Wednesday, January 29, 2014

Kenya yapiga jeki kilimo



 Kenya imezindua mradi mwengine tena ambao ikiwa utafanikiwa utapiga jeki na kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo nchini humo.

Mradi huo 'Galana Kulalu' katika mkoa wa pwani unanuiwa kuziweka katika mpango wa unyunyiziaji maji ekari zaidi ya millioni moja za kilimo hasa cha mahindi na miwa.
Mradi huu unakadiriwa kwamba katika kipindi cha miaka 5 ijayo utagharimu zaidi ya shilingi billioni 250 za Kenya.
Tangu kale maeneo ya bara ya Kenya ndio yamejulikana kuwa na kilimo kinacholisha nchi kutokana na hali nzuri ya hewa na kupata mvua ya kutosha , lakini mpango huu wa Galana Kalula unasemekana utaifanya Kenya kuwa na uwezo wa kujitosheleza kwa chakula na hata kuweka kukiuza nje.
Kila ekari kwa mfano itatarajiwa kuzalisha kati ya magunia 40 na hamsini kutokana na rutuba ya ardhi hiyo na kunyunyiziwa maji kwa kipimo kinachohitajika.
Eneo hilo liko katika majimbo ya Kilifi na Tana river ambayo kwa miaka mingi yamekumbwa na umaskini na yameachwa nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na ardhi nzuri ya kilimo.
Hii ilitokana na sera mbovu, ukosefu wa usalama na hivi majuzi kukumbwa na vita kati ya wakulima na wafugaji vilivyochochewa zaidi kisiasa.
Hadi sasa bado kuna hofu miongoni mwa wenyeji kwamba licha ya kuahidi mengi mazuri , huenda wasitendewe haki. Hata hivyo wadadisi wanasema iwapo mradi huo , utatekelezwa kwa haki na uwazi ni fursa nzuri ya kutatua matatizo yanayoilemea kaunti hiyo.

No comments:

Post a Comment