Friday, May 17, 2013

Wakulima wanusurika kifo

WAKULIMA wawili wilayani Kiteto, wamenusurika kuuawa na wafugaji jamii ya Kimasai baada ya kuibuka mapigano kufuatia ng’ombe kula mazao shambani.
Wakulima hao walionusurika kuuawa ni Samweli Malima (35) na Sanagali Athumani (29), wote wakazi wa Njutaa.
Akizungumza na Mwakilishi wa Blog Yetu jana hospitalini walipolazwa majeruhi, baba mzazi wa majeruhi hao, Waziri Mtambo (55) alisema tukio hilo lilitokea Mei 15, majira ya saa 7 mchana wakati vijana hao wakiwa shambani wakivuna mahindi.
Alisema vijana hao walipofika shambani waliwakuta ng’ombe wanakula mazao ndipo walipowauliza vijana wachungaji waliokuwa wakichunga ng’ombe hao na ndipo ukatokea ubishani.
Mtambo alisema baada ya muda mfupi walitokea Wamasai sita kwenye kibanda cha shambani ambacho Malima na Athumani kipindi hicho walikuwa wamepumzika na kuomba na wao kupumzika wakidai wamechoka baada ya kutembea umbali mrefu wakichunga ng’ombe ambao hawakuwa nao.
“Baada ya muda wakaongezeka tena Wamasai wengine na kuanza kuwachoma choma na sime ubavuni huku wakihoji kwanini wanazuia ng’ombe wasile chakula,” aliongeza.Alisema kutokana na hali hiyo, vijana hao walianza kujitetea, lakini walizidiwa nguvu na Athumani alizimia ndipo walipokimbia.
Mtambo alisema vijana hao waliokolewa na wapita njia ambao walitoa taarifa kijijini na wananchi kwenda mashambani ambako waliwakuta wametapakaa damu huku wakiwa wamepoteza baadhi ya viungo vya mwili.
“Athumani ambaye hali yake ni mbaya amechanwa na sime kichwani na kupasua mfupa wa fuvu, ametobolewa kwapani na sime, paji la uso kushoto karibu na jicho, amechunwa ngozi hadi usawa wa sikio na sime na Samweli Malima amekatwa dole gumba la mkono wa kulia, amejeruhiwa kichwani kwa sime na sehemu mbalimbali mwilini,” alifafanua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba tayari askari wameagizwa kwenda kudhibiti hali katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment