Moja ya matatizo makubwa ya uzalishaji wa zao la korosho ni ugonjwa wa Ubwiri unga.Ugonjwa huu unasababishwa na vimelea aina ya uyoga (fungus) viitwavyo Oidium anacardii. Ugonjwa huu ni muhimu sana, kiasi kwamba kama haukuthibitiwa, unaweza kupunguza mavuno kwa zaidi ya asilimia 70. Ugonjwa huu umeenea katika mikoa yote inayolima zao hili Tanzania. Hapo awali ugonjwa huu ulikuwa unaitwa kwa jina la“ukungu” kutokana na uhusiano wake mkubwa na haliya hewa ya ukungu (litabwe kwa Kimakonde) unaoonekana alfajiri/asubuhi katika miezi ya Juni - Septemba. Hivyo basi, jina la Ubwiri unga linatumika sasa ili kuwawezesha wakulima wasichanganye vitu hivyo viwili.
MASHAMBULIZI
Ugonjwa huu unashambulia maeneo yote machanga na teketeke katika mti wa mkorosho, hasa machipukizi, majani, maua, mabibo na korosho changa (tegu). Athari kubwa ya ugonjwa huu inatokana na mashambulizi ya maua, ambayo hushindwa kufunguka na kuwezesha chavua kufanya kazi yake, hatimaye hunyauka na kukauka.
DALILI
Maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu, hufunikwa na unga unga mweupe au wakijivujivu ambao huonekana kama vumbi vumbi. Vimelea au chembe chembe zinazoshambulia ni ndogo ndogo sana na hazionekani dhahiri kwa macho, ila kwa darubini. Chembe chembe hizi zinapozaliana kwa wingi katika maeneo ya mshambulizi, ndipo huonekana kama unga unga mweupe/kijivu.
KWENYE MAJANI
Pamoja na kufunikwa na unga unga, majani yaliyoshambuliwa husinyaa, hubadilika rangi, wakati mwingine hukunjamana. Majani machanga zaidi yanaweza kupukutika, ambapo yale yaliyokomaa hayashambuliwi. Masalia ya mashambulizi kwenye majani yaliyokomaa, huonekana kama mabaka ya kahawia, hata hivyo hayapukutiki.
KWENYE MAUA
Maua yanaweza kushambuliwa hata kabla ya kuchanua. Pamoja na kufunikwa na unga unga weupe/kijivu, maua yaliyoshambuliwa sana hushindwa kuchanua na hatimaye hukauka kabisa na kuwa kama “majani yachai”. Hili ndilo sababisho kubwa la upungufu wa zao la korosho.
KWENYE MABIBO
Mabibo yaliyoshambuliwa huonyesha unyafuzi,hupasuka pasuka na ngozi yake huonekana kuwa chafu. Hatimaye, mabibo hayo huwa madogo kwa umbo, yenye maji kidogo sana, hivyo kuyafanya maji yake kuwa matamu sana.
KWENYE TEGU NA KOROSHO
Tegu zilizoshambuliwa huweza kubadilika rangi yake ya kijani/nyekundu na kuwa ya hudhurungi au bluu iliyo mzito. Tegu zikishambuliwa zingali changa sana, huweza kupukutika. Tegu zilizoshambuliwa zikifikia kukomaa, zinaonyesha uharibifu mkubwa wa ngozi yake na huonekana chafu, hatimaye, wakati wa mauzo hutengwa katika daraja lachini (grade II).
KUSTAWI KWA UBWIRI UNGA
Vimelea vya Ubwiri unga vinaishi kwenye mimea iliyo hai tu, haijawahi kuoteshwa katika maabara. Ugonjwa huu hushamiri na kustawi vizuri katika majira yenye ukungu, hasa kuanzia mwezi Mei/Juni hadi Septemba karibu kila mwaka. Mazingira mwafaka kwa ugonjwa huu ni:
• Joto: 26 - 28 0C (bora 25 C)
• Unyevu (RH): 80-100% (bora 95%)
Ubwiri unga pia hupendelea zaidi mikorosho iliyosongamana na isiyopitisha hewa vizuri. Ugonjwa huu hupendelea mazingira ya kiangazi, hasa kuanzia mwezi Juni hadi Septemba, haupendelei hali ya mvua na joto jingi. Hivyo basi, katika miezi mingine (hasa wakati wa masika), vimelea hujificha na kuishi Kwenye maotea au machipukizi uvunguni mwa mikorosho au kwenye maua yasiyo ya msimu. Hivi ndivyo vyanzo vya Ubwiri unga, vyenye uwezo wa kuhifadhi ugonjwa msimu hadi mwingine. Ugonjwa huu husambazwa kwa upepo ambao nao pia hushamiri sana katika miezi ya Mei/Juni hadi Septemba.
KUDHIBITI
Zipo njia aina tatu zinazotumika kuthibiti Ubwiri unga, nazo ni mbinu za asili, mbegu bora na madawa.
MBINU ZA ASILI (Cultural control)
Kuondoa vyanzo vya Ubwiri unga (sanitation).
Hii ni kazi ya mikono ya kuondoa machipukizi na maotea yanayojificha kwenye uvungu wa mikorosho, kutumia vifaa kama vile upanga, mundu, shoka nk. Msingi wa kazi hii ni kupunguza kasi ya ugonjwa huu katika shamba kwa kuchelewesha mlipuko na kasi ya mashambulizi.
Kubadili mazingira ya ugonjwa katika miti.
Kupunguzia matawi (prunning) ya mikorosho ili kufanya umbile la mwamvuli katika miti, ili kuruhusu joto na upepo kupenya kirahisi, inasaidia sana kuthibiti Ubwiri unga.
Kupunguza miti (thinning) iliyosongamana na kuacha nafasi ya kutosha kati ya miti, itasaidia kupunguza kuenea kwa ugonjwa. Miti ikiwa katikanafasi ya kutosha, itawezesha hewa kupenya vizuri na kubadili mazingira ili yasiwe mazuri kwa kustawi kwa ugonjwa.
Kupanda mikorosho inayovumilia/kuhimili ugonjwa.
Ipo baadhi ya mikorosho ambayo inaweza kuhimili mashambulizi ya ugonjwa hata kuweza kutoa Mazao bila ya kutumia kinga yoyote. Aina zingine zinaweza kutoa maua na kuzaa kabla ya athari za ugonjwa hata kuweza kukwepa mashambulizi. Hii ni baadhi ya mikorosho bora ambayo hatimaye imepandwa katika eneo moja katika vituo vyetu vyote vya kuendeleza korosho (Cashewnut Development Centre )kama NALIENDELE. Mbegu zinazopatikana toka mashamba hayo ni mbegu bora (polyclonal seed) ambazo zinaweza kuzaa bila madawa, lakini huzaa vizuri zaidi kama mtu atatumia dawa pia.
MATUMIZI YA MADAWA
Dawa ya Salfa (Sulphur)
Salfa ndiyo dawa inayotumika kwa wingi zaidi kukinga ugonjwa wa Ubwiri unga. Dawa hii ambayo ni ya unga, inapulizwa kwa kutumia mashine maalumu (motorised blower) ya kupulizia dawa k.m. Maruyamana Solo. Kiwango cha gramu 250 kwa mti, kwa mzunguko, ndicho kinapendekezwa. Hivyo basi kwa mizunguko mitano kiasi cha kilo 1.25 cha salfa kwa mti kwa mwaka kinahitajika. Pia kuna salfa za maji kama Thiovit ambazo unaweza kupulizia kwa kutumia vinyunyuzia dawa vya kawaida (knapsack sprayer)
Wakati wa kuanza kupulizia sailfa
Mpulizo wa kwanza unaanza ambapo karibu asilimia 20za maua yamejitokeza na wakati sawa, zaidi ya asilimia 5 ya maua hayo tayari yawe yanaonyesha dalili za ugonjwa. Upimaji wa maua ili kujua lini upuliziaji uanze, inasaidia kufanya matumizi sahihi ya dawa, hatimaye faida/pato litakuwa kubwa kwa mkulima.
Inashauriwa kwamba upuliziaji ufanyike asubuhi na mapema, wakati ambapo kuna umande. Asubuhi, upepo nao huwa hauna nguvu sana na inashauriwa upuliziajiusizidi ya saa 3 asubuhi. Umande unasaidia salfa ya unga iweze kunata kwenye majani na maua. Ila kwa salfa ya maji kama thiovit unaweza kupulizia wakati wowote.vipindi vifuatavyo, vimependekezwa katika upuliziaji:Siku 14 14 14 21 21
Dawa zingine badala ya salfa.
Madawa kadha wa kadha yamefanyiwa utafiti sambamba na salfa. Aina tatu za dawa hizo (waterbased organics), zimependekezwa kwa matumizi ya wakulima, nazo ni Bayfidan, Anvil na Topas. Kiwango cha upuliziaji ni ml 10 - 15 za dawa ndani ya0.75 - 1.25 za maji kutegemeana na ukubwa wa mti. Vipindi kati ya mipulizo ni wiki tatu (siku 21) na awamu (raundi) 3 zinatosha kwa msimu. Inashauriwa kwamba kutokana na gharama za dawa yamaji, zinafaa zitumike kwenye mikorosho ambayomkulima ana uhakika wa kutoa zaidi ya kilo 4 baada ya kupulizia. Miti inayotoa chini ya kiasi hicho heri isipuliziwe, vinginevyo italeta hasara
No comments:
Post a Comment