Friday, March 6, 2015

Kilimo cha Njugu


Njugu ni mbegu za mmea wa njugu. Mmea huo unapoendelea kusitawi huwa unachanua maua ya manjano ambayo hujichavusha yenyewe.
Ovari iliyotiwa mbegu ya kiume ambayo iko kwenye ncha ya shina ya mmea huo huanza kuingia udongoni. Ovari hiyo huwa na mbegu. Mbegu hiyo inapoingia udongoni, hukua sambamba na udongo wa juu, halafu inakomaa ikielekea chini. Kisha mbegu hiyo inakuwa njugu. Mmea mmoja unaweza kuwa na njugu 40.
Njugu husitawi vizuri katika maeneo yenye joto na mvua ya wastani. Kuna kipindi cha siku 120 au 160 kati ya wakati wa kupanda na kuvuna, ikitegemea aina ya njugu na hali ya hewa. Wakati wa kuvuna, ni lazima wakulima wa njugu wachimbue mimea hiyo na kuipindua, halafu wanaiacha ikauke ili isioze wakati inapohifadhiwa. Siku hizi, wakulima wengi hutumia mashine za kilimo za kisasa zinazowawezesha kuchimbua mimea hiyo, kuikung’uta, na kuipindua kwa wakati mmoja.
Matumizi Mengi ya Njugu
Njugu ni chakula chenye virutubisho vingi sana. Njugu husaidia sana umeng’enyaji wa chakula, na zina vitamini 13 na madini 26. Vingi kati ya virutubisho hivyo havipatikani katika vyakula vya kisasa. Kitabu The Encyclopædia Britannica kinasema: “Njugu zina protini nyingi zaidi, madini mengi zaidi, na vitamini nyingi kuliko maini ya ng’ombe.” Lakini watu wanaotaka kupunguza uzito wao wanapaswa kutahadhari! Njugu zina “mafuta mengi kuliko malai nzito” na “kalori nyingi kuliko sukari.”
Njugu hutumiwa katika vyakula vingi vinavyopikwa katika nchi nyingi na ni rahisi sana kutambua ladha yake. Anya von Bremzen, mwandishi katika fani ya upishi, anasema: “Ladha ya njugu ni tamu sana na haina kifani, kwa hiyo chakula chochote kilichotiwa njugu kitakuwa na ladha kama ya njugu. Kwa hiyo, uwe ni mchuzi wa njugu wa Indonesia, supu ya Afrika Magharibi, spageti za Kichina, kitoweo cha Peru, au mkate uliopakwa siagi ya njugu, ladha ni ileile.”
Vilevile, njugu ni kitafuno kinachopendwa na wengi kotekote ulimwenguni. Kwa mfano, huko India njugu huchanganywa na maharagwe makavu na kuuzwa barabarani. Kulingana na kitabu The Great American Peanut, inasemekana kwamba siagi ya njugu, ambayo hupakwa kwenye mkate katika nchi kadhaa, “ilivumbuliwa na daktari mmoja kutoka St. Louis [Marekani] wapata mwaka wa 1890 kwa madhumuni ya kutunza afya ya watu wazee.”
Lakini mbali na kutumiwa kama chakula, njugu zina matumizi mengineyo. Katika bara lote la Asia, njugu hutumiwa kutengeneza mafuta ya kupikia. Mafuta ya njugu yanaweza kutumiwa pia kupikia vyakula vinavyohitaji kupikwa kwa moto mkali, na hayapati harufu ya vyakula vinavyopikwa.
Huko Brazili, masalio ya njugu zilizotumiwa kutengeneza mafuta ya kupikia hutumiwa kutengeneza chakula cha mifugo. Na bidhaa nyingi hutengenezwa kutokana na njugu.—Ona maelezo yaliyo juu.
Jihadhari na Mizio ya Njugu!
Njugu zinaweza kukaa kwa muda mrefu bila kuhifadhiwa kwenye friji. Hata hivyo, tunapaswa kutahadhari. Njugu ambazo zimeanza kupata kuvu zina kemikali hatari inayoitwa aflatoxin ambayo ina uwezo mkubwa wa kusababisha kansa. Isitoshe, watu wengine wana mizio ya njugu. Wanapokula njugu ‘wanaweza kutokwa na kamasi puani na kupata vipele au kuathiriwa mwili mzima (anaphylactic shock),’ lasema gazeti Prevention.Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba siku hizi watoto wengi zaidi wanapata mizio ya njugu.
Gazeti Prevention linaripoti kwamba ikiwa wazazi wote wawili wana ugonjwa wa pumu, mzio wa kupata uvimbe puani, au ukurutu, kuna uwezekano mkubwa kwamba mtoto wao atapata mzio wa njugu.
Jambo hilo pia linawahusu watoto ambao mama zao wana mizio na pia watoto wanaopata mzio wa maziwa kabla ya kufikia umri wa mwaka mmoja. Dakt. Hugh Sampson, profesa wa magonjwa ya watoto kwenye Kituo cha Kitiba cha Chuo Kikuu cha Johns Hopkins huko Marekani, anasema: “Ni afadhali wazazi wasiwape watoto wao siagi ya njugu hadi wanapofikia umri wa miaka mitatu.”
Iwe unapenda njugu au la, huenda mazungumzo haya kuhusu matumizi yake mengi yamekufanya uthamini mbegu hiyo ndogo inayopendwa na wengi.

No comments:

Post a Comment