Mgogoro baina ya mwekezaji na Jamii ya wafugaji wapata ufumbuzi
Mkuu wa wilaya ya BABATI mkoani MANYARA, KHALID MANDIA, ametegua kitendawili cha muda mrefu juu ya mgogoro baina ya mwekezaji wa Kifaransa na Jamii ya wafugaji wa kabila la KIBARBAIG, katika kijiji cha VILIMA VITATU wilayani humo na kuwaruhusu waendelee na shughuli zao za ufugaji kwenye eneo ambalo mwekezaji huyo amelihodhi kinyume cha sheria.
MANDIA ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na mwekezaji huyo anayemiliki hoteli ya kitalii ya UN LODGE, pamoja na wafugaji walioweka kambi porini kwa zaidi ya siku nne wakitaka kupatiwa majibu na serikali kuhusu utata wa umiliki wa eneo la mwekezaji huyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya BABATI, DOMINIC KWEKA amefafanua kuwa Halmashauri ya wilaya yake imepima eneo halali la ekari 45 la mwekezaji huyo na kuweka alama ili kuondoa utata huo.
Mkuu wa wilaya ya BABATI, KHALID MANDIA akiwa na kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, amewataka wafugaji hao kusimamia amani na utulivu katika eneo hilo na kuzionya pande hizo mbili kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Baada ya kumalizika kwa mkutano wa ndani kati ya kamati ya ulinzi na usalama na mwekezaji huyo kuhusu suala hilo, msemaji wa kampuni hiyo ya UN LODGE, LEONARD WEREMA amekataa kuzungumzia yaliyojiri katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment