Sunday, March 1, 2015

Tanzania sasa yagundua mbegu mpya ya mahindi

Kilosa. Wataalamu wa kilimo nchini wamegundua aina tatu mpya za mbegu za mahindi ambazo zina uwezo wa kuvumilia ukame.
Mratibu wa Mradi wa Utafiti wa Mahindi Yanayohimili Ukame Afrika (Wema) Tawi la Tanzania, Dk Alois Kulaya alisema ugunduzi huo ni ukombozi kwa wakulima wadogo ambao ndiyo wanaathirika zaidi na ukame.
“Lengo letu wakulima wadodogo wawe na uwezo wa kuzalisha zaidi,” alisema Dk Kulaya.
Alisema katika majaribio yaliyofanyika sehemu mbalimbali nchini, yalionyesha mvua zikinyesha inavyotakiwa mkulima akitumia mbegu hizo anaweza kuvuna wastani wa tani nane kwa hekta moja.
“Lakini kama kutakuwa na mvua kidogo watavuna wastani wa tani nne kwa hekta,” alisema Dk Kulaya.
Dk Kulaya alizitaja mbegu hizo mpya kuwa ni WE2113, WE2109 na WE2112 na wanatarajia zitawafikia wakulima 
“Tunatarajia wakulima wataanza kuzitumia msimu wa kilimo mwaka 2015,” alisema.
Alisema hivi sasa mbegu hizo zinapelekwa kwa kampuni za uzalishaji mbegu, ambazo zitazizalisha na kuzifunga kitaalamu tayari kusambazwa kwa wakulima nchini.
Akizindua mbegu hizo, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Fidelis Myaka aliahidi Serikali kuendelea kuwa na watafiti wa kilimo ili kufanikisha uboreshaji kilimo nchini.
Dk Myaka alisema tangu Tanzania ianze kuathirika na Mabadiliko ya Tabianchi, wakulima wengi wamekuwa wakiyumba kutokana na kutegemea kilimo cha mvua.
Kwa sababu hiyo, alisema ugunduzi huo utasaidia kuinua hali ya maisha ya wakulima hasa kukabiliana na tatizo la ukame ambalo limekuwa likisababisha ukosefu wa chakula nchini mara kwa mara.
Alisema lengo ni kumkwamua mkulima ili kuongeza uzalishaji.

No comments:

Post a Comment