Wednesday, February 25, 2015

VODACOM NA TIGO WAUNGANA KUTOA HUDUMA BORA ZA KIFEDHA

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza (kushoto) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutia saini makubaliano ya kutoa huduma za kutuma na kupokea fedha na miamala mbalimbali ya malipo zinazotolewa na kampuni yake kupitia huduma ya M-Pesa na Tigo kupitia huduma yake ya Tigopesa. Anayeshuhudia kulia ni Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez.
Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kutia saini makubaliano ya kutoa huduma za kutuma na kupokea fedha na miamala mbalimbali ya malipo zinazotolewa na kampuni yake kupitia huduma ya Tigopesa na Vodacom kupitia huduma yake ya M-Pesa. Anaeshuhudia kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza.


Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza (kushoto, aliyekaa) na Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez (kulia, aliyekaa), wakitia saini mkataba wa makubaliano ya kutoa huduma za kutuma na kupokea fedha na miamala mbalimbali ya malipo zinazotolewa na makampuni yao kupitia huduma ya M-Pesa na Tigopesa. Wanaoshuhudia kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Vodacom Tanzania, Ngayama Matongo na kulia ni Meneja wa Chapa ya Tigo, William Mpinga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza (wa pili toka kushoto) na Meneja Mkuu wa Tigo Tanzania, Diego Gutierrez, wakibadilishana nakala za mkataba wa makubaliano ya kutoa huduma za kutuma na kupokea fedha na miamala mbalimbali ya malipo zinazotolewa na makampuni yao kupitia huduma ya M-Pesa na Tigopesa, wanaoshuhudia kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Vodacom Tanzania, Ngayama Matongo na kulia ni Meneja wa Chapa ya Tigo, William Mpinga.

Huduma za kutuma na kupokea  fedha na kufanya mihamala mbalimbali ya malipo zinazotolewa na makampuni ya Vodacom Tanzania kupitia huduma yake ya M-Pesa na Tigo kupitia huduma yake ya Tigopesa zitazidi kuimarika kutokana na makampuni hayo kuingia makubaliano ya kutoa huduma hizo kwa ushirikiano.Ushirikiano huo utawawezesha wateja wa  makampuni hayo kutuma na kupokea fedha na kufanya mihamala ya malipo moja kwa moja.

Makubaliano hayo ambayo yametangazwa leo yatawawezesha mamilioni ya wateja wanaotumia huduma za M-Pesa na Tigopesa kupata huduma kwa ubora zaidi kwa kuwa mteja akipokea au kutaka kutuma pesa au kufanya malipo hatolazimika kutoa fedha kwenye mtandao mmoja kwenda mwingine kama ilivyo sasa bali atafanya akitakacho moja kwa moja na bila kutozwa malipo ya ziada.

Akiongea leo  wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza alisema “Haya ni mapinduzi makubwa katika kutoa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi nchini Tanzania. Katika siku za karibuni wateja wa makampuni haya mawili wataweza kutuma na kupokea fedha na kufanya mihamala ya malipo mbalimbali moja kwa moja bila kulazimika kuzitoa kwa mawakala kwanza na kuziingiza kwenye huduma ya fedha ya mitandao yao kama ilivyo sasa.”

Wateja wa M-Pesa hivi sasa wanaweza  kulipia huduma mbalimbali baadhi yake zikiwa ni kulipia ving’amuzi vya televisheni zao, nauli za usafiri wa ndege, huduma za bima, huduma za maji na umeme, kodi mbalimbali za serikali, karo za shule, kurejesha mikopo katika mabenki na uchangiaji katika mifuko ya pensheni.

“Huduma hizi hivi sasa zinatumiwa na watu wengi na kwa kipindi cha miaka saba tangu zianzishwe zimeleta mapinduzi na kurahisisha maisha ya Watanzania kwa kiasi kikubwa. Tuna imani kwa kushirikiana na Tigo katika huduma hii  tutanufaisha wateja wa makampuni haya mawili kwa kiasi kikubwa na hivi sasa tuko katika mchakato wa kuboresha mfumo wetu wa M-Pesa ili ifikapo mwisho wa mwaka tutakapoanza kutoa huduma hizi pamoja kusiwepo na matatizo yoyote ya kimtandao na tutawekeza kiasi cha shilingi Bilioni 150/-kwa kazi hii,” alisema

Meza aliongeza kuwa kushirikiana kwa makampuni haya mawili katika kutoa huduma za pesa hakutaongeza gharama kwa watumiaji wa Tigopesa na M-Pesa bali kutawarahisishia kupata huduma bora na kwa karibu kutokana na mtandao mkubwa  wa makampuni haya mawili yanayotoa huduma za mawasiliano nchini.

“Tunachofanya hivi sasa ni makampuni haya kujipanga kuhakikisha yatakapoanza kutoa huduma za kifedha kwa pamoja mwishoni mwa mwaka huu yanatoa huduma za uhakika. Mtandao wetu wa mawakala  85,000 wa M-Pesa kwa sasa unahudumia zaidi ya wateja milioni 7 ambao wanafanya shughuli mbalimbali zinazochangia kukua kwa uchumi wa Taifa na tumejipanga kuhudumia wateja wengi zaidi kwenye miaka ya mbele,” alisema Meza.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo,Diego Gutierrez alisema ushirikiano huu utawanufaisha wateja wengi wa makampuni haya mawili na kuwarahishia maisha na kuwawezesha kufanya biashara zao vizuri wakati huo huo fedha zao zikiwa salama

“Tuna imani kwa kushirikiana na Vodacom katika huduma hii  tutanufaisha wateja wa makampuni haya mawili kwa kiasi kikubwa na tutahakikisha wateja wetu wanaendelea kupata huduma bora za kifedha kwa njia ya mtandao bila kuingia gharama ya ziada na tuna uzoefu wakufanya kazi katika ushirikiano kama huu kwa kuwa tayari tunashirrikiana na makapuni ya Airtel na Zantel na wateja wetu wanaendelea kufurahia huduma nzuru.Tunashukuru Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya IFC kwa kufanikisha utaratibu huu wa makampuni  haya kutoa huduma kwa pamoja ”.Alisema Gutierrez 

Huduma za M-Pesa na Tigo Pesa kwa sasa zinatumika  kulipia huduma mbalimbali baadhi yake zikiwa ni kulipia ving’amuzi vya televisheni zao, nauli za usafiri wa ndege, huduma za bima, huduma za maji na umeme, kodi mbalimbali za serikali, karo za shule, kurejesha mikopo katika mabenki na uchangiaji katika mifuko ya pensheni.

Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) limekuwa likiunga mkono kuimarishwa kwa huduma hizi za fedha kwa njia ya simu na  hicho ndicho chanzo cha makampuni haya kuingia makubaliano ya kuunganishwa kwa huduma hizi  nchini Tanzania ili kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake.

No comments:

Post a Comment