Sunday, March 8, 2015

FAIDA YA MBOGA MBOGA KWA AFYA


Mboga ni moja ya vyakula vilivyo muhimu sana kwa uhai wa afya ya binadamu. Mara nyingi mboga hutumiwa kama kitoweo, aina nyingi za mboga huwa na wingi wa Vitamini C, Carotene, ambayo hatimaye hubadilishwa kuwa Vitamin A, Calcium, chuma pamoja na madini mengine.
Mboga ni jina litumikalo kwa aina nyingi za mimea itumiwayo na binadamu kama chakula au kutowelea chakula kingine. Mboga hizo huwekwa katika makundi matano, yaani:


1. Matunda (nyanya, bilinganya, bamia, matango, pilipili na maharage).
2. Majani (kabeji, letusi, seleri, mchicha na mlenda)
3. Mizizi (karoti, radishi na tanipu)
4. Mashina (vitunguu maji, vitunguu saumu na iliki)
5. Maua (koliflawa na brokoli)


Pengine utajiuliza kwa nini usumbuke kulima mboga zako mwenyewe? Zifuatazo ndizo sababu kubwa za kufanya hivyo:

1. Kupata na kutumia mboga zikiwa katika hali ya upya(hazijaanza kuharibika)
2. Ni rahisi, yaani gharama ya kuzistawisha ni ndogo ukilinganisha na bei ya kuzinunua. Isitoshe aina nyingine za mboga huwa na faida mbili, kwa mfano: kunde, maharage na maboga, hutumiwa tunda na majani yake.
3. Raha ya kufanikiwa; tabia ya binadamu ni kufurahia matunda mazuri ya jasho lake, kwani binadamu hupata uradhi kwa kufanya kazi yake mwenyewe na kufanikiwa.

Baada ya mkulima kuamua kustawisha mboga katika bustani yake mwenyewe, yabidi pia ajiweke katika hali ya kupata mavuno mengi iwezekanavyo. Jambo hili linaweza kutimizwa kwa kuzingatia yafuatayo:
a) Kujua aina ya mboga ziwezazo kustawi vizuri kwa kulingana na mazingira yaliyopo, hasa hali ya hewa na udongo.
b) Kujua muda zichukuao hadi kukomaa kusudi mpango wa kufuatisha nyingine ufanywe mapema.
c) Kufahamu aina na kiasi cha mbolea zinazohitajika kutumiwa, na kufanya mipango ya kuipata wakati inapotakiwa.
d) Kufahamu magonjwa na wadudu washambuliao mboga katika eneo lake(mkulima) analo ishi, na kujua jinsi ya kupambana nao.


Ulimaji wa mboga unaweza ukawekwa katika makundi mawili; bustani ndogo ndogo karibu na makazi yetu, na mashamba makubwa kwa ajili ya biashara. 
Leo nakomea hapa.

No comments:

Post a Comment