Wednesday, March 4, 2015

Liki: Zao lisiloshambuliwa na magonjwa

Ni vyema kuchagua aina ya mazao ambayo hayana gharama kubwa kuzalisha, wakati huo huo yakiwa na faidi kubwa.

allium_porrumLiki ni moja ya mazao ya mbogamboga ambayo yanapata umaarufu mkubwa nchini Tanzania, kutokana na kuzalishwa katika maeneo mengi, na kuwa na soko la uhakika. Zao hili ni moja kati ya mazao ya mboga ambayo yanaweza kuachwa shambani kwa muda mrefu baada ya kukomaa, ili kusubiri soko endapo kuna tatizo katika soko ikiwa ni pamoja na bei ya kuuzia.

Namna ya kuzalisha liki
Utayarishaji wa shamba: Baada ya kufanya maamuzi ya eneo utakalopanda liki, hakikisha kuwa eneo hilo limelimwa vizuri. Ondoa taka zote zisizohitajika shambani, ikiwa ni pamoja na magugu yanayoweza kurudia kuota baada ya muda fulani.

Kusia mbegu: Baada ya kufanya maandalizi muhimu ya shamba, tengeneza matuta kwa ajili ya kusia mbegu.

Hakikisha kuwa udongo unaokusudiwa kutengeneza matuta, umechanganywa na mbolea mboji ambayo imeiva vizuri. Utengenezaji wa matuta hutegemeana na hali ya hewa kwa kipindi unachojiandaa kusia mbegu. Wakati wa msimu wa mvua, tengeneza matuta mwinuko. Hii itasaidia maji yasituame kwenye kitalu na kuozesha miche.

Katika msimu wa kiangazi, ni muhimu kutengeneza matuta mbonyeo. Hii itasaidia katika uhifadhi wa maji na kufanya kitalu kiwe na unyevu utakaosaidia miche kukua vizuri.

Baada ya kuandaa matuta kulingana na mahitaji, sia mbegu zako kwa mstari. Unaweza kuchora kwa kutumia kijiti na kina kisiwe kirefu sana ili kuepusha mbegu kushindwa kutokeza juu ya ardhi. Baada ya siku 7 tangu kusia, mbegu zitakuwa zimeota.

Matunzo: Palilia na kuhakikisha kuwa tuta lenye miche ni safi wakati wote, ili kuepusha uwezekana wa kuwepovimelea na magonjwa. Pia ni muhimu kuhakikisha tuta lina unyevu wakati wote.

Kupanda shambani: Hakikisha kuwa shamba limelimwa na kuandaliwa vizuri wiki mbili kabla ya muda wa kupanda liki shambani. Miche ihamishiwe shambani inapokuwa na urefu wa sentimita 15-20. Liki itakuwa na ufanisi zaidi endapo itapandwa kwenye matuta ya kina kirefu ambayo yanakuwa yameshaandaliwa tayari kabla ya muda wa kupanda liki kutoka sehemu iliposiwa.

Nafasi: Tumia kijiti kutoboa shimo kwa ajili ya kupandia miche ya liki. Nafasi kati ya mche na mche iwe ni sentimita 15. Kati ya mstari na mstari iwe ni sentimita 30.

Tumbukiza mche wa liki kwenye shimo kwa uangalifu ili mizizi isiumie na kusababisha kutokuota vizuri. Tumia vidole vyako kuhakikisha kuwa mizizi imezama kwenye shimo vizuri. Funika vizuri kuhakikisha kuwa udongo hautamomonyolewa na maji utakapokuwa unamwagilia.

Palizi: Hakikisha kuwa unapalilia shamba vizuri kila magugu yanapoota. Hii itasaidia liki kukua vizuri bila kuwa na mashindano ya kupata virutubisho na maji kati yake na magugu. Unaweza kutandaza mbolea kavu shambani kuzuia magugu yasiote, lakini pia itasaidia kufukuza wadudu wanaoweza kusababisha uharibifu, ingawa zao la liki halina wadudu wanaolishambulia.

Wadudu na magonjwa: Nchini Tanzania zao hili bado halijawahi kupata tatizo la wadudu wala magonjwa.

Kuvuna: Unaweza kuanza kuvuna liki miezi minne tangu ilipopandwa, ingawa inaweza kuendelea kukaa shambani kwa muda mrefu zaidi kutegemeana na mahitaji na hali ya soko.

Soko: Soko la liki lipo kipindi chote cha mwaka, kwa kuwa mahitaji yake ni ya kila siku.

Matumizi: Liki hutumika kama kiungo kwenye vyakula vya aina mbalimbali. Pia inaaminika kuwa zaoo hili linasaidia sana kwa watu walioko kwenye mpango wa kupunguza uzito wa miili.

No comments:

Post a Comment