Saturday, June 1, 2013

Tanzania kuongeza uzalisha wa kahawa ifikapo 2016

Morogoro. Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza amesema kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha tani 80,000 za kahawa ifikapo mwaka 2016 nia ikiwa ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kukidhi masoko ya ndani na nje ya nchi.
Chiza pia alisema kuwa Tanzania imekuwa ikizalisha wastani wa tani 35,000 na 50,000 za aina mbalimbali za kahawa kwa mwaka ikiwa ni pamoja na aina ya Arabica, Robusta zenye soko kubwa katika soko la dunia.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kahawa unaofanyika mjini Morogoro, Waziri Chiza alisema wizara yake imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha zao hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza mikoa minane ya ulimaji wa zao hilo ambayo ni pamoja na Morogoro, Iringa, Njombe, Katavi, Geita na Manyara huku Serikali ikiendelea kujenga mazingira mazuri zaidi ya kilimo cha zao hilo.
Alisema hakuna sababu ya kilimo cha zao hilo kushuka, kwa kuwa zao hilo lina bei nzuri katika soko la dunia, akiwataka Watanzania kuzalisha kwa wingi hata pale bei ya zao hilo inaposhuka katika soko la dunia kwa kuwa imekuwa na mtindo wa kupanda na kushuka mara kwa mara.
“Zao la kahawa ni muhimu sana na ni lazima kuwapo na utaratibu wa kuwa na bei moja yenye manufaa kwa mkulima na nchi yetu kwani mkulima amekuwa na mahitaji makubwa ya kimaisha na anatakiwa kukuza uchumi wake,” alisema waziri huyo.
Waziri Chiiza alisema, umefika wakati wa kuanza kutafuta masoko mapya ndani na nje ya nchi badala ya kung’ang’ania soko moja na kujikita katika kulalamika na kuongeza kuwa ili kuweza kufanikiwa katika kutafuta masoko hayo, ni lazima balozi zitumike kusaidia ili wakulima waweze kunufaika.
Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na bodi ya kahawa kusaidia kupitia ruzuku kila mwaka na kuzitaka halmashauri kutenga maeneo ya kilimo cha kahawa na kuweka bustani za miche ya zao hilo ili wakulima waweze kupata miche hiyo kwa bei nafuu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mkutano huo, Seleman Chambo mapema akimkaribisha Waziri Chiza alisema kuwa, uzalishaji wa zao la kahawa nchini umeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya mashamba ya kahawa kulimwa mazao mengine huko mkoani Kilimanjaro wakati baadhi ya wadau wa kahawa nchini wakilalamikia kutofuatwa kwa bei elekezi ya kahawa.

No comments:

Post a Comment