BODI ya Pamba nchini (TCB) Kanda ya Ziwa imetoa ufafanuzi kuhusiana na
malalamiko ya wakulima wa zao la pamba wanaolalamikia kugoma kuota kwa mbegu za
pamba zilizosambazwa na Kampuni ya Quton huku wengi wakidai kulipwa fidia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wiki iliyopita, Kaimu meneja
wa bodi ya Pamba, Buluma Kalidushi baada ya kuwepo kwa malalamiko hayo, bodi
yake iliunda timu ya kufuatilia ili kuweza kubaini ukweli wake lakini hata
hivyo wizara kwa upande wake pia iliunda tume ya wataalamu ili kuchunguza
malalamiko hayo.
Kalidushi alisema kwa taarifa alizonazo tayari tume ya wizara imekamilisha kazi
yake na kinachosubiriwa hivi sasa ni kutolewa kwa taarifa hiyo ili kuweza
kubaini sababu zilizosababisha mbegu hizo zisiote katika baadhi ya maeneo huku
maeneo mengine zikionesha matokeo mazuri.
Alisema baada ya kutolewa kwa taarifa ya wataalamu hao kutoka wizarani ndipo
itakapofahamika iwapo kuna umuhimu wa kulipwa fidia kwa wakulima waliopanda
mbegu hizo na zikagoma kuota au kutolewa maelekezo mengine tofauti na suala la
madai ya kutaka kulipwa kwa fidia.
"Ni kweli mbegu za Quton katika baadhi ya maeneo zimegoma kuota na
zimesababisha malalamiko mengi kutoka kwa wakulima, bodi tuliunda timu ya
kufuatilia ili kuweza kubaini tatizo, lakini pia wizara iliunda tume na tayari
imekamilisha kazi yake, tunasubiri kutolewa kwa taarifa.
"Hata hivyo, ukweli ni kwamba tatizo la mbegu kutokuota limetokea kwa
mbegu hizi za Quton, ni tatizo la kila mwaka hata kabla ya kuwepo kwa mbegu
hizo, malalamiko yamekuwa mengi kwa vile mbegu hizo zina mwenyewe (Quton ),
zamani mbegu zilikuwa za wakulima wenyewe hawakupiga kelele sana zilipogoma
kuota," alieleza Kalidushi.
Alisema tatizo la mbegu kugoma kuota mara nyingi linachangiwa na wakulima
wenyewe kuchafua kwa makusudi pamba yao pale wanapokwenda kuiuza kwa lengo la
kutaka kuongeza uzito ambapo wengi wana tabia ya kuweka maji na magadi na hivyo
kusababisha mbegu kuoza.
Alisema tabia ya kuweka maji kwa lengo la kutaka kuongeza uzito wa pamba pale
inapopimwa inafaida kidogo sana ikilinganishwa na hasara anayoipata mkulima
pale anaporejeshewa mbegu zinazotokana na pamba yake aliyoiuza huku akiwa
ameiwekea maji na hivyo kujikuta mwenyewe akipata hasara kwa mbegu hizo
kutokuota.
Kwa upande mwingine kaimu meneja huyo alikanusha madai ya kukiukwa kwa taratibu
za manunuzi kwa mujibu wa sheria katika kutoa zabuni ya usambazaji wa mbegu za
pamba kwa kampuni ya Quton ambapo alisema taratibu zote zilizingatiwa na
kampuni hiyo ndiyo iliyoshinda zabuni baada ya kukidhi vigezo vilivyotakiwa.