Saturday, March 7, 2015

Kilimo cha ufuta chawainua wakulima Babati

“Kabla ya kujishughulisha na kilimo cha ufuta, nilikuwa na hali ngumu kiuchumi, nilikuwa nalima karanga na pamba, ila sasa nalima ufuta na nimejenga nyumba bora ya kisasa, nafuga ng’ombe, kuku na kusomesha watoto.”
Hayo ni maneno ya mmoja wakulima wa ufuta wa Kijiji cha Mwada, Tarafa ya Mbugwe, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Theresia Wilbroad Njaiko ambaye anaeleza faida alizopata baada ya kulima ufuta.
Njaiko anasema baada ya kupata mafunzo ya kulima ufuta kutoka Shirika la Food and Agricultural Research Management (Farm Africa), amenufaika kiuchumi tofauti na awali.
Anasema alianza kulima ekari moja ya ufuta mwaka 1995 na mwaka 2009 Shirika la Farm Africa lilitoa mafunzo ya kilimo bora cha ufuta kwa vikundi viwili vya Nsange na Bessi vyenye wakulima 40.
Anasema msimu uliopita amevuna magunia 10 ya ufuta baada ya kutumia mbegu za Naliendele, Ziada na Lindi White alizopatiwa na Farm Africa na kuuza gunia moja kwa Sh240,000 na kupata Sh2.4 milioni.
Mkulima huyo anatoa ombi kwa Serikali kuanzisha bodi ya zao la ufuta kama ilivyoanzisha bodi ya mazao ya pamba, kahawa na katani ili kuwainua wakulima kiuchumi wa zao la ufuta.
Naye, mkazi wa Kijiji cha Magugu, Khadija Juma ambaye analima ufuta, anaimani kwamba Shirika la Farm Africa litaendelea kuwapatia elimu ya kilimo hicho, mbegu, dawa na kuwatafutia masoko.
“Hivi sasa mkulima amegeukia kilimo cha ufuta kwani kimemuinua, mimi nimefanikiwa kujenga nyumba bora ya kuishi, mwanangu amehitimu kidato cha nne na hivi karibuni anatarajia kuendelea na masomo ya chuo,” anasema Khadija.
Mkulima wa Kijiji cha Magugu, Tabu Issa ameiomba Serikali kutupia jicho kwenye zao hilo, kwani hivi sasa wakulima wengi wamefaidika kupitia ufuta.
“Sasa tunatengeneza sabuni ambayo inaondoa harara na kutengeneza mafuta ya kupikia yasiyo na lehemu, kashata pamoja na unga wa lishe,” anasema.
Kwa upande wake, mkulima wa Kijiji cha Mwada Lucas Said anasema Shirika la Farm Africa linawapatia mbegu na kuwatafutia soko la ufuta.


Naye, Ofisa Masoko wa mradi wa ufuta wa Farm Africa, Rahel Pazzia anasema wakulima wanatarajia kunufaika baada ya kuwatafutia wakulima soko la ufuta India, Uholanzi na China.

No comments:

Post a Comment