Wednesday, March 4, 2015

Fuga kondoo kisasa uboreshe pato lako

Katika eneo letu, idadi ya wafugaji wa kondoo imepungua sana, wakati idadi ya wanohitaji imeongezeka hasa raia wa kigeni, na bei iko juu. Naomba maelezo namna ya ufugaji bora wa kondoo.” – Ester Qwang, msomaji wa MkM,Babati

Kwa siku za nyuma, jumla ya idadi ya kondoo wanaofugwa hapa nchini Tanzania ilikaribiana kuwa sawa na idadi ya mbuzi nchini kote. Kwa sasa, idadi ya kondoo imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na idadi ya mbuzi. Hii imetokana na wafugaji kuhamishia mapenzi yao kwenye ufugaji wa mbuzi.

Kama walivyo mbuzi, kondoo pia wanaweza kufugwa na wafugaji wadogo wadogo na kwenye eneo dogo ambalo hutumika kwa kilimo pia. Kinachotakiwa ni namna ya kuongeza mazao na kuwa na ufanisi. Kwa kuzingatia yafuatayo, mfugaji wa kondoo ataweza kuwa na ufanisi mzuri.
Kondoo hupenda kujilisha kwenye makundi
Kondoo hupenda kujilisha kwenye makundi

Banda la kondoo

Banda na malazi ni lazima yawe mazuri na lenye nafasi ya kupitisha hewa vizuri, linaloweza kuwakinga mifugo dhidi ya mvua, jua na upepo. Sakafu iliyo nyanyuka ni nzuri zaidi.
Lakini sehemu ya mbele ya banda iwe na uwazi. Inashauriwa sakafu iwe na mwinuko kidogo.

Usafi

Ni lazima kinyesi kiondolewe kila siku ili kuweka banda katika hali ya usafi na ukavu kila wakati. Hii, itasaidia kuzuia magonjwa ambayo hushambulia kondoo mara kwa mara kama vile Pneumonia na kuoza kwato, pamoja na kupunguza uwezekano wa kuwepo wadudu nyemelezi.
Kwa kondoo wanaochungwa wakati wa mchana, banda la kawaida lililoezekwa linatosha kuwasitiri kondoo nyakati za usiku. Tenga walau skwea mita 1.5 kwa kila mnyama ili kuzuiuwezekano wa magonjwa yanayotokana na msongamano.

Kwa kondoo wanaolishwa ndani, inatakiwa:

• Sehemu kavu, banda lenye hewa na kuezekwa vizuri (skwea mita 2)
• Kihondi kizuri cha kulishia ili kufanya malisho kuwa safi na kupunguza uharibifu.
• Sehemu nzuri ya nje inayowafaa kondoo kutembea. Tenga walau skwea mita 3 kwa kila kondoo. Kila mwanakondoo anahitaji eneo la kutosha kwa ajili ya kukimbia na kucheza.
• Maji safi na jiwe la chumvi vinahitajika kuwepo wakati wote.
• Utahitajika kuwa na banda la ziada ama kwa muda kwa ajili ya kondoo wenye mimba, kuzalia na kwa ajili ya wanakondoo. Pia, kwa kondoo wanaoumwa.
• Banda la uzio kwa ajili ya kondoo unaweza kuwa rahisi zaidi kwa kuwa kondoo hawaruki wala kupanda juu.

Virutubisho kwa ajili ya kondoo

Kondoo hutumia muda mwingi wakati wa mchana kula majani na baadaye hucheua na kutafuna. Wanapendelea zaidi kula majani na vichaka ambavyo vina mchanganyiko wa madawa ya asili. Wanakondoo hujifunza kutoka kwa mama zao ni nini chakula. Kama unawaanzishia aina mpya ya chakula, lisha kwa kiasi kidogo na uweke kwenye sehemu walikozoea kulishiwa.
Kuwa makini na ukumbuke kuwa wanyama wanaopata lishe duni ni rahisi kushambuliwa na magonjwa na hawana uwezo wa kukabiliana na vimelea vya magonjwa. Kondoo jike asiyelishwa vizuri hawezi kubeba mimba. Uzalishaji wa maziwa pia huwa kidogo kiasi cha kufanya watoto wake kuwa dhaifu na kukua kwa shida.

Kuchunga

Kwa kawaida kondoo wanapenda kulisha kwa kula ardhini, lakini wanakula aina tofauti za majani. Kondoo na ng’ombe wanakuwa na muunganiko na kundi zuri la kujilisha kwa kula majani yaliyomo ardhini. Hii inatokana na kuwa wanyama hawa hushambuliwa na wadudu na magonjwa tofauti na hakuna anayedhuru mwingine. Kondoo hawaogopi mvua kama walivyo mbuzi, lakini kusimama kwenye matope husababisha ugonjwa wa miguu na kuoza kwato.

Ili kuepuka kulisha kupitiliza katika eneo moja, jambo linaloweza kutengeneza na kusababisha vimelea, usiwaache kondoo wako kula sehemu moja kwa muda mrefu zaidi ya wiki 2.

Kila kipande cha uwanda kinatakiwa kuachwa bila kulishiwa kondoo au mbuzi kwa kipindi cha wiki sita. Unahitaji kuwa na walau vipande 4 vya uwanda kwa ajili ya kuchungia kwa mzunguko. Hekari moja yenye malisho mazuri, ni lazima itoe malisho ya kutosha walau kwa kondoo wanne na watoto wao. Gawanya eneo unalohitaji kwa ajili ya kondoo wako mara nne kisha ulishe kwa mzunguko katika eneo hilo.

Kwenye eneo lenye malisho duni unahitaji kuwapatia kondoo eneo kubwa zaidi, na pengine kuwaongezea chakula chenye virutubisho. Tumia majani ya malisho anayozidi wakati wa mvua kutengeneza hay kwa ajili ya kulishia wakati wa kiangazi.

No comments:

Post a Comment