Benki ya DCB yatoa mikopo kwa wajasiliamali wanawake
Benki ya DCB imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 47.5 kwa wanawake wajasiliamali 79, 464 katika kipindi cha mwaka jana, ikiwa ni jitihada za benki hiyo kuwainua kiuchumi na kupunguza umaskini.
Mikopo hiyo ilitolewa kati ya Januari na Desemba 31, 2014, kupitia huduma za mikopo ya vikundi, kwa wanawake katika wilaya zote tatu za mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa na Meneja wa Bidhaa na Masoko wa Benki ya DCB, Boyd Mwaisame, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana Tanzania, uliofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhudhuriwa na wanachama, maafisa wa benki na wajasiliamali.
Alisema benki hiyo inatoa huduma mbalimbali za mikopo kwa wajasiliamali wadogo na wa kati, huku akiwasihi watumie fursa hiyo kuomba mikopo ili kuendeleza shughuli zao.
“Tathmini ya kina imefanywa kuhusu huduma ya mikopo ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya waombaji (wajasiliamali wadogo na wa kati),” alisema Boyd.
Akielezea alisema mikopo kutoka benki ya DCB ina riba nafuu, hivyo kuwafanya wajasiliamali wadogo na wa kati kuweza kurejesha mikopo yao kwa muda na kuendeleza biashara zao kwa upande mwingine.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Wanawake na Vijana Tanzania, Sophia Mwakagenda, aliipongeza benki ya DCB kwa kudhamini mkutano huo na kuweka mikakati inayolenga kuboresha shughuli za
wajasiliamali wadogo na wa kati nchini.
inetolewa na ipp media
No comments:
Post a Comment