Thursday, May 23, 2013

Bajeti ya kilimo mwaka huu yawaacha wadau njiapanda

Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inapita kwa mbinde katika kikao cha Bunge la bajeti 2013 mjini Dodoma hivi karibuni.
Taarifa zinabainisha kwamba haikuwa rahisi kupita kwa bajeti hiyo kutokana na sababu nyingi, lakini kubwa ni mfumo wa stakabadhi ghalani na utaratibu wa ruzuku ya pembejeo, ushirika na sintofahamu iliyopo kwa wakulima wa pamba, miwa na tumbaku.
Mazao hayo ingawa ni roho ya uchumi wa mataifa mengi ulimwenguni, nchini wakulima wake wapo njia panda na mbaya zaidi hata fedha zizozotengwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kilimo hazieleweki zinaenda wapi na zinafanya nini?
Hata hivyo bajeti ya serikali 2012/2013 haijaonyesha kutoa nafuu yoyote kwa wenye viwanda vidogo na wakulima na hali hiyo kuwaweka njiapanda watendaji katika sekta hizo kwani kilichotokea katika bajeti iliyopita haikuakisi nuru kwa bajeti ijayo.
Kulingana na Waziri wa Fedha na Uchumi, William Mgimwa, Sh17.7 trilioni, zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2012/2013 na bajeti  ya sasa inatenga fedha za matumizi makubwa katika mafungu matano.
Mafungu hayo ni pamoja na kulipa deni la Taifa ambalo limetengewa Sh2.7 trilioni wakati Wizara ya Ujenzi Sh1 trilioni, ulinzi Sh920 bilioni, elimu Sh721  Bilioni na nishati na madini Sh641 bilioni. Jumla ya fedha zote ambazo zitatumika kama mafungu ya juu ni Sh5.982 Trilioni.
Serikali katika bajeti ijayo katika kile ilichoelezwa kuwa ni kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na tija na ukosefu wa ajira,  imetenga fedha katika maeneo tofauti kwa ajili ya la kuhuisha sekta ya kilimo.
Kulingana na bajeti ya sasa, Sh30 bilioni zimetengwa kwa ajili ya Benki ya Rasilimali (TIB) Sh40 bilioni kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, fedha ambazo zinaifanya benki hiyo mpya kuwa na mtaji wa Sh100 bilioni.
Waziri Mgimwa anasema bajeti imelenga kuboresha mazingira ya biashara na kutenga maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini.
Anasema lengo lingine ni kukuza ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na hatua hiyo inaenda sanjari na kuboresha viwanda vidogo vidogo nchini na kwamba  Sh128.4 bilioni, zimetengwa katika eneo hilo.
Bajeti ya serikali katika sekta ya kilimo inatajwa Sh328.1 bilioni kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, na Sh130.5 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo  na Sh5.7 kwa ajili ya ushirika ambao unalalamikiwa kuwa ni kama umekufa.

No comments:

Post a Comment