha mkataba, bali ni kutokana na kukiuka kwao utaratibu wa usambazaji dawa hizo za kuua wadudu ambapo mbali ya kuuza kwa fedha taslimu fedha hizo hawakuziwasilisha bodi ya pamba ambayo ndiyo iliyowapatia dawa hizo," alieleza Magalula.



MAHIZA AWAKUNA WAKULIMA WA KOROSHO



WAKULIMA wa zao la korosho mkoani Pwani wamefurahishwa na uamuzi wa Mkuu wa mkoa huo, Mwantumu Mahiza kutaka maofisa ushirika kuwajibishwa kwa kuwaondoa maofisa ushirika kutokana na utendaji mbovu na kushindwa kufuatilia madeni ya mikopo kwa vyama vya ushirika na fedha za wakulima wa zao la korosho. 

Mahiza alitoa agizo hilo kwenye kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) kilichofanyika hivi karibuni mjini Kibaha na kubainisha kuwa ni kipindi kirefu aliomba matokeo ya kulipwa kwa madeni ya mikopo hiyo na fedha za wakulima hao suala ambalo usimamizi wake umeonekana sio wa kuridhisha.
Mkuu huyo wa mkoa alitaka kuwajibishwa kwa watendaji hao kutokana na vyama vya ushirika wa mazao (AMCOS) vilivyofanya biashara kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani msimu wa 2011/2012 kwa kutumia fedha kwa kukusanya mazao ya wakulima ambazo zilipatikana kutokana na mikopo toka kwenye taasisi za kibenki za NMB na CRDB ambapo jumla ya sh. bil 12 zilikopwa.
Mmoja wa wakulima wa zao hilo la korosho wilayani Kibaha, Peter Malundi alisema watendaji hao hawana msaada wowote hali ambayo inasababisha shughuli za kilimo cha zao hilo kutokuwa na manufaa kutokana na fedha zao nyingi kutolipwa kwa walikopwa korosho zao muda mrefu.
Malundi alisema kuwa hata deni hilo kubwa ambalo lilikopwa benki hizo kwa udhamini wa mkoa lingeweza kulipwa endapo watendaji hao wangekuwa makini lakini kutokana na kutowajibika ipasavyo kumechangia hali hiyo. 

"Kauli ya Mahiza kusema kuwa kwasasa hawataki watendaji hao ambao hawana manufaa na mkoa huo hususan wakulima hivyo haina budi kupitia kikao hicho kutamka rasmi hawafukuzi bali hawataki mkoani hapo kwa maslahi ya mkoa ni kauli inayoonyesha uwajibikaji na iwe fundisho kwa watendaji wengine," alisema Malundi.
Alisema kuwa baadhi ya watendaji ndani ya mkoa huo wamekuwa hawawajibiki na kuona kuwa Mkoa wa Pwani ni sehemu ya kupumzika pasipo kufanya kazi jambo hilo si sahihi kwani na wananchi wa mkoa huo nao wanataka maendeleo kama ilivyo mikoa mingine.
"Kwa kuwa mkuu wa mkoa alisema kuwa mwanzo wa mkakati wake wa mwaka 2014 kutaka uwajibikaji kwa watendaji kwenda kwa wananchi na kusimamia kero zilizopo pasipo kukaa kusubiri kero mezani kutoka kwa wananchi ni mpango mzuri," alisema Malundi.
Awali hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia wizara ya kilimo na ushirika iliwataka viongozi na watendaji wa vyama vya msingi kulipa madeni yaliyotokana na uzembe wao sambamba na kuwaondoa viongozi hao na kuteua bodi mpya.



WAJASIRIAMALI WAPATA MAFUNZO USINDIKAJI MUHOGO

WAJASIRIAMALI 16 kutoka Mikoa ya Mwanza, Pwani na Kagera wamepata elimu ya usindikaji wa zao la muhogo na viwango vinavyozingatia ubora unaokubalika katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA C).


Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, wilayani Misungwi baada ya mafunzo hayo, mshauri wa usindikaji na masoko wa IITA Dkt. Gabriel Nduguru, alisema wakulima wasindikaji wa zao la muhogo, hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu viwango na ubora wa bidhaa zao.
Alisema kuwa mafunzo hayo kwa wasindikaji hao, yalitolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango nchini (TBS ).
Alisema IITA ilifanya utafiti na kubaini changamoto hiyo kwa wasindikaji wengi wa zao la muhogo, hivyo ikaamua kutoa elimu inayohusu ubora na viwango kwa wasindikaji hao ili kuwawezesha kupata masoko ya uhakika.


"Wakulima na wasindikaji hao hawakuwa na elimu, hivyo bidhaa zao hazikuwa bora na salama na zilitishia afya za walaji.Baada ya kubaini hilo tukaona tuwafundishe jinsi ya kusindika muhogo salama kwa kuzingatia viwango vya ubora kulingana na mahitaji ya walaji," alisema Dkt. Ndunguru.
Alisema wanafanya utafiti wa mazao na kusaidia kuainisha viwango vinavyotumika kwa nchi za EAC, baada ya kuridhiwa na mawaziri wa nchi za Jumuiya hiyo.
Alisema wananchi watafahamu viwango vya ubora baada ya kuwapa mafunzo ya usindikaji na watazalisha chakula chenye ubora na kuuza katika masoko ya uhakika na watajiongezea kipato .
Dkt. Ndunguru alisema changamoto kubwa kwa wasindikaji zao la muhogo, ni vifungashio na mitambo ya kisasa kwani ni kiwanda kimoja tu ambacho hakitoshelezi mahitaji.
 

Monday, February 24, 2014

MWAKA WA KILIMO WA AFRIKA WAZINDULIWA MKOANI IRINGA

Mkuu wa mkoa wa Iringa Mh.Dkt Christine Ishengoma akipiga makofi mara baada ya kukata utepe
kuashiria uzinduzi wa ghala la mazao,katika kijiji cha kaning'ombe, wilayani iringa mkoni humo wakati wa uzinduzi wa mwaka wa kilimo



Sehemu ya wadau mbalimbali walio shiriki katika uzinduzi wa mwaka wa kilimo mkoani humo



Mwakilishi wa shirika la afrika one kutoka afrika kusini, Mercy Erhiawarien akitoa ufafanuzi mbele ya wadau wa kilimo kuhusiana ana namna kilimo kinavyoweza kuwasaidia watanzania, hasa kwa vijana na akina mama




 Pichani juu na chini ni mabalozi wa kilimo nchini, msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Prof Jay pamoja na mchora katuni maarufu nchini, Massoud kipanya wakizungumza mbele ya wadau wa kilimo namna kilimo kinavyoweza kuwakomboa vijana 


Baadhi ya wadau viongozi wakifanya ukaguzi wa shamba la mfano katika kijiji cha kaning'ombe mkoani Iringa.




Wasanii ambao ni mabalozi wa kilimo nchini, Mrisho mpoto na Profesa Jay amabao ni mabalozi wa kampeni ya ''KILIMO KINALIPA,JIKITE'' walikuwepo

 
Sehemu ya shamba la mfano la mkulima mdogo, Mzee Mbagile