Friday, April 10, 2015

HANANG watakiwa kupanga matumizi bora ya ardhi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Dkt. MARY NAGU
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Dkt. MARY NAGU, amevitaka vijiji vyote wilayani HANANG mkoani MANYARA, kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro miongoni mwa makundi mbalimbali katika jamii

Dkt. NAGU ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika vijiji vipya vilivyosajiliwa mwaka jana na kuwataka wananchi kushirikiana na viongozi wao kudumisha amani miongoni mwao.

Waziri NAGU amewaeleza wananchi hao kuwa uamuzi wa serikali wa kuanzisha vijiji vingi zaidi umelenga kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.

Hata hivyo ameonya kuwa bila kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji ili kuyapanga makundi mbalimbali yaweze kuishi kwa usalama, upendo na mshikamano, maendeleo ya haraka yaliyokusudiwa hayawezi kufikiwa kwa wakati.

Viongozi wa vijiji hivyo kwa upande wao, wameiomba serikali na Mbunge huyo wa Jimbo la HANANG, kuwasaidia kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao ikiwemo maji, elimu na baadhi ya barabara za vijiji.

Katika ziara hiyo pia ambayo mpaka sasa imehusisha vijiji vipya 30, DOKTA NAGU amewahimiza wananchi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, kujiunga katika mfuko wa afya ya jamii-CHF ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya wilayani humo pamoja na kuipigia kura katiba inayopendekezwa wakati utakapofika.

No comments:

Post a Comment