Tuesday, March 3, 2015

KUKU WEUSI KUTOKA MALAWI TEGEMEO KWA WAJASIRIAMALI


NA ADAM MALINDA
*Wanakua na kufikia uzito wa kilo 4
UJASIRIAMALI ni jambo jema katika mapambano dhidi ya umasikini, lakini pia ili kuweza kuwa mjasiriamali, yanahitajika maarifa ya ziada, ikiwamo ubunifu katika kuboresha shughuli unazozifanya ili ziwe na tija.
Nilipomtembelea kijana Peter Kitembe nyumbani kwao Mburahati Jijini Dar es Salaam, aliniambia anamiliki kampuni ya kifamilia iitwayo Peace Poultry Farm, ambapo alinisimulia kilichomsukuma kuingia katika ujasiriamali wa kufuga kuku wa kienyeji.

“Nilikuwa katika kampuni moja ya kutengeneza chakula cha kuku ambayo ilinipa changamoto za kimawazo, nikajiuliza, kwa nini nami nisiwe mmoja wa wafugaji wanaoweza kuinua hali ya kipato na kuupiga vita umasikini,” alianza kueleza kijana huyo.

Kitembe alisema amekuwa akisukumwa na hali ya umasikini ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakiamka asubuhi na mapema kuwahi maeneo mbalimbali kujitafutia fedha za kujikimu, lakini wakirudi nyakati za usiku wanakuwa hoi, hali inayowafanya baadhi yao kukata tamaa na wengine wanaamua kukaza buti hadi kupata mafanikio.


“Nilianza kufuga kuku Mei 10, mwaka 2010, kwa kuanzia na vifaranga 67, kati ya hivyo, viwili vilikufa na kubakiwa na kuku 65, ambao kizazi hicho kimeniwezesha kuwa na kuku zaidi ya 1,500 sasa,” alisema Kitembe.



Akielezea aina ya kuku anaowafuga, alisema amekuwa akifuatilia aina mbalimbali za kuku wa kienyeji na akaridhia kufuga aina moja iitwayo kuchi, hao ni jamii ya kuku wanaofugwa katika mikoa ya kanda ya kati na Ziwa Victoria wenye umbile kubwa na nyama tamu inayopendwa na watu wengi.

Anabainisha kuwa amekuwa na mawasiliano na wafugaji wa nchi jirani ambapo alipata mbegu ya kuku weusi kutoka Malawi ambao sasa wameonekana kufanya vizuri katika utagaji wa mayai ya kienyeji na ukuaji unaowafanya kufikia uzito wa kilo tatu hadi nne.

Kitembe anadai kupata mafanikio makubwa katika uamuzi wake wa kuingia katika ujasiriamali kwa msaada na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wanafamilia wenzake na hasa baba yake, Mzee George Kitembe.

“Changamoto iliyonikabili ni namna ya kuwa na eneo la kufugia, kuwa na uwezo wa kununua chakula cha kuku, na usimamizi, ambapo baba yangu na mama walikubali niendeshe shughuli hizi katika eneo lao,” anasema Kitembe.

Anaeleza awali alipata shida alipokuwa anahitaji kupata chakula cha kuwapa kuku waliokuwa wakiongezeka kwa kasi, huku akiwa hana fedha za kununulia chakula.

Anasema alitumia kinu kutwanga chakula, hali iliyomsababisha kuchubuka mikono na kumsababishia maumivu makali, hali iliyomlazimu kubandika plasta katika mikono yake na kuendelea na kazi hiyo ili aweze kupata chakula cha kutosheleza mifugo yake.

Hakuishia hapo, alibuni njia nyingine ambapo alitumia ujuzi na uzoefu alioupata katika kampuni ya kutengeneza chakula cha kuku kwa kufanya utafiti wa chakula bora na kukipeleka kwa wataalamu wa wizara ya mifugo kuona kama kinafaa kulisha kuku, ndipo alipoidhinishiwa kuwa kinafaa.

Alisema changamoto kubwa iliyo mbele yake ni namna ya kupata fedha, malighafi za kutengenezea chakula na namna ya kusaga chakula kwa wingi ili kutosheleza kuku alionao.

Anadai kwa bahati nzuri aliweza kuuza mayai, na mwisho alipata fedha za kununulia mashine ndogo ya mkono, ambayo sasa inasaga chakula kingi anachoweza kukiuza kwa wafugaji wengine.

“Unajua mwandishi katika kipindi cha mwezi wa Juni, hadi Oktoba, dagaa hupanda bei na Ziwa Victoria ni pekee linalotoa dagaa wengi katika nchi za Afrika mashariki na kati, hivyo kushindwa kutosheleza mahitaji ya walaji na kusababisha sisi wafugaji kununua bei ya juu,” alisema Kitembe.

Anasema, amejivunia tafiti mbili kubwa za ubunifu wa kutengeneza chakula bora cha kuku chenye gharama nafuu ambapo amefanikiwa, hali inayomwezesha kupunguza gharama za uzalishaji.

Anafafanua kuwa, ufugaji una changamoto kubwa hasa kwa upande wa gharama za chakula na magonjwa yanayowasumbua kuku wa kisasa na kienyeji, jambo ambalo huwatia woga wajasiriamali wengi kuingia katika sekta ya ufugaji kuku.

“Kinachotakiwa kuzingatiwa ni kuwapa chanjo kwa wakati husika, kama vile ‘malex’, ‘new casstle’ ‘Gombollo’ na nyinginezo, vinginevyo ufugaji unaweza kuwa sekta isiyowezekana.

Anasema, ukuaji kuku ni kati ya miezi 4 na wiki mbili ambapo kama ni mtetea utaanza kutaga ama kama ni jogoo ataanza kuwika.

Akielezea zaidi kuhusu kuku hao wanavyoweza kuwa na tofauti kubwa na kuku wa kisasa, Kuchi huweza kustahimili hali zote katika mazingira ya nchi za kitropikali, sanjari na kuku weusi wa kutoka nchini Malawi ambao wana kasi kubwa ya kutaga na kuwa na umbile kubwa linalofaa kwa nyama.

Anafafanua faida zinazoweza kupatikana kwa kufuga kuku kuchi na wale wenye mbegu nyeusi ya Malawi, kuku mmoja kwa makadirio ya chini anaweza kutaga mayai 15 ambapo yakitotolewa katika mashine kwa siku 21, utakuwa umepata kuku 15 kwa miezi 4 na wiki mbili ukiongeza mwezi mmoja wa mama kutaga na wiki 3 za kutotolewa mfugaji.

Anazama zaidi kwa kusema kuwa mfugaji anavyoweza kupata faida maradufu kutokana na kufuga kuku hao weusi wa mayai na nyama pamoja na kuchi, kuwa mfugaji atakuwa na kuku mmoja, baada ya miezi 6 anakuwa na kuku 15, baada ya miezi 6 mingine wanakuwa wakubwa tayari kwa kuuzwa.

“Utaona kuku mmoja amemuwezesha kupata kuku 15 kwa mwaka, mfugaji mwenye uwezo wa kufuga kuku 100 atakuwa na kuku 1500 ambao akiwauza kwa Sh 10,000 kila mmoja atakuwa amejipatia Sh milioni 15, ni dhahili huyo atakuwa ameuaga umasikini,” anasema Kitembe.

Anasema yeye kwa sasa ana mashine ya kutotolea vifaranga 4,800 kwa wakati mmoja, hivyo anachofanya sasa ni kutotolesha mayai ya wateja kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa bei nafuu.

Akizungunzia namna anavyokusudia kuwasaidia wajasiriamali wenzake wenye lengo la kuondokana na umasikini, anasema wameanzisha kituo cha utoaji elimu ya ujasiriamali na mawasiliano ili kuwawezesha wafugaji kuelewa namna ya hatua za ufugaji zinavyoandaliwa na kuweza kumkomboa.

“Pale maeneo ya External njia iendayo jeshini tumefungua kituo cha kutoa elimu ya ujasiriamali cha ICT4 TD Leaning Centre, ambacho kinalenga kumpa maarifa na mbinu za ujasiriamali mfugaji na wengine wanaotaka kujikomboa na umasikini,” anasema Kitembe.

Alitolea mfano wa Bi Joyce Mnyanga, mkazi wa Ubungo (EPZA) ambaye ameweza kufuga kuku weusi wa mayai na nyama kutoka nchini Malawi ambao wamemtoa katika umasikini na kuwa miongoni mwa akina mama waliopiga hatua kimaendeleo kwa kufuga kuku zaidi ya 800, ambazo zimemwezesha kupata mayai na fedha za kutosha.

Amewaasa wafugaji kutumia mbegu ya kuku hao kwa kuwa wamekuwa wavumilivu katika maambukizo ya magonjwa yanayosumbua kwa miaka mingi ambapo baadhi ya wafugaji walikata tamaa na kuacha ufugaji.

No comments:

Post a Comment