Sunday, March 8, 2015

UTI WA MGONGO WA TAIFA UMEKUFA

 Habari ndugu zangu watanzania, ni matumaini hamjambo nyote. Poleni na shughuli za ujenzi wa Taifa, wakulima wanahangaika kuandaa mashamba maana maeneo mengi ya nchi mvua zimeanza kunyesha sasa, poleni sana na nawaomba muongeze nguvu zenu mashambani. Ndugu zangu, leo hebu tujaribu kuangalia hili la kwamba walau kila mtanzania ama anajua, amesikia au kuambiwakuwa Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa. Wakubwa, wenye mamlaka wamekuwa wakituimbia kila leo huo wimbo, ni wimbo mzuri sana, lakini je wanaouimba na kuutangaza unatoka mioyoni mwao na kweli uko akilini mwao hasa? Hebu kila mmoja wetu ajiulize mara mbili mbili wakati tunaenda kulijadili hili.

  Kwanza kabisa nakubaliana na hoja hiyo ya kwamba Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa letu (Tanzania). Na naelewa na kuamini kwamba mlinzi hasa wa uhai wa uti wa mgongo huu si mwingine bali Mkulima, tena si mkulima tu, Mkulima mdogo mdogo wa huku vijijini. Ndugu zangu ili tuite Kilimoni uti wa mgongo kuna vitu na mambo mengi ya kufanya kwenye hilo na si kusema tu kwa maneno.
  Mkulima anakabiliwa na changamoto nyingi sana kwenye Kilimo chake. Ili mkulima apate tija katika kilimo chake kuna vitu vinavyohitajika shambani, yaani mbolea, mbegu na madawa (Pembejeo). mkulimanamfugaji1@gmail.comPembejeo zinahitaji pesa. Mkulima anahangaika huku na kule kudunduliza kupata mbolea, changamoto nyingi anazipata wakati akihangaika kupata pembejeo ni pamoja na kupata pembejeo feki ama zimechakachuliwa au zimekwisha muda wa kutumika. Huyu mkulima anapovuna mazao yake, je soko la uhakika la mkulima huyu liko wapi? ni dhahiri shairi halipo, anahangaika tena kutafuta soko, sokoni ananyanyaswa, anapangiwa bei ya mazao yake na wafanyabiashara, hana haki tena katika mazao yake. Mfanyabiashara huyu anayempangia mkulima bei ya mazao yake, amemsaidia nini katika kuzalisha mazao yake? hakipo alichomsadia. Kwa nini basi serikali isidhibiti, kuratibu na kusimamia utaratibu wote wa masoko ili kulinda maslahi ya mkulima na mazao yake.
  Katika hilo la wajibu wa serikali, ni mipango mingi ya kumhusu mkulima anayoibuliwa, lakini utekelezaji wake ni hafifu kiasi flani. Ni kweli kwamba kuna tatizo la rasilimali Pesa katika nchi yetu maskini yenye rasilimali kibao, lakini kama kweli tunaimba huu wimbo wa kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa ni lazima tuhakikishe kwamba pesa inayohitajika kwenye kilimo itoke katika pesa ya ndani, na syo kutoka kwa wahisani ambao wanatoa masharti ya jinsi ya kuzitumia kwa matakwa yao na ya nchi zao. Katika hili lazima wenye mamlaka wajue kwamba Tusikubali watu wetu washibishwe na Wazungu. Hebu sasa tujiulize kama watanzania, tuko wapi katika kilimo na tunataka kufika wapi?
  Suluhisho la jambo hili ni kuhakikisha kwamba mkulima analima kwa tija na anapata soko la uhakika kwa kuwekewa mazingira shirikishi katika kilimo chake. Hayo ni maoni yangu, toa maoni yako mkulimanamfugaji1@gmail.comukimlenga mkulima na kilimo chake ukilinganisha na wimbo huu  "kilimo ndio uti wa mgongo wa taifa"

No comments:

Post a Comment