Monday, March 2, 2015

Jikinge na Kansa kwa Kula Vyakula Asilia


Kwa  mujibu  wa  tafiti  mbalimbali  duniani, ugonjwa  wa  kansa  unatajwa  kuwa  ndio  ugonjwa  wa  hatari  zaidi  pengine  kuliko  ugonjwa  mwingine  wowote  uliowahi  kutokea  katika  historia  ya  mwanadamu. Nchini   Tanzania  pekee  kiasi cha watu 100 hufariki dunia KILA SIKU kutokana na magonjwa ya saratani, hii  ni  kwa  mujibu  wa  taarifa  ya  Taasisi  ya  Saratani  ya  Hospitali  ya  Ocean  Road a  jijini  Dar  es  salaam  kupitia  Mkurugenzi  wake  Dk. Twalib  Ngoma.
Hali ni  mbaya  zaidi katika  nchi  zilizoendelea   ambako  tunataarifiwa  ya  kwamba   kuna  idadi  kubwa  sana  ya  watu  wanaopoteza  maisha  yao  kila  siku  kutokana  na  magonjwa  ya  kansa ambayo  kimsingi  yanasababishwa na  na ulaji wa vyakula tunavyokula kila siku. Mfano  nchini  Marekani  pekee  karibu  theluthi  moja  ya  wagonjwa  wa  kansa  inasababishwa  na  vyakula  wanavyokula  kila  siku, na  hii  ni  kwa  mujibu  wa Taasisi  ya  Saratani  ya  nchini  Marekani. 
Pamoja na kuwepo habari hiyo mbaya na ya kusikitisha ya kupoteza mamia ya ndugu zetu kila siku, kuna habari njema pia kuwa unaweza kabisa kujikinga na ugonjwa huu hatari kwa kula vyakula vinavyostahili na kuepuka vinavyochangia saratani.

Kwa leo hebu tuangalie orodha ya baadhi ya vyakula ambavyo vinaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kupambanana seli zinazosababisha saratani mwilini. Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuzuia na Kutibu Saratani, DK. Richard Béliveauwa Chuo Kikuu cha Québec, Montreal Canada, anasema kuwa tafiti zote zinaonesha kuwa kinga ya saratani iko kwenye ulaji wa vyakula vitokanavyo na mimea (Plant-based foods).
Unachotakiwa kufanya ili kuupa mwili wako kinga dhidi ya saratani, kula matunda na mboga za majani za aina mbalimbali kila siku, hasa hizi zifuatazo:

BROKOLI (BROCCOLI)
Brokoli
Hii ni aina fulani ya mboga ya majani, iko kama maua ya maboga au uyoga, inapatikana katika masoko mengi makubwa nchini. Aina hii ya mboga inaelezwa kuwa na kiasi kingi cha kirutubisho aina ya ‘sulforaphane’ ambacho uwezo wake wa kutoa kinga ni mkubwa. Inatoa kinga dhidi ya saratani ya matiti, ini, mapafu, kibofu, ngozi, tumbo na kizazi.

BERI (BERRIES)
Beri
Haya ni matunda maarufu ambayo hujulikana pia kama matunda ya kuongeza damu au ‘matunda damu’ kutokana na kuwa na rangi nyekundu na mengine meusi na kijani. Ulaji wa matunda haya hutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo, koo, mdomo na ngozi.

NYANYA (TOMATOES)
Nyanya
Wengi tunaidharau nyanya na kuipuuzia kwa kutoila katika milo yetu ya kila siku, wakati nyanya ziko nyingi kiasi zingine zinaoza mitaani. Nyanya inaelezwa kuwa na kirutubisho aina ya ‘Lycopene’ ambacho kina uwezo mkubwa wa kuzuia saratani ya kizazi ambayo nchini Marekani inaua zaidi ya watu 8,000 kila mwaka, kwa Tanzania hali ni mbaya zaidi. Nyanya huzuia pia saratani ya mapafu, tumbo na kibofu.

KITUNGUU SAUMU (GARLIC)
Saumu
Faida za kitunguu saumu zipo nyingi, lakini miongoni mwa hizo faida ni kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani. Kwa kuweka mazoea ya kula mara kwa mara, kwa kuchanganya katika mlo wako au saladi yako utakuwa umejijengea kinga mwilini. Hutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo, matita, koo na tumbo kwa ujumla.

MAHARAGE (BEANS)
Beans
Wengi wetu hatupendi kula maharage tukiamini ni mboga ya kimaskini! Ukweli ni kwamba maharage ni mboga muhimu na ina faida nyingi mwilini, ikiwemo kutoa kinga dhidi ya saratani ya utumbo na matiti. Utafiti kuhusu faida za maharage uliofanywa na Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani umethibitisha faida hizo.

Kwa ujumla, magonjwa ya saratani yanaweza kuepukwa iwapo mtu atazingatia ulaji wa mboga na matunda asilia kila siku na kujiepusha na ulaji wa vyakula vya ‘kutengeneza’. Wiki ijayo nitakuletea orodha ya vyakula vinavyosababisha saratani ambavyo unatakiwa kuviepuka kama ukoma!

No comments:

Post a Comment